Ni muhimu mwandishi kutofautisha matbaa mbalimbali

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  15:19

Kwa Muhtasari

Ni muhimu mwandishi kubaini ni mashirika gani ya uchapishaji ambayo hupendelea tanzu fulani kuliko nyingine. Kwa mfano kuna mashirika ambayo huchapisha fasihi ya watoto kwa wingi.

 

Na ALEX NGURE

KUNA matbaa nyingi ambazo ziko tayari kuchapisha kazi zozote 'nzuri’ bora tu, ziwe zimetimiza vigezo na viwango wanavyotaka wenyewe wachapishaji.

Lakini aghalabu matbaa nyingi haziweki wazi vigezo na viwango vyenyewe, isipokuwa pale ambapo wamemjukumisha mwandishi fulani. Hivyo mara nyingi mwandishi anakuwa kama mfa maji anayetapatapa kwenye bahari yenye kina kirefu bila kuwa na usaidizi wowote.

Hata hivyo, ni muhimu mwandishi kubaini ni mashirika gani ya uchapishaji ambayo hupendelea tanzu fulani kuliko nyingine. Kwa mfano kuna mashirika ambayo huchapisha Fasihi ya Watoto kwa wingi.

Pana uandishi wa namna mbili. Kuna ule wa kitaaluma, unaohitaji kutoa maelezo ya kitaaluma kuhusu jambo fulani. Uandishi huu huwa na uyakini na hutoa kauli maalum kuhusu mada fulani ya kitaaluma.Nao una kanuni zake.

Pili, kuna uandishi wa kisanaa unaoizalisha fasihi-andishi. Uandishi huu huzalisha kazi za kubuni zenye misingi katika maisha yanayofahamika kwa binadamu. Uandishi wa aina hii humtaka msanii kuwa na macho yanayopenya katika jamii yake, ili aweze kubuni sanaa itakayosawiri maisha halisi ya jamii yake vile anavyoyaelewa na jinsi yanavyoeleweka na wanajamii.

Uandishi ni kama upishi.Kwa mfano ingawa mchele ni mmoja, mapishi ni tofauti. S A Mohamed anasisitiza kuwa ni vigumu kuandika bila kupata msukumo wa hisi.

'Mwandishi aandikapo huanza yeye mwenyewe kufumwa na hisi fulani, ambazo hujaribu kuzitoa na kuziwasilisha kwa njia ya maandishi kwa hadhira yake. Na katika kufanya hivyo, mwandishi huwakoleza wasomaji wake kwa kutegemea aina za hisi alizofumwa nazo na ubingwa wake wa kuchungua na kupanga maneno’

 Hatua ya awali kumfaulisha msanii katika taaluma hii ni kusoma kwa mapana na marefu. Kwa kusoma kazi za watu wengine utaweza kubaini ubora au udhaifu wa kazi hizo na kukadiria kiwango cha kazi unayokusudia kuandika. Sifa kuu za kazi yoyote ya kubuni ni kuwa:

-Inaundwa kutokana na fikra au hisi za mwandishi fulani. Hisia na fikra za mwandishi aghalabu hupatikana kutokana na jamii yake finyu au jamii yake pana (kijiji, wilaya, gatuzi, nchi nzima au ulimwengu wote)

-Inabeba mawazo,fikra, falsafa na hisi za mwandishi katika mtazamo wake wa kibinafsi, na kuziwasilisha kwa wasomaji wanaoitwa hadhira katika fasihi.

-Inaweza kuhusiana na maisha, utamaduni,uchumi,siasa,dini,elimu, saikolojia na nafsi ya mwandishi mwenyewe na jinsi ayaonavyo mambo mbalimbali ya nje (mazingira yote ya nje: ardhi na anga na vyote  vilivyomo juu yake na ndani yake) na mazingira ya ndani (mambo yanayohusiana na roho, miungu,mashetani na nguvu zozote tisizoziona na ambazo mwanadamu huona zinaendesha ulimwengu tulio nao).

Jambo linalofuata baada mfumo wa hisi ni ubunaji. Ubunaji hautokani na ombwe tupu, bali unatokana na hali halisi-hali ya mambo ambayo msanii ameyaona, ameyasikia, ameyanusa, ameyaonja, ameyahisi au ameyasoma pahala. Hakuna ubunaji ambao  hautegemei mambo ambayo yamo kwenye uzoefu na tajriba zetu au tajriba za jamii zetu.

Udongo wa mfinyanzi

Kwa kutumia kipawa chake cha kubuni, msanii atayafinyanga  upya mambo hayo ili kuunda umbo la kisanaa. Hali hii tuimithilishe na udongo wa mfinyanzi utumikao kufinyangia vyombo kadhaa vya usanii na mapambo na visivyokuwa vya mapambo.Udongo huo ni kitu ambacho sote twakiona na kukigusa kila siku. Lakini hatuvutiki nao mpaka pale msanii (mfinyanzi) anapouchukua na kuutayarisha  na kuutengeneza kwa kuutumia kufinyangia vyombo au mapambo yenye kuvutia. Ubunaji wa hadithi unalingana na ufinyanzi wa aina hii.

Kwa upande mwingine, maneno ni kitu kilichopo ndani ya lugha zetu. Ni kitu tunachokijua na kukitumia kila siku na wala hatuvutiwi nayo kila wakati. Lakini  msanii (mwandishi) anapoyachukua maneno hayohayo na kuyabebesha maana na hisia fulani kwa kuyatumia kisanaa, basi huwavutia wengi.

Mara nyingi upeo wa hisi na kiwango chake hufikiwa pindipo mwandishi akitekeleza yafuatayo: Akiweza kupata mada au anuani mpya ambayo waandishi wengine hawajaiandikia au ambayo waandishi wengine wamewahi kuiandikia, lakini hawajapata kuipa mwelekeo au mtazamo  mpya.

  alex.ngure@yahoo.com