Kiswahili cha kitaaluma si kigumu kama tunavyodhani

Imepakiwa Tuesday November 20 2018 | Na MGENI WETU

Kwa Muhtasari:

Baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo kwamba istilahi za Kiswahili ni ngumu kuliko hata za Kiingereza.

Na ERASTO DUWE

KATIKA mijadala mingi iliyohusisha matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo kwamba istilahi za Kiswahili ni ngumu kuliko hata za Kiingereza.

Watu hao wamekuwa na mtazamo kuwa ni vyema Kiingereza kikaendelea kutumika kwa kuwa wanakiona ni rahisi katika ufundishaji na ujifunzaji kuliko Kiswahili.

Hata hivyo, katika makala hii, lengo si kuibua mjadala wa Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika viwango mbalimbali ya elimu, la hasha, hilo limeshalijadiliwa sana katika mijadala mingi na watu mbalimbali wametoa maoni.

Katika makala hii lengo hasa ni kujadili ikiwa kweli Kiswahili cha kitaaluma ni kigumu au la.

Awali ya yote tunapozungumzia Kiswahili cha kitaaluma tunamaanisha aina ya lugha (msamiati na istilahi maalumu) itumikayo kufundishia masomo mbalimbali kama vile Biolojia, Kemia, Hisabati, Jiografia na masomo mengineyo katika ngazi mbalimbali za elimu.

Jibu la mtazamo huo kwamba Kiswahili hicho ni kigumu linaweza kuwa na sura mbili tofauti. Ikumbukwe kwamba, watumiaji wengi wa Kiswahili wamezoea kutumia Kiswahili cha kawaida kwa ajili ya kukidhi mawasiliano yao.

Kiswahili cha mawasiliano, kinajichomoza katika sura mbili. Wapo watumiaji wa Kiswahili wanaokitumia katika mawasiliano bila kujali urasmi wake.

Kwa maneno mengine, wao huongea tu bila kujali wanazingatia taratibu za lugha hiyo au la. Kwa sababu hiyo, hata kama wanabananga kwao si tatizo ilimradi tu wakidhi mawasiliano yao.

Kwa upande mwingine, wapo watumiaji wa Kiswahili wanaokitumia huku wakijali sana uzingativu wa taratibu au sarufi ya lugha.

Miongoni mwa hao ni pamoja na wasomi katika uga huo wa Kiswahili na baadhi ya vyombo vya habari.

Lugha yoyote ya kufundishia, kwa kawaida inaangukia katika kundi la lugha rasmi.

Urasmi huo hujitokeza katika kufuata taratibu mbalimbali (sarufi ya lugha) na kuwa na istilahi maalumu za taaluma husika tofauti na lugha ya kawaida ya mawasiliano.

Ikumbukwe pia kwamba hata Kiingereza ambacho baadhi ya watu hukiona kuwa ni rahisi kama lugha ya kufundishia na kujifunzia, dai lao si la kweli.

Kuna tofauti kati ya Kiingereza cha kawaida kitumikacho katika mawasiliano na kile kitumikacho katika ufundishaji wa masomo mbalimbali. Tofauti yake ni kwamba, Kiingereza kitumikacho kufundishia, kina istilahi nyingi na pengine kina mfumo maalumu kutegemeana na somo husika.

Haiyumkiniki wasemao Kiingereza cha kufundishia ni rahisi kuliko Kiswahili, wanaongea hivyo kwa sababu tu ya mazoea, yaani Kiingereza wamekizoea kufundishia na kujifunzia hususan katika kiwango cha sekondari na vyuo.

Kiswahili kinaonekana kigumu kwa kuwa hakitumiki kama lugha ya kufundishia katika viwango tajwa. Istilahi zake zinaonekana ngumu kwa kuwa hakijazoeleka.

Endapo kingekuwa kinatumika tangu muda mrefu uliopita kama ilivyo kwa Kiingereza, wasemao hivyo wangekizoea na kukiona rahisi kama wakionavyo Kiingereza.

Hata hivyo, ifahamike kuwa, lugha ya kutolea taaluma mbalimbali ni tofauti na lugha ya kawaida ya kimawasiliano.

Utofauti huo hutokana na sababu tulizokwisha zitaja kwamba, lugha ya kufundishia ina istilahi zake kutegemeana na somo husika; ina mfumo wake maalumu na nduni nyinginezo.

Istilahi kutotumika sana

Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa, Kiswahili cha kufundishia kinatazamwa kuwa kigumu kwa kuwa istilahi zake hazitumiwi sana.

Kwa upande mwingine, Kiswahili cha namna hiyo si kigumu kwa kuwa tayari zana kama kamusi zipo na endapo ufundishaji kwa Kiswahili utafanyika, kitazoeleka na kuonekana cha kawaida kama Kiingereza kinavyochukuliwa na watu wenye mtazamo huo.

Kilicho muhimu ni Watanzania kujikubali kuwa tuna Kiswahili kama tunu yetu ya kujivunia. Ugumu au urahisi wa maneno katu usiwe sababu ya kukidunisha Kiswahili kikakosa nafasi yake stahiki.

Kilicho chako hakiwezi kuwa kigumu na itoshe tu kusema kuwa hata hicho Kiingereza tunachokikumbatia nacho kina maneno lukuki magumu

Lakini haya hayaonekani, yanaonekana maneno magumu ya Kiswahili. Tafadhalini Watanzania tupende kilicho chetu.

 

Erasto Duwe anapatikana kwa simu namba +255713646322

Share Bookmark Print

Rating