Kuua lugha asili ni sawa na kuteketeza maktaba

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, March 24  2016 at  14:07

Kwa Muhtasari

LUGHA na utamaduni ni mambo yanayokurubiana. Lugha ni kibebeo cha utamaduni mbali na kuwa chombo kinachosheheni fikra, imani na matamanio ya watu.

 

Lugha na utamaduni ni mambo yanayokurubiana. Lugha ni kibebeo cha utamaduni mbali na kuwa chombo kinachosheheni fikra, imani na matamanio ya watu.


Kwa sababu hiyo, juhudi za kimakusudi zinapaswa kufanywa kuihifadhi kwa kuhimiza matumizi ya lugha hizo.

Ingawa kumekuwapo na malalamishi kwamba uhuru wa vyombo vya habari miaka ya tisini – ambao ulichangia mlipuko wa vituo vya Redio za FM vinavyotangaza kwa lugha za kiasili 'umechochea ukabila’, sikosei kudai kwamba kuna manufaa tumbi nzima ya hali hii.


Lugha zetu asili zimepata fursa ya kuhuishwa. Hata hivyo, licha ya lugha asili kupata nafasi ya kutumiwa katika vyombo vya habari, bado kuna baadhi yazo ambazo zinakabiliwa na hatari ya kuangamia na kutoweka ulimwenguni.


Je, chanzo cha 'vifo’ vya lugha ni kipi? Tatizo kuhusu tishio la kufa kwa lugha limekwisha kutambuliwa ulimwenguni kote. Takriban nusu ya ndimi au lugha 6,000 (asilimia 50) zinazokisiwa kuzungumzwa ulimwenguni huenda zikatoweka.

Wataalamu wa masuala ya 'vifo’ vya lugha wamedai kwamba lugha hizo zinazungumzwa na watu wazima ambao hawafundishi kizazi chipukizi lugha hizo.


Isitoshe, asilimia arobaini (40) zaidi ya lugha hizo huenda zikatoweka kwa sababu idadi ya watoto wanaojifunza lugha hizo inapungua kila uchao. Hii ina maana kwamba asilimia 90 ya lugha zinazozungumzwa duniani kwa sasa huenda zikatoweka au zikaangamia katika karne ijayo.


Nchini Kenya, ambapo tuna zaidi ya lugha 45 – sawa na mataifa mengine duniani, hatujasazwa na tatizo hili la kufa kwa lugha za kiasili.

Kwa muda mrefu, Kenya imekuwa ikitumia Kiingereza kuwa lugha rasmi na Kiswahili kuwa lugha ya taifa hadi mwaka 2010 ambapo Katiba ilikikweza hadhi Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kwanza sambamba na Kiingereza.

Tishio la 'kufa'
Baadhi ya lugha zinazokabiliwa na tishio la 'kufa’ nchini Kenya ni pamoja na El-Molo au Ndorobo, Fura au Dehes, Seng’wer, Yaaku, Waata au Boni, Terik, Burji, Dahalo au Bong’omeek, Suba na Sagall.

Lugha ya Olusuba (Suba) kwa mfano inafifia kwa sababu ya kukandamizwa kiisimu na Dholuo. Utangamano na mitagusano kati ya Waluo na Abasuba imesababisha Dholuo 'kumeza’ Kisuba.


Hali ya vifo vya lugha nchini Kenya imechangiwa zaidi na ukosefu wa juhudi za kimakusudi katika kuzitafitia lugha za kiasili, na kuziandikia vitabu.

Hatua za dharura zisipochukuliwa, wazungumzaji wachache wanaozifahamu lugha hizo huenda wakafariki bila maarifa yao kuhifadhiwa kwa njia ya maandishi au njia nyingine murua.


Waandishi na wasomi wakiwemo Ngugi wa Thiong’o, Grace Ogot, Okoth Okombo, Kennedy Momanyi Bosire na Gladys Kwamboka Machogu walikwisha kufanya juhudi za kuziandikia lugha za asili za makabila yao – ingawa juhudi zao hazijafanikiwa sana.

Bw Kennedy Momanyi Bosire na Bi Gladys Kwamboka kwa mfano wamekwisha kuandika na kuchapisha kamusi ya Ekegusii (Endabaro Endasaba Y’Ekegusii). Profesa Ngugi wa Thiong’o na marehemu Grace Ogot wamekwishatoa mchango wao kwa kuandika kazi za fasihi kwa lugha za Kikikuyu na Dholuo mtawalia.

Neema ya Redio
Nilivyotaja mwanzoni mwa makala haya, mlipuko wa vituo vya Redio za FM ulioshuhudiwa nchini Kenya mapema miaka ya 2000 unapaswa kuchukuliwa kuwa neema badala ya balaa. Juhudi za watu binafsi katika kuzitetea lugha asili hazipaswi kupingwa bali kuungwa mkono.


Halikadhalika, Kenya inahitaji kuimarisha sera yake ya lugha ili kukabiliana na wimbi lenye dhoruba kazi la 'vifo’ vya lugha.

Kuna hasara gani lugha 'inapokufa’? Lugha ifapo, huwa ni kana kwamba maktaba nzima ya jamii imeteketezwa. Kuna maarifa yanayofumbatwa na lugha zetu za asili- ambayo hayawezi kamwe kuelezwa kwa lugha nyingine yoyote ile.


Sura ya Pili, Kifungu cha 7, Ibara (3) ya Katiba ya Kenya inasema: Serikali (a) Itakuza na kulinda lugha tofauti za wananchi wa Kenya; na (b) Italinda na itastawisha matumizi ya lugha za kiasili, Lugha Ishara ya Kenya, Breli na njia nyingine za mawasiliano na teknolojia zinazoweza kufikiwa na watu wenye ulemavu.

Tamko hili linapaswa kuwa kichocheo cha kuzithamini lugha zote asili nchini Kenya.