Matatizo ya uainishaji wa tanzu za kifasihi

Imepakiwa Thursday February 19 2015 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Makala haya yanalenga kuangalia upande wa pili wa sarafu ambao mwandishi Alex Ngure hakuumulika katika makala yake. Mitazamo na ufafanuzi wa dhana  ‘riwaya’ (Taifa Leo, Februari 16, 2015) labda kwa sababu ya ukosefu wa nafasi. Nitaangazia chanzo cha mtafaruku wenyewe kwa kutumia Nadharia ya Tanzu (Genre Theory) kwa mujibu wa Fowler Alaistair katika kazi yake ya Kinds of Literature (1982).

MSUKUMO wa kuandika makala haya unatokana na makala ya Mwalimu Alex Ngure  -  ‘Mitazamo na ufafanuzi wa dhana  ‘riwaya’ (Taifa Leo, Februari 16, 2015). Mwandishi alijaribu kuangazia mtafaruku ulio(kuwe)po baina ya wataalamu katika kutoa fasiri ya ‘riwaya’. Makala yangu yanalenga kuangalia upande wa pili wa sarafu ambao mwandishi hakuumulika kwa sababu ya labda ukosefu wa nafasi. Kwa usemi mwingine, ninalenga kuangazia chanzo cha mtafaruku wenyewe kwa kutumia Nadharia ya Tanzu (Genre Theory) kwa mujibu wa Fowler Alaistair katika kazi yake ya Kinds of Literature (1982). Nadharia ya Tanzu ni utaratibu wa kuainisha fasihi katika misingi ya aina mbalimbali kwa kuegemea miundo na maumbo. Umbo ni sifa za nje zinazoipa kazi ya fasihi sura za kutambilika. Sura hizi ni pamoja na  sura, matendo, maonyesho, vina, mizani n.k. Muundo nao ni jumla ya uhusiano unaokuwepo kati ya vijisehemu mbalimbali vinavyounda kitu kamili au kwa jumla.

Muundo wa tamthilia kwa mfano una maana ya matendo yake pamoja na maonyesho mbalimbali na jinsi visehemu vyote vinavyohusiana kuunda kazi nzima inayoitwa tamthilia. Nadhatia ya tanzu ina misingi yake katika Kipindi cha  Urasmi ambapo fasihi ya Ugiriki na Urumi ilifana. Katika Poetics kwa mfano, Aristotle  anaeleza maana na sifa za tamthilia ya kitanzia. Kwa hiyo, kazi hii ni kiwakilishi cha Nadharia ya Tanzu.  Sifa hizi zinafaa kuwaelekeza na kuwaonesha jinsi kazi za utanzu fulani zinavyopaswa kuwa; urefu, idadi ya matukio ambayo mtazamaji anaweza kuyakumbuka n.k. Kwa hiyo, nadharia ya tanzu katika kipindi cha urasmi ililenga kuwekea  tanzu mipaka. Aidha, tuna nadharia ya tanzu ya kisasa.

Mara nyingi, nadharia ya kipindi hiki ni ya kimaelezo tu. Inaeleza tanzu zilizopo, sifa zao – bila kuziwekea sheria zozote au mipaka yoyote. Inatambua kuwa tanzu za kifasihi zinazotambulika  zinaweza kuchanganywa na vilevile zinaweza kuzaa tanzu mpya (umahuluti wa tanzu). Kwa mfano, tamthilia inaweza kuwa mseto wa tanzia na  futuhi na tukawa na futuhi ya kitanzia – kwa mfano Mkaguzi Mkuu wa Serikali (Nikolai Gogol). Riwaya ya kibarua kwa mfano Barua Ndefu kama Hii (Mariama Ba) imeandikwa katika mtindo wa barua. Waandishi wengine wamechanganya nathari na ushairi – kwa mfano Maisha yangu na Baada ya Miaka Hamsini (S. Robert). Katika kipindi cha urasmi ambacho tumekigusia, jambo hili halingeweza kutokea kamwe kwa sababu kila utanzu ulifuata kanuni fulani. Hakuna mtunzi aliyethubutu  kuchanganya tanzu.

Badala ya kusisitiza upekee wa kila utanzu, nadharia ya  tanzu ya kisasa inaangalia sifa za jumla za kila utanzu, kunga zake na lengo lake kifasihi. Kwa mfano, iwapo ni riwaya, badala ya kusisitiza upekee wa riwaya, itaelezea sifa zake za kimsingi (k.m inatumia usimulizi wa kubuni kimfululizo) na vilevile lengo lake la kijumla – kutoa picha halisi ya maisha katika jamii – hasa riwaya za kiuhalisia. Hata hivyo, nadharia ya tanzu haijasaidia sana katika sana katika kutoa uainishaji thabiti wa tanzi zilizopo. Imeshindwa. Je, ni vipi utambuzi wa aina mbalimbali za tanzu unavyosaidia katika kufasiri tungo za kifasihi? Fowler anasema, thamani kuu ya nadharia ya tanzu haitokani na suala la uainishaji; inatuwezesha tu kueleza jinsi tunavyoweza kuweka kazi fulani katika  tanzu mahususi ili tuweze kuifasiri na kuishughulikia. Kwa hiyo, uainishaji unapaswa kuwa  hatua ya kwanza katika uhakiki. Kwa mfano, Kwaheri Iselamagazi (B. Mapalala) ni riwaya. Ni riwaya ya aina gani? Ni ya kihistoria. Je, riwaya ya kihistoria ina sifa gani? Tukikwisha kujubu maswali haya tunaanza kuihakiki kwa kubainisha ni kwa kiwango gani inatimiza sifa za riwaya za kihistoria.

 Uhakiki wa kiutanzu

 Kuzitalii kazi za fasihi, kuziweka katika makundi ya tanzu na kutathmini ni zipi zinakiuka kanuni za tanzu husika, kwa kiasi gani na kwa sababu gani ni uhakiki wa kiutanzu. Kwa mfano, tunapouangalia utanzu wa riwaya, tunaweza kurejelea kazi ya Edward Morgan Forster, Aspects of The Novel ambapo ameeleza baadhi ya sifa za kimsingi za utanzu wa riwaya. Kwa mfano Forster anasema kwamba riwaya inapaswa kuwa na maneno 120,000 au takriban kurasa 403.  Forster ni Mwingereza kwa hiyo mifano au vigezo anavyotoa ni vya riwaya na kiulaya au Kiuingereza. Riwaya nyingi za Kiafrika hazina urefu huu. Kwa nini? Kwa sababu, kwanza, riwaya za Kiafrika inafanana sana na ngano za fasihi simulizi ambazo si ndefu. Pili utamaduni wa kusoma na kuandika haujakita sana Afrika – na hivyo basi hakujawa na mazoea ya kuandika kazi ndefu. Uhakiki wa kiutanzu unamwezesha mhakiki kutambua mchango wa kila kazi husika katika utanzu husika. Hii ina maana kwamba, kinadharia, kila kazi mpya inayotungwa huchangia utanzu husika kwa njia moja au nyingine. Mchango huu unaweza kuwa katika upande wa fani au maudhui.

Uhakiki wa kiutanzu humwezesha mhakiki kupambanua kazi bora au duni kwa kurejelea kanuni kuu za utanzu unaohusika. Kwa mfano, drama ya kitanzia na sifa zake zinaweza kutumika kutathminia kazi za aina hiyo – na kazi hizo zinapopungukiwa na vigezo vya drama ya kitanzia, inaweza kudaiwa kuwa ni duni. Hata hivyo, tatizo mojawapo linalojitokeza katika uhakiki wa kiutanzu ni kuzuka kwa fasihi mpya inayozua tatizo la istilahi na lugha ya kuielezea. Kazi mpya hutatiza kwa muda katika kutafuta istilahi za kuielezea kitaalamu – hasa inapokuwa imekiuka aina za fasihi zilizopo. Kwa mfano, bado wahakiki wanatatizika katika kuhakiki kazi mbili za Euphrase Kezilahabi – Nagona na Mzingile. Kwa nini? Kwa sababu hazina fani ya riwaya, hazina upana wa masimulizi wala ukuzaji wa wahusika – licha kwamba zina uzito kimaudhui. Je, kazi hizi ni riwaya? Je, ni hadithi fupi? Kwa hiyo, kazi hizi mbili bado zinawakanganya watu wengi kwa sababu ya tofauti yao na utanzu wa riwaya kwa jinsi inavyozoeleka.

Vilevile, Kezilahabi na wanamapinduzi wengine walipotunga mashairi yasiyofuata vina na mizani, ushairi huo huru uliwatatiza wahakiki hasa kuhusiana na jina lake. Je, ni macue? Mashairi ya mtiririko? Masivina? Au ni mashairi huru? Tanzu pia hukua na hatimaye kuchakaa au ‘kufa’ hasa pale ambapo mazingira yanayolea utanzu husika yanapotoweka. Katika fasihi ya Kiswahili, utanzu wa utendi/ tenzi unaweza kudaiwa kwamba ‘umekufa’. Hatuoni watu wengi wakitunga tenzi siku hizi. Hata hivyo, tunachoshuhudia ni usimilishwaji wa baadhi ya hizi tenzi na baadhi ya watunzi kuzisimulia tendi zilezile katika maumbo au tanzu nyingine. Kwa mfano novela ya Bitugi Matundura, Mkasa wa Shujaa Liyongo imesimilisha Utenzi wa Liyongo (Mohamed Kijumwa). Tamthilia ya Kifo  Kisimani ya Kithaka wa Mberia imetokana na utenzi huo – huku riwaya ya Siri Sirini 1,2 & 3 ya Rocha Chimerah imetumia kiunzi cha tenzi za Fumo Liyongo na Mwanakupona.

Msingi huu kuhusu  nadharia ya tanzu na uhakiki wa kiutanzu unatupatia mwanga wa kuweza kuona kitaalamu ni kwa nini wataalamu aliowataja Mwalimu Ngure kwenye makala yake wana mitazamo mbalimbali kuhusu dhana ya ‘riwaya’. Inategemea mkabala na vigezo anavyochukua mtaalamu katika  kufikia kauli zake. Mtaalamu akiegemea vigezo vya Forster kwa mfano katika kuainisha riwaya ya za Shaaban Robert – kuna uwezekano wa kuhitimisha kwamba  tungo kama vile  Kusadikika, Kufikirika  na Adili na Nduguze si riwaya.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

 

Share Bookmark Print

Rating