http://www.swahilihub.com/image/view/-/2758636/medRes/1040993/-/hpl66o/-/nyonyesha.jpg

 

Fasihi andishi na saikolojia ya mtoto

Mwanamke amnyonyesha mtoto

Mwanamke amnyonyesha mtoto. Picha/MAKTABA 

Na JENITHA KIMAMBO

Imepakiwa - Thursday, April 5  2018 at  12:51

Kwa Muhtasari

Watoto hupendelea sana fantansia; mambo ya ajabuajabu ambayo hayawezekani katika ulimwengu halisi.

 

FASIHI ni sanaa inayotumia lugha ili kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyokusudiwa.

Kuna aina kuu mbili za fasihi ambazo ni fasihi simulizi na fasihi andishi. Fasihi simulizi ni fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya mdomo na kusambazwa kwa njia ya mdomo. Kadhalika, fasihi andishi ni aina ya fasihi ambayo huwasilishwa kwa njia ya maandishi na kusambazwa kwa njia ya maandishi.

Katika miaka ya hivi karibuni (1990) kumeibuka fasihi ya watoto.

Fasihi ya watoto ni aina ya fasihi ambayo imeandikwa na watoto au na watu wazima lakini ikiwalenga watoto kimaudhui. Wahusika wake wakuu ni watoto. 

Dhana ya neno saikolojia imebebwa na tabia. Mtoto, tofauti na mtu mzima, kuna vitu ambavyo anavipenda zaidi. Mathalan kusimuliwa hadithi, kucheza, kuangalia picha, kusikia au kuona mambo ya ajabuajabu ambayo hayawezekani katika ulimwengu halisi (fantansia), safari na misako, upepelezi. Ili kuvuta saikolojia ya mtoto waandishi wa kazi za fasihi huandika mambo wayapendao watoto.

Dhana ya mtoto ni tata inaweza kufasiliwa kwa mitazamo mbalimbali kama vile; Mtoto ni mtu yeyote chini ya umri wa miaka kumi na minane. mtoto ni mtu yeyote aliye chini ya uangalizi wa wazazi au walezi, ni mtu asiyeweza kujiamulia mambo yake mwenyewe pasipo msaada wa wazazi au walezi. Kwa mtazamo wa dini sisi sote ni watoto wa Mungu.

Fasihi andishi inajali, kusisitiza na kuendeleza saikolojia ya mtoto. Riwaya ya Marimba ya Majaliwa iliyoandikwa na Edwin Semzaba mwaka 2008, Safari ya Prospa iliyoandikwa na Elieshi Lema mwaka 1995, na Moto wa Mianzi iliyoandikwa na MM Mulokozi mwaka 1996 zimegusia zaidi saikolojia ya mtoto. Yafuatayo ni mambo wanayoyapenda watoto yaliyoelezewa katika riwaya hizo:

 

Michezo

Watoto wanapenda sana kucheza. Kucheza ni miongoni mwa haki za watoto. Michezo husaidia kuimarisha afya na ni sehemu ya burudani katika makuzi ya mtoto. Ifuatayo ni baadhi ya michezo iliyojibainisha katika  riwaya ya Marimba ya Majaliwa.

·       Dalili zilipoonyesha kuwa simba anataka kumrukia yule swala, bibi akampiga yule simba mgongoni. Simba akaruka pembeni akitoa mlio. Wakati huohuo akizungukazunguka kumtafuta aliyempiga ... Bibi akamfuata tena na kuuvuta mkia wake… Bibi alimkaribia na kumvuta sikio. Safari hii simba aliamua kukimbia (uk 76).

·       Wakakaa juu ya mgongo wa mtoto wa tembo kwa nguvu, pum! Mtoto wa tembo akapiga kelele za maumivu, mama yake akamgeukia mwanaye na kumtazama … Bibi aliutua tena ungo kwenye mgongo wa mtoto wa tembo, pum! Mtoto wa tembo akapiga tena kelele za maumivu … Bibi alipandisha tena ungo na kwenda kulivuta sikio la kushoto la mama tembo. Mama tembo alistuka na kupeleka mkonga wake haraka sikioni … Bibi alimvuta sikio lake la kulia … akatua nyuma kabisa karibu na mkia … Bibi akaamua kumpigapiga mgongoni kama anapiga ngoma. Tembo akashindwa kuvumilia, akatimua mbio. Mtoto naye akamfuata mama yake, ambaye alionekana kupandwa na kichaa (uk. 77).

 

Hadithi

Watoto wanapenda kusimuliwa hadithi. Mara nyingi hadithi zinazowavutia ni zile zenye wahusika wanyama, majitu, mazimwi na vitu ambapo wahusika hao hupewa sifa za kutenda kama binadamu. Ifuatayo ni hadithi iliyopo kwenye riwaya ya Marimba ya Majaliwa;

Paukwa…

Pakawa…

Hapo zamani za kale, kabla Mjerumani hajaingia Tanzania, Kibo na Mawenzi walikuwa kina dada waliopendana sana. Waliishi vizuri kwa muda mrefu, lakini Mawenzi akaanza uvivu wa kupika. Kila siku Mawenzi alipoomba moto wa kuwashia jiko lake la kupikia, Kibo alimpatia.  Mawenzi alikuwa hafiki na ule moto nyumbani kwake. Alirudia njiani na kukuta Kibo amekwishaivisha chakula. Basi, Kibo alimkaribisha dada yake, wakala wote. Hali hii iliendelea kwa muda mrefu. Mawenzi huenda kuomba moto, badala ya kwenda kwake kukoka moto apike, yeye alikuwa akibana mahali hadi dada yake Kibo aivishe, kisha aende kula.

Siku moja alipewa moto kama kawaida lakini hakuenda nyumbani. Alijificha. Alipoona kuwa dada yake atakuwa ameivisha akajitokeza. Wakati dada yake, Kibo alipokuwa akipakua chakula ugomvi ukatokea. Dada, Kibo alimwambia Mawenzi. Nimechoka kukulisha kila siku. Kuanzia leo, uache uvivu wako na ujipikie chakula chako! Mawenzi alikasirika sana. Akaukamata mwiko Kibo aliokuwa anapakulia ugali, akachota ugali na kumpiga nao Kibo kichwani. Ugali ulisambaa kwenye kichwa cha Kibo, na tangu wakati huo, Kibo akawa na kichwa cha kung’aa. Mawenzi alikimbia na kwenda kuishi mbali. Haya, hadithi yangu kama ni nzuri ichukue na kama ni mbaya niachie mwenyewe (uk. 58).

 

Safari na Msako

Watoto wengi wanapenda safari. Mama akiwa anajiandaa wanajua kabisa anatoka hivyo nao hujitayarisha kwa safari hiyo. Watoto hupendelea zaidi safari za msako, kufanya safari ambayo itamwezesha kugundua au kupata kitu kilichopotea, ndio maana kuna mchezo wa kombolela ambao wachezaji hujificha na mwenye zamu huwatafuta. Zifuatazo ni safari zilizofanywa na Prospa kwa lengo la kumchafua mpwa wake, Merisho katika riwaya ya Safari ya Prospa.

“Nakwenda Dar es Salam kumtafuta Merisho kwa ndugu yao Mohamed”, Prospa alisema. Aliamini kwamba Dar es Salaam haiwezi kuwa mbali sana. Prospa alifunga safari kutoka TPC hadi Moshi mjini. Alifanikiwa kupata gari liendalo Dar es Salaam lakini alishushwa njiani kwa sababu hakuwa na nauli ya kutosha.

Aliposhushwa kwenye gari kwa sababu hakuwa na nauli ya kutosha, alitambua yupo Same, alikutana na Sara Edison. Wakaungana wote kuanza safari ya Dar es Salaam kumtafuta Merisho kwa ndugu wa Mohamedi kwani waliamini kuwa atakuwa amemuiba kwa kuwa hakuwa na mtoto. Walipofika Dar es Salaam, waliulizia Manzese ambapo alikuwa akiishi kaka Petro.

Walipompata kaka Petro, aliwapa nauli ya kwenda Zanzibar kwa ajili ya kumsaka Merisho na kuwaambia wasirudi tena Mazense kwa kuwa hali yake ya maisha haikuwa nzuri hivyo hakuweza kuwahudumia. Walifika Zanzibar lakini hawakufanikiwa kumpata Merisho.

Walirudi hadi Manzese, walikutana na Mansa na Tofa. Hawa walikuwa watoto wa mitaani. Sara alipelekwa kwenye kundi la wasichana. Prospa, Mansa na Tofa walianza kumsaka mjomba Feliksi. Mjomba Feliksi alikuwa anamjua baba yake Merisho hivyo waliamini wakifika kwake watajua anapoishi baba yake Merisho, hivyo watafanikiwa kumpata Merisho na kurudi naye TPC  kwa dada yake.

 

Fantansia

Fantansia ni mambo ya ajabuajabu ambayo hayawezekani katika ulimwengu halisi. Watoto hupendelea sana fantansia kwani ni sehemu ya kiburudisho kwao. Zifuatazo ni baadhi ya fantansia katika riwaya ya Marimba ya Majaliwa;

Ø  Yule papa taratibu akaanza kugeuka binadamu. Kilianza kichwa, kisha kifua na mwisho tumbo na kubakia umbo la samaki aina ya nguva kuanzia kiunoni kwenda miguuni. Kisha, huyo nguva mtu akatumia mapezi ya mkiani kutembelea (uk 5).

Ø  Wakati wowote  utakaposikia una njaa, ingia hotelini na kugusa rubi yako kisha ukitaje chakula cha mtu yoyote atakayekuwa anakula (uk 21).

Ø  Aliwapiga chenga za ajabu na zenye maudhi, huku maji yakirushwa hewani kama vile yalitoka kwenye pampu ya maji ya kuzimia moto (uk 8).

Ø  Bibi alitoa pumzi chafu kwa nguvu, sauti yake kama mzinga. Basi, vile vibwengo vyote vikakimbia na kutawanyika huku vimekamata pua zao (uk 26).

Ø  Kuna kila aina ya mitambo (tumboni kwa bibi) wa kutoa cheche za moto, wakutoa mbigili, yaani kila aina ya mitambo (uk 26).

Ø  Nyangumi alipofungua mdomo, ukubwa wake ulikuwa kama kontena mbili kwa pamoja (uk 37).

Ø  Tumbo la nyangumi kuwa kubwa na lenye kuweza kuingiza kontena kumi kwa wakati mmoja . Mayai ya nyangumi yalikuwa makubwa kama magunia yaliyojaa mchele (uk 37).

Ø  Bibi alichukua kijani na kukichomeka juu ya nywele za Majaliwa. Palepale Majaliwa akajiona amevaa koti, suruali na viatu vya baridi.

 

Kuishia na ushindi

Watoto hupenda  mambo wanayoyafanya kuishia na ushindi. Mhusika mkuu ambaye ni mtoto akishindwa, mtoto hukata tamaa ya kuendelea kusoma. Kwa kuwa mhusika mkuu ni mtoto, watoto hupenda kusoma kitabu na kushangilia ushindi pamoja na mtoto mwenzao kwa kujiona ni sehemu ya ile hadithi. Ufuatao ni ushindi walioupata Mugoha na Sapi katika riwaya ya Moto wa Mianzi.

Kwa upande wetu sisi wahukumiwa, ni vigumu kueleza hisia tuliyoipata baada ya kusikia maneno ya Sakarani.

Tulikuwa tumekwisha jiandaa kufa. Hivyo maneno haya yalikuwa kama talasimu ya ajabu iliyoturejesha duniani  kutoka kuzimu. Hatukujua kama tutabasamu au tulie, tufurahi au tusikitike. Tulijihisi kama watu wapya. Tulihisi kuwa pengine mahoka wetu walikuwa wametunusuru ili tuendelee kuishi na kukamilisha kazi walioianza wazee wetu ambao watanyongwa leo mbele ya umati huu (uk. 97).

Kupongezwa pindi wafanyapo vizuri

Watoto hupenda kupongezwa na kupewa zawadi kama ishara ya kutambua mchango wao katika jambo husika. Kumpongeza na kumpa zawadi mtoto ni motisha ambayo itasababisha kufanya jambo lingine kwa ufanisi zaidi. Zifuatazo ni pongezi walizopata Prospa, Sara, Mansa na Tofa katika riwaya ya Safari ya Prospa.

Mjomba aliwaamba wafikirie mradi ambao wataweza kuuendesha, halafu yeye na Mzee Mchau watakuwa wanawapa ushauri wa mara kwa mara. Juu ya hayo, Mjomba aliongeza, “Mimi nitawaongezea pesa nyingine, lakini nitawapa baada ya kuona bidii yenu ilivyo” (uk. 164).

Mjomba alipouliza kuwa anataka zawadi gani, alifikiri kwa muda mrefu. Alifikiri sana, halafu alisema, “Mimi nataka baiskeli ili inisaidie wakati wa kwenda shule au wakati nikitumwa mjini”. Lakini Prospa alikuwa akimfikiria Mustafa. Aliwaza: Merisho amepatikana, sasa nikipata baiskeli juu ya huo ushindi, Mustafa ataniheshimu zaidi.

Mjomba Feliksi alisema “Najitolea kuwasomesha vijana Mansa, Sara na Tofa, kama wanapenda”. Wao walikataa. Walisema kwamba walikwisha acha shule zamani, hawataweza tena kurudi shule kusoma na kufanya mitihani (uk. 166).