Kuna haja ya kufufua leksikoni ambayo ilikufa?

Imepakiwa Thursday April 7 2016 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Jukumu kubwa la vyombo vilivyotwikwa mamlaka ya kustawisha lugha katika mataifa mbalimbali limekuwa ni kubuni istilahi kukidhi mahitaji ya elimu na mawasiliano.

JUKUMU kubwa la vyombo vilivyotwikwa mamlaka ya kustawisha lugha katika mataifa mbalimbali limekuwa ni kubuni istilahi kukidhi mahitaji ya elimu na mawasiliano.

Baadhi ya asasi zinazotekeleza jukumu hili ni Kituo cha Istilahi za Ufundi cha Uswidi, Baraza la Lugha ya Taifa [Dewan Bahasa dan Pustaka] nchini Malaysia, Akademia ya Kihibrania ya Uyahudi na Baraza la Lugha la Taifa la Tanzania (BAKITA).

Asasi nyingine zinazochangia katika maendeleo ya istilahi au msamiati ni vyombo visivyo vya serikali ambavyo huunda istilahi zinazohusiana na shughuli zavyo.

Katika kundi hili tuna vyombo vya habari kwa mfano Taifa Leo.

Mtaalamu Hermans Mwansoko anasema pia kwamba huko Malaysia, Kampuni ya Shell imejishughulisha sana katika uundaji wa istilahi zinazohusu uchimbaji na usafishaji wa mafuta katika lugha ya Kimalaysia.

Vyombo vingine vya kimataifa vinavyojishughulisha na uundaji wa istilahi ni Shirika la Uchumi la Ulaya, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Ubora wa Viwango.

Mwansoko anasisitiza kwamba mchango wa vyombo hivi mara nyingi hujikita katika istilahi zinazohusu shughuli zao katika lugha kuu za ulimwengu au lugha za wanachama wao.

Kwa bahati mbaya, Kenya haina chombo cha kiserikali kinachoshughulikia mchakato wa uundaji, usanifishaji na usambazaji wa istilahi.

Kutokana na pengo hili, watu binafsi wamejitokeza kufidia hali hii. Baadhi ya wataalamu wanaotumia raslimali zao kuchangia katika maendeleo ya leksikoni nchini Kenya ni pamoja na Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa, Profesa Rocha Chimerah (Chuo Kikuu cha Pwani) na Profesa Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mkabala

Katika makala haya, ninaangazia mkabala wa Mzee Sheikh Nabhany wa 'ufufuaji wa msamiati chakavu’ na kuurejesha tena katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Makala pia yatautathmini mkabala huu na kutoa maoni iwapo unafaa au haufai.

Tasnifu ya Mzee Sheikh Nabhany inauma kuwili.

Kwanza, anahisi kwamba Kiswahili kinakopa sana msamiati kutoka lugha nyingine (hasa za kigeni) – hata pale ambapo maneno hayo ama tayari yapo katika Kiswahili au lugha za Kibantu zinazokurubiana na Kiswahili.

Pili, mtaalamu huyu anahisi kwamba mkondo wa ukopaji kiholela unafanya Kiswahili kipoteze upekee wake.

Kwa hivyo, anapendekeza kwamba upanuzi wa leksikoni ukuzwe 'mumo kwa mumo’ katika kuegemea kanzi lugha za kiasili kabla ya kukimbilia ukopaji kutoka kwa lugha za kigeni.

Wataalamu wanakisia kwamba asilimia 60 ya msamiati wa Kiswahili ni maneno ya Kibantu; Kiarabu (asilimia 30) na asilimia 10 (msamiati kutoka kwa lugha nyingine).

Katika Kandi ya Kiswahili (2012) Mzee Sheikh Nabhany ameorodhesha takriban maneno 60 ya Kiswahili cha kale na visawe vyake vya Kiarabu na lugha nyingine ambayo yanatumiwa katika Kiswahili sanifu.

Baadhi ya mameno hayo ni: Alfajiri (Kiarabu), Mshekuu (Kiswahili cha kale); Ami (Kiarabu); Bakulu (Kiswahili cha kale), Damu (ngeu), hofu (kicho); jahazi (sambo); kiburu (ndeo), bara (tinene), asali (uki), picha (uyoo); jabali (mwamba); mfalme (makame) n.k. Maneno kwenye mabano ni ya Kiswahili cha kale.

Anachopendekeza Mzee Sheikh Nabhany ni kwamba Kiswahili kisikubali ukopaji wa maneno ambayo tayari yamo katika utamaduni wa Waswahili au lugha nyingine za Kibantu ambazo zinakurubiana mno na Kiswahili.

Ukopaji

Swali tunalofaa kujiuliza ni hili; Je, ukopaji wa aina hii ni wa pekee katika Kiswahili?

Tathmini inaonesha kwamba Kiingereza – ambayo ni mojawapo ya Lingua Franca maarufu ulimwenguni ina visawe vingi vya maneno yaliyokopwa kutoka kwa lugha nyingine ulimwenguni.

Kiingereza kwa hakika ndiyo lugha yenye idadi kubwa ya visawe kuliko lugha nyingine yoyoye ile ulimwenguni.

Kwa hivyo, mbali na kwamba mkabala wa Mzee Sheikh Nabhany kuhusu uendelezaji wa leksikoni ya Kiswahili unakubalika kinadharia, hauna mashiko kiutekelezaji.

Kwa nini? Kwa sababu lugha daima zinabadilika kila uchao kutokana na mitagusano ya tamaduni.

Hali kadhalika, dhana ya 'visawe’ katika lugha mara nyingi haipo kwa sababu msamiati fulani hufumbata dhana fulani vizuri zaidi kuliko nyingine.

Hata hivyo, michango na maoni ya watu binafsi na vyombo vya habari kuhusu kuendeleza leksikoni ya Kiswahili haipaswi kupingwa bali kuungwa mkono pale inapochangia kukiendeleza Kiswahili.

Share Bookmark Print

Rating