Dhana mawasiliano

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Friday, October 5  2018 at  08:24

Kwa Muhtasari

Kuwasiliana ni kupitisha ujumbe fulani.

 

MAWASILIANO ni kupitisha ujumbe fulani. Na mawasilino bora huhitaji ujumbe husika ueleweke jinsi ulivyokusudiwa na mwasilishaji wake.

Bila shaka, lugha ni mojawapo ya namna za kimsingi za kuwasilisha ujumbe.

Lugha hii huweza uwa katika maandishi au mazungumzo.

Mara nyingi binadamu huyategemea mazungumzo na mwenzake kama njia kuu ya kuwasiliana.

Hata hivyo, kuna mawasiliano mengi yanayoendelea hata bila ya mtu kusema neno. Kimya chenyewe ni namna ya mawasiliano. Kimya baina ya watu huenda kuwa kinasema,

“Sina haja nawe tena!” au, “Nakuchukia!” kimya hicho chasemekana kuwa na mshindo mkubwa sana.

Mawasiliano mengine huwezeshwa hata na rangi mbalimbali.

Hii ni kutokana na kuwa rangi huambatanishwa na maana mahsusi katika jamii zetu.

Kwa mfano, iwapo bosi atavaa nguo nyekundu, basi siku hiyo huenda akawa ni mwenye hasira.

Wafanyakazi humtoroka kwa hofu hiyo. Ila mtu anapompa mpenziwe ua jekundu, ina maana tofauti kabisa na hio.

Zaidi ya hayo ni kuwa, katika maongezi yetu, sisi huyaambatnisha na ishara za mwili na za uso ambazo hujitokeza tu bila kuziwazia mno. Ishara hizo basi huwa na ujumbe wa kipekee tena uliokamilika zaidi ya yale tuyasemayo.

Kwa mfano, iwapo mtu atatabasamu huwa ana ujumbe gani? Na kicheko je? Huenda ikawa ni furaha, bezo, uchungu, chuki au dharau katika kicheko chake. Haya yote huwasilisha ujumbe wa kipekee tena mzito.

Kumuangalia mtu machoni

Kunao watu wasioweza kuwaangalia wenzao machoni wanapozungumza nao, hii huweza kuashiria hali ya lawama fulani inayowasumbua nyoyoni; au pengine aibu ya aina yake.

Tabia nyingine ni kama kujikunakuna ovyo au hata kuumauma kucha kuashiria woga kwa yule anayeongea. Bila shaka hapa kuna mawasiliano zaidi ya yale yanayosemwa ila haya huwa yana ukweli na uwazi zaidi.

Tukichunguza vyema, bila shaka tutanufaika na mawasiliano mema zaidi nje ya maneno tu.