Dhana ya utendaji katika nadharia ya Sarufi Zalishi

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Wednesday, October 24  2018 at  17:52

Kwa Muhtasari

Utendaji ni utumiaji wa lugha katika mazingira halisi ambao huweza kuathiri maana za maneno kulingana na matumizi yake au  mambo yanayomhusu mzungumzaji mwenyewe kama vile kutokuwa makini au kukosa kumbukumbu, kuongea akiwa amekasirika, kasoro za ala za sauti kama vile mapengo, kigugumizi na kadhalika.

 

Na MARY WANGARI

TUMEKUWA tukiangazia kuhusu dhana za kimsingi katika nadharua ya sarufi zalishi ya Kiswahili.

Katika makala iliyopita, tulichambua na kutathmini kwa kina kuhusu dhana ya umilisi katika sarufi ya Kiswahili.

Hii leo tutachambua kuhusu dhana nyingine muhimu katika sarufi zalishi inayofahamika kama utendaji.

 

Dhana ya Utendaji

Utendaji ni utumiaji wa lugha katika mazingira halisi ambao huweza kuathiri maana za maneno kulingana na matumizi yake au  mambo yanayomhusu mzungumzaji mwenyewe kama vile kutokuwa makini au kukosa kumbukumbu, kuongea akiwa amekasirika, kasoro za ala za sauti kama vile mapengo, kigugumizi na kadhalika.

Utendaji ni usemaji na utumizi wa ujuzi wa mzawa wa lugha katika kutumia lugha yake ndani ya muktadha mahususi, mtumiaji wa lugha huweza kuitumia lugha kulingana na mazingira aliyopo.

Kwa mujibu wa Yule (1997), matumizi ya lugha huzingatia muktadha, wahusika, jinsia, utamaduni na mada ya mazungumzo. 

Kwa mfano:

(i) Muktadha

Muktadha wa hotelini k.m., Nipe mbuzi chapati.

Muktadha wa kanisani k.m., Bwana awe nanyi.

 

(ii) Wahusika

Matumizi ya lugha huzingatia wahusika, kuna matumizi tofauti ya lugha kutegemeana na kundi la wahusika.

Kundi la rika moja hutumia lugha inayofanana mfano kundi la vijana hutumia misemo kama vile:-

 

Twende ngoma. (Maana ni twende densi)

Leo unaniachaje? (Unanipa nini cha maana leo?)

 

Kundi la watu wenye rika tofauti huwa na matumizi tofauti ya lugha.

Mfano;

Mzazi na mtoto

              Mzazi:  Mwanangu niletee kikoi changu.

              Mtoto: Sawa mama.

 

Mwajiri na mwajiriwa.

              Mwajiri    :  Leta faili la madai.

              Mwajiriwa:  Sawa mkuu.

 

(iii) Mada ya mazungumzo

Kuna aina tele za mada ya mazungumzo mathalan  mada za kijamii, kwa mfano ndoa, unyago, mapenzi, kifo, matanga, burudani na muziki  

Kuna mada za kibiashara kwa mfano bidhaa, kodi, vibali, fedha, hasara na faida.  Hivyo basi, ili mazungumzo yaweze kwenda vizuri, wazungumzaji wanatakiwa kuzingatia mada husika.

 

Kwa mfano: wafanyabiashara

Mzigo mpya umeingia.

Nauza kwa bei ya jumla.

 

Mada ya kilimo

Mbolea ya ruzuku bado haijaletwa.

Mwaka huu nitawahi kupalilia shamba.

Msimu wa mvua umewadia

Mwaka jana nilivuna kiasi kikubwa cha mahindi.

 

Wasiliana na Mwandishi kupitia baruapepe: marya.wangari@gmail.com