Asili ya sanaa

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Tuesday, April 3  2018 at  17:27

Kwa Muhtasari

Tunaangalia mitazamo miwili ya asili ya sanaa; mtazamo wa kidhanifu na mtazamo wa kiyakinifu.

 

ASILI YA SANAA

TUNAANGALIA mitazamo miwili ya asili ya sanaa; mtazamo wa kidhanifu na mtazamo wa kiyakinifu.

1.      Mtazamo wa kidhanifu

Kwa mujibu wa mtazamo huu, inaaminika kuwa chimbuko la sanaa (ikiwemo fasihi), lilitokana na Mungu.

Mwanasanaa huipokea sanaa hiyo kutoka kwa Mungu baada ya kuandaliwa ipasavyo.

Ni mtazamo wa wanafalsafa wa Kigiriki na Kirumi mathalan Socrates, Plato na Aristotle waliouchunguza ulimwengu wa sanaa na asili yake.

Kwa mujibu wa wanafalsafa hawa, maandalizi ya sanaa huonekana kama shughuli ya kiungu inayomwiga Mungu ambaye ndiye msanii wa kwanza.

Sanaa hutoka kwa Mungu na kumfikia msanii ambaye huipitisha kwa jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo:

Mungu - Sanaa - Msanii - jamii

Mtazamo huu unapinga wazo kwamba sanaa hutokana na jitihada za akili na mikono ya binadamu.

Sanaa hupokelewa kutoka kwa mikono ambayo binadamu hana uwezo wa kuiona.

Mtazamo huu unamtenga msanii na jamii yake na wakati uo huo kumwinua na kumfanya kuonekana kuwa wa ajabu na aliye karibu zaidi na Mungu kuliko watu wengine wa kawaida.

Mtazamo huu umetumika sana kufafanua ushairi, hasa ule wa zamani.

Katika utamaduni wa Kiswahili mtazamo huu umetumiwa na wataalamu kama vile:

F.V. Nkwera (1985) anasema kwamba: “Fasihi ni sanaa inayoanzia kwa Muumba, humfikia mtu katika vipengele mbalimbali … ni hekima ambayo mtu ameshirikishwa apate kumtambua muumba wAke.”

2.      Mtazamo wa kiyakinifu

Kulingana na mtazamo huu, asili ya sanaa ni mazingira halisi ya jamii papa hapa duniani. Sanaa yoyote ni zao la mazingira, nayo hususan ya mwanzo, ilifungamana na kazi na uzalishaji mali.

Waasisi wa mtazamo huu wanasema kuwa tangu dunia ilipoumbwa wanadamu wamekuwa wakitafuta njia na nyenzo za kuendeshea vyema na kuendeleza mbele maisha yao.

Kupitia utafiti na majaribio chungunzima ya kisayansi ya kutafuta ukweli kuhusu mazingira, sayansi imefaulu kuelezea chanzo cha binadamu, jinsi alivyoanza kufanya kazi, na historia yake yote tangu mwanzo wake hadi sasa.

Kwa muhtasari, sanaa ni kazi ya mikono na akili ya binadamu; nayo aghalabu ina umbo dhahiri lenye maana na dhana maalumu.

Ni kazi za binadamu zenye mwigo wa uyakini uliofungamana na wakati, mazingira na mifumo ya jamii zinazohusika.