Mawanda ya taaluma ya  isimujamii

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Tuesday, February 17  2015 at  11:25

Kwa Muhtasari

Isimujamii ni tawi la isimu linalochunguza uhusiano na mtagusano au mwingiliano baina ya lugha na jamii, matumizi ya lugha hiyo pamoja na miundo na mikondo ambayo kwayo watumizi wa lugha hiyo huishi. Kwa hivyo inahusu eneo la kijeografia, umri wa matumizi na jinsia, matabaka za watumizi wa lugha.

 

MOJAWAPO wa masomo yanayofundishwa katika Kiswahili  kwenye ngazi ya shule za upili na vyuo vikuu ni isimujamii. Isimujamii ni tawi la isimu linalochunguza uhusiano na mtagusano au mwingiliano baina ya lugha na jamii, matumizi ya lugha hiyo pamoja na miundo na mikondo ambayo kwayo watumizi wa lugha hiyo huishi. Lugha ni nyenzo muhimu sana katika mawasiliano na ni chombo kinachosheheni fikra, maarifa, utamaduni na mbeko za binadamu. Mumo kwa mumo katika lugha ya binadamu mna utamaduni wake.

Utamaduni unafumbata maisha ya mtu na jinsi anavyoyaishi. Inapotokea kwamba watu wananyimwa lugha yao, huwa kwa hakika ni kana kwamba watu hao huwa wameachwa uchi. Lugha hivyo basi hutumiwa kwa mitindo tofauti, mahali tofauti kama vile mahakamani, kwenye vyombo vya habari, misikitini na makanisani  -au maeneo ya maabadi, sokoni na kadhalika. Lakini ikumbukwe kwamba, lengo la matumizi ya lugha – licha ya kutumika katika mazingira na miktadha tofauti huwa ni kuwasiliana.

Lugha pia inaweza kutumika kwa namna ambayo inatinga mawasiliano. Kwa hivyo ni bayana kwamba  hapana njia moja mahususi ya kutumia lugha. Mtu mmoja hutumia lugha kwa mtindo wa pekee anapolinganishwa na mtu mwingine, lugha hutumika kama chombo cha kijitambulisha katika ngazi za ukabila, taifa na maeneo ya kijiografia. Lugha kwa upande mwingine ina uwezo wa kuwaunganisha watu au hata kuwatenganisha kabisa. Lugha vipindi za Sheng na Engsh kwa mfano ni kitambulisho kikubwa sana miongoni mwa vijana nchini Kenya.

Kiswahili  sanifu kwa upande mwingine ni lugha ambayo inaaminika kuwa na uwezo wa kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa taifa la Kenya lenye zaidi ya ndimi 42. Tanzania ambayo ina makabila zaidi ya 100 imefanikiwa kuibua mshikamano na utaifa wa namna fulani.Si mara zote ambapo nchi yenye lugha moja inaleta mshikamano wa taifa. Nchi ya Somalia ina lugha moja tu – Kisomali. Hata hivyo, nchi hiyo haijakuwa na utaifa wowote kwa zaidi ya miongo miwili. Hii ina maana gani? Ina maana kwamba mumo kwa mumo katika taifa moja, kuna makundi yanayopigania maslahi mbalimbali ambayo huzua mikinzano na tofauti ambazo haziwezi kusuluhishwa kwa urahisi kwa matumizi ya lugha. Mara nyingi mikinzano hii huwa ni ya siasa, uchumi na jamii.

Maswali

 Kwa hiyo, isimujamii ni taaluma ambayo huuliza maswali yafuatayo ya kimsingi: Je, eneo fulani kijiografia (wilaya, mkoa, nchi au bara) lina lugha ngapi na lugha hizo ni zipi? Je, watu wa umri  na jinsia tofauri hutumia lugha kwa  njia sawa au kuna tofauti. Je, lugha katika nchi au eneo fulani zimepangiwa vupi? Kuna zile zilizoteuliwa na kuendelezwa au kustawishwa kimakusudi? Je, lugha zilizopo zinaimarika au zinafifia au kufa? Je, kuna taasisi maalumu za serikali zinazojishughulisha na shughuli za ustawishaji wa lugha? Je, lahaja husababishwa na nini? Je, kuna mpaka upi baina ya lugha na lahaja?

Haya na mengine mengi ni maswali ya kimsingi ambayo mtaalamu wa isimujamii hujiuliza. Baadhi ya majibu ya  maswali haya humwelekeza  mtaalamu wa isimujamii kwenye ukweli kwamba, katika uhalisia wa mambo, lugha husawiri matabaka katika jamii, mitindo ya lugha hudhibitiwa na mahitaji ya jamii, lugha ndiyo kibebeo cha mitazamo na falsafa za jamii, kuna misimbo mbalimbali katika matumizi ya lugha katika jamii na hata  mabadiliko katika jamii hushurutisha lugha kubadilika pia.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuka

mwagechure@gmail.com