Ukakamavu wa Julius Malema kuzamia lulu Kiswahili ni wa kuigwa

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  14:21

Kwa Muhtasari

Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Party nchini Afrika Kusini Julius Malema amependekeza Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano mapana barani Afrika.

 

KINA CHA FIKIRA

MBUNGE na kiongozi wa chama cha Economic Freedom Party nchini Afrika Kusini Julius Malema amewashangaza wengi kwa kukipendekeza Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano mapana barani Afrika.

Malema ni mwanasiasa ambaye ulimu wake unawaka moto kama tanuri anawapofokea mahasimu wake wa kisiasa. Yeye ni miongoni mwa raia wa Afrika Kusini weusi wanaodai mfumo wa kiuchumi uliopo unawakandamiza weusi kwa faida ya weupe.

Wazungu walio wachache kabisa wanamiliki asilimia 70 ya ardhi nchini Afrika Kusini. Kwa hiyo anapigania sera ya kuwapokonya Wazungu ardhi  bila fidia na kuwapa watu weusi.

Kwa mtu ambaye hali duni ya watu wake ni jambo linalomshughulisha kila uchao, ni ajabu kwamba anaweza hata kukumbuka kwamba kuna kitu kiitwacho Kiswahili hapa duniani.

Kiswahili si sehemu ya zile lugha kumi na moja rasmi nchini Afrika Kusini. Hii haimaanishi kwamba hakuna kabisa Kiswahili nchini humo. Nakumbuka mwalimu wangu wa usomaji habari za Kiswahili Anderson Kalu, kaka yake Daniel Lolani Kalu, alihamia Channel Afrika mapema miaka ya tisini kwenda kutangaza katika idhaa ya Kiswahili.

Anderson Kalu alikuwa miongoni mwa wasomaji habari mahiri sana wa habari nchini Kenya siku hizo, na kwamba Channel Afrika, kituo cha habari cha Afrika Kusini, kilimchukua akifanyie kazi ni ishara kwamba tangu hapo Kiswahili kilipewa umuhimu fulani nchini humo. Ila tusisahau kwamba idhaa za Kiswahili zimekuwapo katika mataifa ya Afrika nje ya Afrika Mashariki kama vile Misri, Ghana na Naijeria.

Turudi kwa Julius Malema. Inakuwaje kwa mtu ambaye uchumi wa watu wake ndio muhimu zaidi, na ambaye hakijui Kiswahili mbele wala nyuma, akitetei namna hii? Kitu kizuri ni kitu kizuri na ndivyo kilivyo Kiswahili. Ni kama walivyosema Wahenga, “Kibaya chajitembeza, kizuri kinajiuza.”

Kizuri

Kiswahili kimeendelea kujiuza chenyewe hata kwa wasiokuwa wazawa wa Afrika Mashariki kama vile Julius Malema.

Wengine waliovutika nacho bila kukijua au kukijua vizuri ni waandishi magwiji kama Wole Soyinka na Chinua Achebe, wote wa Naijeria. Malema angeweza kukipendekeza Kizulu chake, Soyinka Kiyoruba chake, na Achebe Kiigbo chake. Lakini walivutwa na raghba ya Kiswahili isiyozuilika.

Hutokea hata watu wa mabara mengine kama vile Ulaya, Esia na Marekani Kaskazini wakakorwa na uzuri wa Kiswahili wakizamia lulu na kukijua toka utandanoni hadi ukokoni.

Mifano ya watu kama hawa ni mingi wala nafasi ndogo ya safu hii haitoshi kuwaorodhesha wale ninaowafahamu sikwambii wengi wengine nisiowajua. Uelewa wao wa Kiswahili na kunga zake ni wa kupigiwa mfano.

Wasomi hawa wameondokea kuwa wabobevu wa taaluma za Kiswahili na watetezi wakubwa wa lugha na utamaduni wa Waswahili.

Ilmuradi Kiswahili kimepata watetezi na wakereketwa wengi wasiotarajiwa na ambao usuli wao ni nje ya kitovu cha lugha hii yenyewe. Wapo Malema wengi nje; je nani ndio Malema wa ndani ya Afrika Mashariki kwenyewe? Zindukani jamani!

Prof. Ken Walibora ni msomi wa fasihi, mwanahabari na mwandishi mtajika katika ulimwengu wa Kiswahili