Dhana na dhima ya Nadharia za Kiswahili kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Tuesday, October 2  2018 at  10:32

Kwa Muhtasari

Kuna nadharia anuwai katika lugha ya Kiswahili. 

 

Na MARY WANGARI

KUNA nadharia anuwai katika lugha ya Kiswahili. Baadhi ya nadharia hizi ni kama vile:

 1. Nadharia ya sarufi

 2. Nadharia ya mawasiliano

 3. Nadharia ya maana

 4. Nadharia za kifalsafa

 5. Nadharia za kihistoria

 6. Nadharia za fasihi

 7. Nadharia ya utabia

 8. Nadharia za chimbuko la lugha ya Kiswahili

 9. Nadharia ya chimbuko na chanzo cha lugha

 10. Nadharia ya ufundishaji wa moja kwa moja

 11. Nadharia ya ufundishaji vitendo

 12. Nadharia ya kijumuia na kibinadamu

Wasomi na wataalamu wa Kiswahili wenye mitazamo tofauti tofauti wamefafanua dhana na dhima za nadharia za Kiswahili jinsi ifuatavyo:

Wamitila, (2003:22); kulingana naye, nadharia ni mawazo, dhana au maelezo yanayotolewa kuelezea hali fulani yaani chanzo chake, muundo wake, utenda kazi wake na mwingiliano wake wa ndani na nje.

TUKI (2004:300) Inafafanua nadharia kama mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani.

Mdee (2011) anaeleza nadharia kuwa mpango wa maneno uliotungwa ili kuelekeza jinsi ya kufanya au kutekeleza  jambo. Fasili hii inawiana kwa kiasi fulani na ufafanuzi wa TUKI.

Kwa mantiki hii, nadharia hubeba mawazo ,dhana au maelezo yanayotolewa kwa nia au lengo la kueleza hali fulani, chanzo,muundo, utendaji na mwingiliano wa ndani na nje.

Wafula na Njogu (2007:7) wanasema nadharia ni jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.

Fasili hii imeegemea hasa katika nadharia ya uhakiki wa fasihi. Pia imetaja vitu muhimu kama vile, maelekezo ambayo ndiyo yanamuongoza msomaji au mhakiki ili asivuke mipaka ya mawazo ya hiyo nadharia aitumiayo ili kufanikisha kazi kwa ufasaha.

Kwa mujibu wa Sengo (2009:1) nadharia ni wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani.

Kwa mantiki hiyo nadharia ni dira au mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni.