Binadamu viumbe waharibifu sana

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Monday, February 26  2018 at  12:09

Kwa Muhtasari

Uharibifu ni hali ya kuvuruga mpangilio mzuri uliokuwepo awali.

 

UHARIBIFU ni hali ya kuvuruga mpangilio mzuri uliokuwepo awali.

Katika dunia hii, binadamu ndio viumbe waharibifu zaidi ingawa wao ndio wenye akili kuwashinda wote wengine.

Viumbe hawa binadamu huendeleza maovu ya kiharibifu kwa njia mbalimbali kisha kwa njia zinazostaajabisha kweli. Mojawapo ya uharibifu wao mkubwa hupatikana katika ukataji ovyo wa miti. Hili ni jambo ambalo wao hulifanya bila masikitiko wala haya yoyote.

Cha kushangaza ni kuwa binadamu yuyo huyo anafahamu barabara madhara ya tendo hilo kwa maingira yakena hatimaye kwake mwenyewe. Lakini wapi! Ujuzi wake mkubwa wa mambo haujafanikiwa kumkomboa!

Pamoja na hayo ni kuwa sisi binadamu pia huwaua kiholela wanyama mwitu ati kwa kutaka vipusa,  ngozi na sehemu zao nyingine kwa sababu ya ubinafsi wetu. Binadamu pia huona rahisi kuwaangamiza viumbe ambao wao huwafikiria kuwa tishio kwao.

La kustaajabisha zaidi ni kuwa binadamu huyu huwa hasumbuki kwa vyovyote vile hata anapomtoa uhai mwenzake na wakati mwingine yeye hata hujiua mwenyewe! Hili ni jambo ambalo katu haijapata kuonekana kwa mnyama kujiua mwenyewe au hata kumuua mnyama mwenzake bila sababu yoyote. Licha ya hayo, ukweli ni kuwa tumewahi kusikia mbwa koko akamwokoa mwana wa binadamu aliyetupwa na mamake mwenye akili razini!

Maajabu mengine ni hali ambayo binadamu humbaka mtoto mdogo katika visa vingi ambavyo tumewahi kuvisikia. Je ni wapi tumewahi kumsikia mnyama akimbaka mwanawe?

Yaliyo makubwa zaidi ambayo kila uchao tunayaaona yakiendelezwa na watu ‘walioendelea’ ni yale ya mume kumuoa mume mwenzake hadharani.

Hayo kwa kweli katu hata hayafikiriki kwa mnyama kuyatekeleza.

Sasa je, inakuaje binadamu hupenda kila mara kwenda kinyume na maumbile na daima kuharibu ruwaza iliyopo?

Pengine zaidi hulka yake ya kupenda makuu kutokana na uwezo wa kipekee aliotunukiwa na Muumba wake.

Mbona asiutumie uwezo huu kuiboresha hali yake, mwenzake na dunia hii ya mola kwa jumla? Au pengine kutokana na tamaa na ubinafsi wake usioweza kutoshelezwa kwa vyovyote vile.

Ndipo yeye hujipata akiharibu kila anachokigusa?

Ama kwa kweli kiumbe huyu hawezekani ila tu kwa kutumia nguvu ili kumzuia kuendeleza maovu yanayomletea yeye mwenyewe maangamizi.