Ipo haja ya dharura ya kukisanifisha upya Kiswahili

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, March 10  2016 at  15:43

Kwa Muhtasari

Mtaalamu Abdalla Khalid katika The Liberation of Swahili from European Appropriation anahisi kwamba uteuzi wa Kiunguja ulikuwa ni njama ya chini kwa chini iliyoendelezwa na Wazungu ili kuendeleza utumwa.

 

KABLA ya mataifa ya Afrika ya Mashariki kujipatia uhuru, palizuka haja ya kusanifishwa kwa Kiswahili mnamo 1930.

Usanifishaji kimsingi ni utaratibu wa kuondoa tofauti zote zisababishwazo na wingi wa lahaja, maeneo, matabaka kwenye maandishi au othografia, msamiati, matamshi na sarufi.

Mtaalamu Ireri Mbaabu anasema kwamba usanifishaji wa Othografia unanuiwa kupata mtindo mmoja wa kuendeleza kila neno katika lugha kulingana na matamshi.

Wataalamu wa Kiswahili wameanza kutilia shaka kuwapo kwa Kiswahili sanifu. Je, nchini Kenya watu huzungumza Kiswahili au 'Viswahili?’.

Mtaalamu Dkt Ayub Mukhwana wa Chuo Kikuu cha Nairobi aliwahi kuuliza miaka ya 1990; Kiswahili sanifu, Je kipo? Swali la Dkt Mukhwana labda lilichochewa na mabadiliko mengi kwenye nyanja na taaluma mbalimbali yanayojiri katika jamii ya sasa ambayo Kiswahili hakina budi kuyakidhi. Ni kwa nini Kiswahili kilisanifishwa?

Kwanza, kulikuwapo na lahaja nyingi za Kiswahili – na hali hii ilitatiza mawasiliano katika nyanja za dini, elimu na shughuli za utawala.

Kwa hivyo, ili kufanikisha mawasiliano katika nyanja hizo, nchi za Afrika ya Mashariki zilianzisha Kamati ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki mnamo 1930. Kamati hii ilitwikwa jukumu la kukisanifisha Kiswahili.

Kamati hii iliteua lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa kusanifisha Kiswahili kwa sababu mbalimbali.

Kwanza, lahaja hii ilikuwa imesambaa mno kuliko Kimvita ambacho kilikuwa pia kinawania nafasi hiyo.

Pili, asemavyo Ireri Mbaabu katika Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili ni kwamba, Kiunguja kilikuwa rahisi kufahamika kuliko Kimvita kwa kuwa matamshi yake hayakuwatatanisha wasemaji wengi.

Tatu, Kiunguja kilikuwa kimekwisha kufanyiwa utafiti mwingi na wataalamu kama vile kina Askofu Edward Steere, mbali na kutumiwa kwa marefu na mapana katika mahubiri na uandishi wa vitabu.

Mwisho, Kiunguja kilikuwa lugha ya biashara na vilevile lugha ya kisiwa cha Zanzibar – ambacho wakati huo kilikuwa kitovu cha Biashara Afrika ya Mashariki.

Mtaalamu Abdalla Khalid katika The Liberation of Swahili from European Appropriation anahisi kwamba uteuzi wa Kiunguja ulikuwa ni njama ya chini kwa chini iliyoendelezwa na Wazungu ili kuendeleza utumwa.

Kimvita kilistahili

Anadai kwamba Kimvita ndicho kilichostahili kuteuliwa kwa kuwa lahaja hiyo ni rahisi kueleweka kuliko lahaja nyingine na vilevile kuwa ni lahaja yenye historia ndefu ya maandishi ya fasihi inapolinganishwa na lahaja nyingine.

Khalid anadai kuwa Kiunguja ni lahaja ya 'kijingajinga’ iliyochafuliwa na Kiarabu. Kwa sababu hiyo, Khalid anapendekeza Kiswahili kisanifishwe upya kwa kutumia Kimvita kama lahaja ya Kimsingi.

Hisia za kupinga Kiswahili sanifu zimewahi kuibuka hata miaka ya hivi karibuni. Katika kongamano la wadau wa elimu jijini Mombasa miaka michache iliyopita, Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa alipendekeza kwamba kila mojawapo wa lahaja zaidi ya 16 za Kiswahili itahiniwe kivyake katika mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE).

Hata hivyo, mbali na kwamba mwengo wa usanifishaji upya wa Kiswahili unazibiwa masikio, ukweli uliopo ni kwamba kuna 'Viswahili’ vingi vinavyotofautiana katika matamshi, maendelezo sarufi na hata msamiati.

Mkabala huu unapaswa kuwaziwa upya na wataalamu wa Kiswahili nchini Kenya – hasa ikifahamika kwamba Kenya hadi leo haina chombo cha kiserikali kinachoweza kutwikwa shughuli za uratibu wa maendeleo ya Kiswahili.

Shughuli hii imeparaganywa na watu binafsi – wengine wanaojitafutia makuu. Hata hivyo, juhudi hizo haziwezi kupingwa bali kuungwa mkono.

Mchakato wa usanifishaji wa lugha hauwezi kufanywa mara moja na kukamilika – bali unapaswa kuendelezwa kadri Kiswahili kinavyoendelea kukua na kupanuka kila uchao.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka na mtunzi wa kazi nyingi za kifasihi.

mwagechure@gmail.com