Kiingereza ni tishio kwa lugha nyingine kote ulimwenguni?

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, October 31  2018 at  07:37

Kwa Muhtasari

  • Suala zima la ukoloni wa lugha ya Kiingereza limejadiliwa.

  • Si Kiswahili tu, hata Kijerumani, Kifaransa na Kireno, lugha zote hizi zinatishiwa na uwepo duniani kote kwa Kiingereza kinachosambaa kama ugonjwa wa ebola.

 

UKOLONI wa Kiingereza ni wazo la kutisha ingawa kwa wengine ni jambo lisilofikirika. Wanakienzi Kiingereza kana kwamba kwenda ahera au mbinguni kunategemea kukifahamu.

Hili suala limejadiliwa hivi karibuni katika kongomano la School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.

Kongomano liliandiliwa kumuenzi Prof Farouk Topan aliyestaafu zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Wamefanya vizuri sana kumuenzi Topan mwandishi na msomi aliyetopea na aliyefundisha kwingi, tokea kwao Zanzibar na London. Linalonishangaza ni vile wanavyokumbuka umuhimu wa kuwa na kongomano la kumuenzi miaka 15 baada ya yeye kustaafu. Ila hilo silo linalonichochea kuandika makala leo.

Aidha bora niseme sikualikwa kwenye kongomano hili la London. Wapo baadhi ya marafiki zangu walialikwa na kuwepo kwao kulitosha. Sina shaka walifanya kazi kubwa katika hafla hiyo ya ya kumuenzi Mzee Topan Farouk kwa mchango wake katika taaluma za Kiswahili. Isipokuwa niseme tu kwamba rafiki yangu mmoja walimwalika pasina kumpa ufadhili, imebidi marafiki kuchanga ili kumwezesha kufika London.

Muhimu hapa kufanyika mkutano Uingereza na suala zima la ukoloni wa lugha ya Kiingereza limejadiliwa. Yaani vidokezi nilivyopewa, maana sikuwapo, ni kwamba wanakongomano walijasiria kuongelea tishio la Kiingereza kwa maenezi ya lugha nyingine duniani.

Si Kiswahili tu, hata Kijerumani, Kifaransa na Kireno, lugha zote hizi zinatishiwa na uwepo duniani kote kwa Kiingereza kinachosambaa kama ugonjwa wa ebola. Utalielewa hili vizuri ukiwatazama vijana wa Kichina wanashindania usemaji fasaha wa Kiingereza katika vipindi vya redio nchini China au vile watoto wa Kifaransa na Kijerumani wanavyowania kukimanya Kiingereza yaani “Kiswahili cha dunia,” chambilecho hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Utaelewa hili ukasikiliza maneno kama yale ya mama mmoja aliyepiga simu katika Radio Citizen au Radio Maisha majuzi yale na kusema yupo Lodwar anasomea masomo ya ngumbaro, “masomo ya baada ya chamcha” kama alivyosema mwenyewe. Na ingawa lengo lake lilikuwa kuwatakia watahiniwa wa mitihani ya kitaifa heri njema na mafanikio, na kuwaomba wasiibe mitihani, alijitahidi kupita kiasi kuonesha kwamba kweli anasoma kisomo cha watu wazima. Vipi? Alihamisha ndimi mara moja na kuanza “How are you? Good Morning? Good Afternoon?

Kiingereza ndicho Kiswahili cha dunia

Kasumba kwamba mtu hakusoma kama hawezi kuzungumza Kiingereza inatawala, sio Lodwar au Kenya tu, bali dunia nzima kwa kiasi fulani. Na kama tulivyomnukuu Nyerere akisema Kiingereza ndicho Kiswahili cha dunia.

Hili tunaweza kuliona kiutumwa kuwa jambo zuri au tulione lilivyo hasa katika uhasi wake kama ithibati ya ukoloni wa Kiingereza. Mbona yule mama hawezi kuchagua kutusabahi kwa Kiturkana chake, “Ejokh?” au kwa Kiswahili na bado athibitishe kwamba kasoma bila kugeukia Kiingereza.

Sikualikwa katika kongomano la Uingereza ila nawapongeza waandalizi na wajumbe kwa ujasiri wao wa kuukemea ukoloni wa Kiingereza duniani. Siku nyingine wakinialika nitawapa maoni yangu ya mlalahoi kama yaliyomo katika makala hii.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"