Matoleo mengi ya kamusi ni ithibati lugha inakua

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Tuesday, June 28  2016 at  10:20

Kwa Muhtasari

Ukweli ni kwamba, katika taaluma ya elimu, mikabala ya kutaja jambo lile lile ni mingi jinsi ilivyo idadi ya watu ulimwenguni.

 

UKWELI ni kwamba, katika taaluma ya elimu, mikabala ya kutaja jambo lile lile ni mingi jinsi ilivyo idadi ya watu ulimwenguni.

Kauli hii inanipa idhini ya kutoa mtazamo wangu kuhusu makala ya mwandishi Enock Nyariki, 'Hakuna kamusi faafu ya Kiingereza – Kiswahili’ (Taifa Leo, Juni 23, 2016).

Kwenye makala hayo, Bw Nyariki anahisi kwamba idadi ya kamusi za Kiswahili ambazo zimekwisha kuchapishwa katika karne ya 21 ni ishara ya maendeleo ya Kiswahili.

Mwandishi huyu hata hivyo alitahadharisha wachapishaji wa kamusi hizo dhidi ya kuingiza 'msamiati uchwara (?)’ kwenye kamusi mpya kwa kisingizio kwamba msamiati wenyewe umekolea katika matumizi ya kila siku.

Onyo

Alionya pia kwamba kutofanya hivyo kutazua hali ambapo mashirika ya uchapishaji yataishia kuchapisha 'kamusi za Sheng’ yakidhani kwamba ni kamusi sanifu za Kiswahili.

Mwandishi alisema kwamba baadhi ya maneno ya Sheng yaliyoingizwa kwenye baadhi ya kamusi ni msamiati 'poa’.

Kadhalika, Bw Nyariki anaonekana kukerwa na hali ambayo msamiati unahusu watu au makabila ambayo hayahusiani kwa damu wala usaha na historia ya Kiswahili umeingizwa kwenye baadhi ya kamusi.

Kufikia hapa, mwandishi Nyariki anaonekana kutamatisha awamu ya kwanza ya Makala yake na kuingia katika awamu ya pili ambapo anasema lengo la Makala yake – kuangazia umuhimu wa kuwepo kwa kamusi mwafaka ya Kiingereza – Kiswahili.

Mwandishi Nyariki anashangaa kwamba Mmishenari, Fredrick Johnson aliwapiku wazawa wa lugha ya Kiswahili kwa kuandika A Standard English- Swahili Dictionary (Oxford, 1939).

Matini

Nimenukuu kwa marefu matini ya Bw Nyariki kwa lengo la kuyachokonoa na kutoa mtazamo kuhusu suala hili zima.

Kwanza, kulihitajika muumano kati ya sehemu mbili za makala yake.

Pili, nahisi kwamba kauli ambazo nimezitilia alama (?) si za kweli.

Hakuna msamiati 'uchwara’ katika lugha yoyote iwayo. Haiyumkiniki kamusi yoyote iwayo kuweza kusheheni kila neno, istilahi au msamiati katika lugha.

Badilika

Hii inatokana na sababu ya kimsingi kwamba lugha inabadilika kila uchao na kuna dhana ngeni zinazozuka. Ndiposa wanaleksikografia wanajitahidi kuboresha kamusi na kutoa matoleo mbalimbali.

Ukweli ni kwamba, mchakato wa uandishi wa kamusi daima huwa ni kama mzunguko wa dunia na hakuna siku utawahi kukoma. Mwandishi alitaja kuwepo kwa matoleo ya kwanza na pili ya English-Swahili Dictionary (TUKI).

Kauli hiyo ni ithibati tosha ya kuonesha kwamba lugha zinakua kwa kasi mno na ni shughuli ghali mno kuandaa kamusi.

Utunzi wa kamusi si jambo rahisi watu wengi wanavyofikiria.

Tatu, neno 'poa’ ni la Kiswahili sanifu na hulka ya Sheng ni kwamba, ina maneno ya Kiswahili sanifu na maneno ya lugha nyingine kutoka lugha nyingine.

Nne hakuna hatia ya mashirika ya uchapishaji kuchapisha Kamusi za Sheng. Kwa hakika, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ambayo sasa inaitwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili imechapisha Sheng-English Dictionary : Deciphering Africa’s Underworld Language iliyotungwa na msomi wa Kiswahili Ireri Mbaabu na Nzuga Kibande.

Mapengo

Kwamba Kamusi ya Johnson ina mapengo mengi ni kauli ya kawaida kwa sababu Fredrick Johnson hakuwa mwanaleksikografia na hivyo basi si ajabu kwamba kamusi yake ina matatizo.

Isitoshe, lengo lake la kutunga kamusi lilikuwa ni kumwezesha kufanikisha shughuli zake za kueneza injili wala haikuwa shughuli ya kiakademia.

Nilikuwa mmoja wa wahariri wa Kamusi ya Karne ya 21 (Longhon, 2011) na ninafahamu fika changamoto zinazoikumba taaluma ya leksikografia ya Kiswahili.

Vilevile, maneno katika kamusi za Kiswahili si lazima yawe ya makabila yanayohusiana na Waswahili tu.

Kiswahili kimepasua kingo zake na kuwa lugha ya dunia.

'Vuvuzela’

'Vuvuzela’ kwa mfano si msamiati wa kabila linalohusiana na Waswahili.

Kwamba Kiswahili kinatohoa sana, utohozi ni jambo la kawaida kwa lugha ambayo haina dhana zile katika utamaduni wake; kuwepo kwa vivuli vya maneno (hakuna usawe katika lugha yoyote iwayo na vivuli vya maneno ni jambo la kawaida) na kadhalika.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka na alikuwa mhariri msaidizi wa Kamusi ya Karne ya 21 (Longhorn, 2011)