Barua iliyoniliza

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Thursday, April 26  2018 at  09:34

Kwa Muhtasari

Unashauriwa ufanye kitu kwa kiasi sababu hujui kinaweza kuwa na madhara kiasi gani.

 

Anasimulia Gift;

BARUA hii inanikumbusha mengi sana na kila nikiisoma najikuta moyo unaingiwa na ganzi na ninakosa furaha na sina amani moyoni, naishia kulia tu.

Mimi na Blenda tulikuwa ni marafiki tuliopendana sana.

Urafiki wetu ulikuwa ni zaidi ya undugu sababu hakuna tulichofichana,

Kuna muda tulitaniana mpaka katika mambo ya ndani sana.

Siku moja niliamua kumtania Blenda kuhusu mpenzi wake ambaye aliaga atasafiri kwenda Arusha kwa wiki mbili kwenye harusi ya rafiki yake. Nikatumia nafasi hiyo kutengeneza utani huo.

Baada ya harusi nikampigia simu Shem na kumuomba anitumie picha alizopiga na Bi Harusi yaani yeye na bi harusi.

Aliponitumia, basi nikaitumia ile picha kumdanganya Blenda kuwa Daniel kumbe sio mwanaume sahihi kwako na siamini kama Shem D muda wote alikuwa anakuigizia.

Aliuliza kwa mshituko mkubwa: "Wee G una maana gani?

Nikamjibu huwezi amini, Dani ameoa na jana ndo ilikua harusi yake.  Blenda akasema kwa kujiamini mmh! Hakuna kitu kama hicho, sababu hujui ni ahadi gani tuliyoipanga mimi na D.

Nikamuuliza unakifua nikupe yaliyojili? Mbona D ni muhuni!

Mimi niliona nikae kimya tu.  Nikamuonesha ile picha ambayo Dani alinitumia. Hapo Blenda akakaa kimya na kuanza kutetemeka.

Nikamwambia shoga, ngoja nikuoneshe na sms alizokuwa akinitongoza. Nikatoa simu na kumuonesha. Kumbe sms zenyewe nilizitengeneza kwa kutumia simu yangu kipindi Blenda ameenda kuoga.  

Alipotoka tu, nikachukua simu yake nikaandika, kisha nikaedit jina la Blenda kwenye simu yangu na kuandika Shem D.  SMS 2 zilizosomeka hivi;

1. Shem huwa unanichanganya kwa kifua chako. Natamani siku moja nikunyonye.

2 Plz, usimwambie B, namjua anapresha.  Anaweza kufa plz and plz.

Blenda alianza kulia na akachukua simu yake ili ampigie Dani.

Kwa bahati mbaya simu yake ilikuwa haipatikani.

Akiwa bado anahangaika, ghafla simu yangu ikaita.

Kuangalia alikuwa ni baba yangu hivyo ikanilazimu kutoka nje nikaongee kisha. Nilipanga nikirudi nimwambie Blenda kuwa nilikua namtania na nimkumbushe jinsi Dani alivyotuaga na kumuonesha kuwa zile SMS ni kutoka kwenye simu yake mwenyewe.

Nilipomaliza kuongea na baba na  kurudi ndani, sikumkuta Blenda na nilipojaribu kupiga simu yake ikawa haipatikani

Mara zikapita siku mbili bila B kuonekana wala simu kupatikana. Ikabidi nimpigie simu mama yake, naye akashtushwa na habari ile.

Tukatoa taarifa polisi na kuendelea kumtafuta.

Mara ikatolewa taarifa kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akutwa amekufa kwenye stoo ya hostel. Kwenda kuangalia sikuamini. Alikuwa ni Blenda, niliumia sana na kwa haraka sikuweza kutambua sababu ni nini.

Kilichokua kinaniuma kwanza ni kifo chake na pili ni jinsi wenzetu walivyokuwa wakinihoji na wengine kunipa pole.

Nguo

Baadaye familia ilihitaji nguo za marehemu na ikanibidi nikachambue nguo zake sababu tulikua tunaweka pamoja. Katika kuzichambua ndipo nikakutana na barua ambayo inanifanya nisimulie kisa hiki.

Baada ya kuwapa zile nguo na msiba kumalizika nikaingiwa na shauku ya kutaka kujua kilichoandikwa ndani ya barua ile. Nikarudi hostel,  nikaichukua na kuiweka kwenye mkoba kisha nikaenda nayo nyumbani ili nikaisomee huko.

Nilipofika nyumbani nilienda moja kwa moja hadi chumbani; nikajifungia mlango na kuanza kusoma barua iloanza kwa neno;

Dear G
am,

Sorry kwa kukuacha peke yako ila imenilazimu. Plz, naomba nifikishie ujumbe huu kwa Daniel.

Mwambie, Moyo ameshaugawa na amesahau ahadi zote alizoniahidi. Mkumbushe kwamba hata titi la bibi linathamani ingawa wengi hudharau kutokana na mikunjo na kusinyaa kwake.

Mwambie, Nimevuta subira sana, nimeambulia vumbi ambalo limeniuguza na nimeshindwa kuvumilia, nimechoka kulialia.

Mwambie, Nimeshindwa kuvumilia sababu Mungu kanipa moyo mdogo ambao ulikua kwa ajili yake tu ila sio kuvumilia alichokifanya na nashukuru sababu sikuwahi kumpenda mtu mwingine zaidi yake na wewe ni shahidi.

Mwambie, Nilikuwa siwezi kulala bila kumuona ama kuisikia sauti yake na sitaki kuamini kwamba kumbe nilikua najisumbua dah! Basi sa ivi nitalala bila kumsumbua na hata sumbuliwa tena na SMS wala simu zangu.

Sanda

Mwambie, Yeye anajifunika shuka huku kichwa cha mpenzi wake kikiwa kifuani kwake ila mimi mwenzie shuka langu ni sanda na mchanga mzito kifuani kwangu.

Mwambie, Namuombea maisha ya furaha na amani ila bado nakumbuka alivyokua akinisifia na siamini kama alikua akinidhihaki.

Mwambie,
Nakumbuka tulikula, kunywa, kucheza na kutaniana ila nakoenda mwenzie sitokula, kunywa wala sina wa kutaniana nae.  Ila bora nikaishi kwenye giza na wadudu watakaonila taratibu bila kunisaliti.

G usiwaamini wanaume sababu kama Dani nilivyomheshimu na kumpenda ila hakuiona thamani ya penzi langu sidhani kama utampata wa tofauti.

By Blenda

Daaah! Mungu anisamehe sababu sikukusudia na sikujua kama yatatokea yote haya. Kinachoniuma zaidi ni baada ya Blenda kupimwa alikutwa amekunywa sumu na Daniel anashutumiwa kuwa chanzo cha kifo chake. Sijui nifanye nini! Naumia saaanaa.

Jifunze: Fanya kitu kwa kiasi sababu hujui kinaweza kuwa na madhara kiasi gani.

 

Mtunzi BEATUS KUSAGA ‘Sauti ya Kasuku’

Simu: +255719368158