Uandishi wa kazi za kibunifu hauhitaji nguvu za uchawi

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, June 23  2016 at  14:47

Kwa Muhtasari

Kwa takriban kipindi cha miaka mitano ambacho nimefundisha nimekuwa nikishuhudia 'utasa’ wa waandishi chipukizi waliopitia katika mikono yangu – kwa misingi kwamba, hapajakuwapo hata mwanafunzi wangu mmoja ambaye amechapisha kazi ya kubuni.

 

MOJAWAPO ya kozi ambazo ninafundisha katika chuo kikuu ni 'uandishi wa kubuni katika Kiswahili’.

Kwa takriban kipindi cha miaka mitano ambacho nimefundisha nimekuwa nikishuhudia 'utasa’ wa waandishi chipukizi waliopitia katika mikono yangu – kwa misingi kwamba, hapajakuwapo hata mwanafunzi wangu mmoja ambaye amechapisha kazi ya kubuni.

Nilipokuwa nikiajabia hali hii na kuelekea kukata tamaa; kwamba 'huwezi kumfunza mtu kuwa mwandishi wa kubuni’ (kwa kuwa waandishi huzaliwa wala hawaandaliwi), mmoja wa wanafunzi wangu wa zamani, Bw Samuel Mwenda alinipigia simu akiniambia kwamba amekwisha kuchapisha riwaya inayoitwa Mvuvi na kampuni ya Nsemia Inc., Toronto, Canada.

Iwapo mwandishi wa kubuni huzaliwa akiwa na uwezo wa kuandika au anaweza kufundishwa kuandika – hilo ni suala la mjadala.

Hata hivyo, katika makala ya leo ninaangazia jinsi ambavyo mwandishi wa kubuni anavyoweza kupata au kuzua visa vya kutungia.

Ninapotanguliza somo hili katika vipindi vyangu chuoni, huwafahamisha wanafunzi kwamba 'uandishi wa kubuni si uchawi’.

Je, waandishi wa kubuni hutoa wapi visa wanavyovitungia? Swali hili ni muhimu kwa sababu haiwezekani mtunzi yeyote awaye kutunga kwenye ombwe.

Sharti pawe na chemchemi ambayo kutoka kwayo, waandishi wa tungo za kibunifu huteka visa vya kutungia. Kazi yoyote inayozingatia uyakinifu wa kijamii ina kiwango fulani cha ubunifu na kiwango cha uhalisia wa maisha.

Yaani, tungo zote za kibunifu zina ukweli fulani unaoakisi hali halisi anamokulia mwandishi.

Kwa mfano, ili tumwelewe Ebrahim Hussein (yaani maana ya kifasihi katika tungo zake), tunaweza kujikita kwenye matini ya kazi zake pekee, tunaweza kurejelea mazingira na tajriba zake maishani, muktadha, au msomaji akatumia tajriba zake binafsi kusimbua msimbo katika kazi za Hussein au tukaangalia mwingiliano-matini.

Mwandishi yeyote yule wa tungo za kubuni hutegemea hisi, moyo na mikono yake katika kutekeleza jukumu la uandishi.

Kwa hivyo, mwandishi wa kubuni huweza kuona, kusikia, kuonja, kuhisi na kunusa mambo mbalimbali ambayo hatimaye anayaandikia.

Mbinu

Kimsingi, kuna njia nyingi ambazo mwandishi anaweza kufuata ili kuzalisha matini za kiubunifu.

Njia hizi ni pamoja na fikra, matembezi, mazungumzo na watu wengine au wataalamu, vyombo vya habari (magazeti, redio, runinga, mtandao wa intaneti au wavuti, fasihi nyinginezo au hata ndoto.

Tukio la hivi majuzi la kuuawa kwa mfanyabiashara Jacob Juma kwa njia isiyoeleweka ni msingi mzuri sana kwa mwandishi anayetaka kuandika riwaya ya kiupelelezi.

Ingawa nimekwisha kutaja kwamba uandishi wa kubuni si uchawi, mtu yeyote anayepania kuwa mwandishi atakayeacha taathira katika jamii sharti awe tayari kusoma kwa marefu na mapana fasihi za watu wengine pamoja na kazi nyingine katika taaluma mbalimbali kama vile falsafa, elimu, fizikia, kemia, biolojia na kadhalika.

Kwa kuwa malighafi ya mwandishi na nyenzo anayotumia kuwasilisha mawazo yake ni lugha, mtu yeyote anayetaka kuwa mwandishi ni sharti awe mjuzi na mweledi wa lugha.

Watunzi wazuri wa kazi za kifasihi wana uwezo wa kuifanya lugha iwatumikie jinsi wapendavyo.

Baada ya kupata kisa cha kutungia na kuimudu lugha ya kusimulia kisa chenyewe, mwandishi sharti aketi chini na kutunga.

Siri ya kufanikiwa katika uandishi ni kuandika – wala hakuna njia nyingine ya kufanikiwa katika fani hii. Labda kabla ya kujitosa katika bahari ya uandishi, ni muhimu kwanza mtu ajifunze kuogelea katika bahari hiyo kwa sababu ni shughuli inayowahitaji watu wenye mioyo ya chuma – wasiokata tamaa na wala wasioandika kwa malengo ya kujipatia hela.

Ni vigumu sana kupata shilingi hata moja kutokana na uandishi wa kazi za kubuni.

Ikiwa unataka kupata hela kutokana na uandishi, basi ningependekeza kwamba uandike vitabu vya kiada. Huko ndiko kuna hela.

Aidha, isichukuliwe kwamba kila kazi inayochapishwa ni bora.

Katika taaluma ya uandishi wa kubuni hasa katika Kiswahili, kuna watu wanaong’ang’ania kutunga hata pale ambapo hakuna kipawa.

Mimi huwaita waandishi wa aina hii 'waandishi wa masafa mafupi’. Wala idadi ya vitabu anavyotunga mtu haimaanishi kwamba inamfanya kuwa mwandishi bora.

Kuna watunzi kama Mohamed Suleiman Mohamed waliotunga kazi tatu tu – yaani riwaya za Nyota ya Rehema, Kiu na mkusanyo wa hadithi fupi wa Kicheko cha Ushindi, basi.

Lakini huwezi kuizungumzia fasihi ya Kiswahili bila angalau kumtaja mwandishi huyu.