Udhanaishi katika riwaya na tungo za Kezilahabi

Imepakiwa Thursday February 4 2016 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Udhanaishi ni falsafa ambayo inamulika kwa kina masuala ya maudhui ya kifo, uhuru wa mtu binafsi, wajibu wa binadamu duniani, ubinafsi, kukata tamaa, udhaifu wa binadamu, furaha, ukengeushi na kuwepo au kutokuwepo kwa Mungu.

WAHAKIKI wa fasihi ya Kiswahili wamekwisha kukubaliana kwamba mwandishi Euphrase Kezilahabi ni mtunzi anayeegemeza tungo zake katika nadharia ya udhanaishi (existentialism).

Tatizo la maisha ya mwanadamu (existence) linaonekana kumshughulisha Kezilahabi katika takriban tungo zake zote – mathalan Kichomi na Dhifa (ushairi), Rosa Mistika, Kichwamaji, Dunia Uwanja wa Fujo, Nagona na Mzingile (riwaya).

Euphrase Kezilahabi labda ndiye mtunzi wa kazi za kubuni kwa Kiswahili ambaye amezungumzwa sana na wahakiki wa fani hizi katika karne hii.

Mwandishi huyu alizaliwa katika kijiji cha Ukerewe – Tanzania mwaka 1943.
Alielimishwa katika seminari ya kikatoliki ya Nyegezi, ambako alijifunza falsafa za kidhanifu za dini, lugha ya Kilatini na masomo mengine ya Kawaida.

Mtaalamu Mugyabuso Mulinzi Mulokozi anadai kwamba, baada ya kidato cha sita, Kezilahabi ambaye sasa ni profesa wa fasihi ya Kiswahili alitimuliwa katika seminari kwa sababu walimu wake walifikiri hakuwa na ‘wito’ wa kutosha kwa kazi ya upadre. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisomea ualimu, lugha na fasihi.

Onesha

Tathmini ya jicho kali ya tungo za Euphrase Kezilahabi inaonesha kwamba kazi zake zinaweza kuwekwa katika awamu mbili pana. Awamu ya kwanza inajumuisha kazi alizozitunga miaka ya sabini – Rosa Mistika (1971), Kichwamaji (1974), Dunia Uwanja wa Fujo (1975) na Gamba la Nyoka (1979). Awamu ya pili inahusisha tungo zake za miaka ya tisini – Nagona (1990) na Mzingile (1991).

Katika tungo zake zote – hasa riwaya, Kezilahabi hulitazama suala la maisha katika viwango viwili. Kiwango cha kwanza ni cha mtu binafsi – ilihali cha pili ni kile cha mtu huyohuyo katika jamii pana. Mtunzi huyu chambilecho Mulokozi humchukua mtu binafsi katika hatua zote za maisha yake: uzazi na ujana, malezi, ndoa, uzee na hatimaye kifo.

Hadithi ya Kichwamaji inasimuliwa pakubwa na Deusdedit Kazimoto bin Mafuru ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Anatuhadithia kisa hiki anapokuwa likizo ya miezi mitatu nyumbani kwao Ukerewe.

Hadithi hii inahusu uhasama kati ya Kazimoto na Manase Kabenga.

Uhasama

Uhasama huo unasababishwa na hatua ya Manase kumpachika mimba Rukia, dada yake Manase. Licha ya uadui baina ya wahusika hao wawili, mambo yanageuka kuwa kinyume. Kazimoto hatimye anamuoa Sabina.

Manase na Kazimoto wanajipata katika njia panda kwa sababu ya kuambukizwa maradhi ya zinaa ambayo matokeo yake ni kuwa, watoto wanaozaliwa wana vichwa vikubwa – yaani vichwamaji. Mwishowe, Kazimoto anajiua na hatua hiyo inazua hisia mbalimbali katika jamii.

Mtazamo

Vyombo vya habari vinawasilisha tanzia hiyo katika maoni na mitazamo tofauti – Uonaji wa mambo kwa mtazamo wa Kimagharibi na ‘Naizi Kachoka na Maisha’.

Aidha, kuna gazeti moja lililomtazama Kazimoto kama kiwakilishi cha bara la Afrika na kuandika kichwa cha habari chenye anwani, ‘Kutokuwa kwa Afrika katika ujadiliano’.

Udhanaishi ni falsafa ambayo inamulika kwa kina masuala ya maudhui ya kifo, uhuru wa mtu binafsi, wajibu wa binadamu duniani, ubinafsi, kukata tamaa, udhaifu wa binadamu, furaha, ukengeushi na kuwepo au kutokuwepo kwa Mungu.

Kazimoto kwa mfano haamini kwamba Mungu yupo. Anazua mjadala huo kwenye kikao cha kunywa pombe alipomtembelea rafiki yake Kamata aliyekuwa katika kijiji cha Sakwa.

Mjadala huo unazua mihemko, hamaki na makasiriko na kutishia kuharibu kikao. Tahakiki ya jicho pevu ya kazi za mwandishi huyu inaonesha bayana jinsi alivyobwia na kuathiriwa na masomo yake ya seminari.

Motifu hiyo inajidhihirisha katika tungo zake zote – huku ikipea mno katika tungo zake za Nagona na Mzingile.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka
mwagechure@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating