Kiswahili bado ni mtoto wa kambo huku kwetu Kenya

Imepakiwa Wednesday January 30 2019 | Na KEN WALIBORA

Kwa Muhtasari:

Hata katika mapambano dhidi ya ufisadi kuna chembechembe cha utambuzi wa Kiswahili katika harakati na hamkani za kitaifa.

KINA CHA FIKIRA

MNAMO wiki iliyopita nilihudhuria kongomano la kitaifa dhidi ya ufisadi.

Na mpaka sasa sijui kwa nini ndugu zetu Watanzania hupenda kuuita ufisadi rushwa.

Sikuwa na hakika kama lilidhamiria kutuhamasisha dhidi ya ufisadi au kutufundisha mbinu mwafaka zaidi za ufisadi.

Nilitoka huku nikiwa na mseto wa matumaini na kutokuwa na matumaini.

Matumaini kwa sababu kwa mara ya kwanza niliona Wakenya wanajadiliana waziwazi na tena katika mawanda rasmi kabisa kile wanachokiona kama janga la kitaifa.

Bango la kongomano lilikuwa kauli mbiu katika maandishi ya Kiswahili yanayosema: “Pamoja tuangamize ufisadi.”

Neno ‘pamoja’ siku hizi linabeba vivuli vya mirengo ya kisiasa, lakini hilo lisitufumbe macho tusione fahari ya kongomano kuongozwa na kauli mbiu iliyoandikwa kwa Kiswahili.

Haiwi hivyo siku zote.

Hata katika mapambano dhidi ya ufisadi kuna chembechembe cha utambuzi wa Kiswahili katika harakati na hamkani za kitaifa.
Nilitaka kuona kama wajumbe wa kongomano wataruhusiwa kutoa maoni yao kwa uwazi na ujasiri. Pili nilitaka kuona kama Kiswahili kitapewa kipaumbele katika mdahalo mzima. Kuhusu utoaji wa maoni, wajumbe wa kawaida kama mimi hatukuruhusiwa kupaaza sauti. Tuliundiwa wenzo wa mtandao mahsusi kutuma maoni yetu ambayo yalirushwa kwenye viwambo. Ni juu yako ewe msomaji kuamua kama tija ya kuruhusiwa kuandika maoni kunafidia hasara ya kutoruhusiwa kutamka waziwazi kila mtu kwa kinywa chake mwenyewe.
Niliona kwamba wote waliozungumza ni wale waliokuwa wameratibiwa kuzungumza. Mama mmoja aliyejaribu kupaaza sauti muda mfupi kabla rais Uhuru Kenyatta kuingia ukumbuni, alitoswa nje. Mpaka sasa sijui alichotaka kukisema hasa maana hawakumpa fursa ya kumwaga dukuduku la moyoni mwake. Je, huenda ikawa yule mama (ambaye kwa mbali nikidhani alikuwa anazungumza Kiswahili), alikuwa na suluhisho (napenda hili neno hapa kuliko suluhu) kwa janga la ufisadi nasi tumemtilia mguu wa kausha?
Basi tuje kwa wasemaji walioratibiwa kuzungumza. Idara muhimu serikalini ziliwakilishwa, si bunge la Senati, si bunge la taifa, si serikali kuu, si serikali za kaunti, si idara ya mahakama, si walinda usalama na wapelelezi wa jinai. Isitoshe, tasnia mbalimbali pia ziliwakilishwa ikiwemo ile ya vyombo vya habari, muungano wa wanataaluma, dini na vijana. Karibu kila msemaji alizungumza Kiingereza, kama nilivyotarajia. Hata balozi wa Marekani Robert Godec alipowasalimu wajumbe kwa Kiswahili, “Humjambo? Niaje?” walionekana kushangaa.

Kiswahili

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Bw Hajji ndiye peke yake aliazimia kuwasilisha hotuba yake kwa Kiswahili.

Alifafanua kwa Kiswahili fasaha kidogo hamasa yake ya kuangamiza ufisadi na changamoto zinamkabili yeye na idara yake. Kama kuna mtu aliyeeleweka vizuri zaidi na Wakenya waliomsikiliza redioni au kumtazama kwenye runinga basi ni huyu Bw Hajji. Baadaye rais Uhuru na Raila walijaribu kutupatupa maneno mawili matatu ya Kiswahili. Wengine wote walikuwa wanawahutubia mabalozi wa kigeni.
Hitimisho: Kiswahili bado ni mtoto wa kambo nchini Kenya.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara" 

Share Bookmark Print

Rating