Dhana ya vimanilizi

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Friday, November 17  2017 at  06:30

Kwa Muhtasari

Searle (1969) anaeleza kuwa vimanilizi hutokea pale ambapo wasemaji humaanisha zaidi ya kile kinasemwa.

 

SEARLE (1969) anaeleza kuwa vimanilizi hutokea pale ambapo wasemaji humaanisha zaidi ya kile kinasemwa.

BROWN & YULE (1983) wanasema kuwa neno kimanilizi hutumika kuelezea kile ambacho msemaji huweza kudokeza au kumaanisha ambacho ni tofauti na kile kisemwacho moja kwa moja. 

THOMAS (1995) anafasili kimanilizi kuwa ni maana ambayo ni tofauti na pia ni ziada kwa maana isemwayo.

OGRAD na wenzake wanasema kimanilizi ni maana aipatayo msikilizaji kutokana na yale yaliyosemwa hata kama maana hiyo haikuelezwa bayana katika hayo yaliyosemwa.

Hivyo kulingana na fasili hizo zilizoorodheshwa tunaweza kusema kuwa;

Kimanilizi ni yale yasiyosemwa ambayo tunayajua kutokana na yaliyosemwa.

Kimanilizi ni kile kinachomaanishwa na msemaji ingawa hakikusemwa moja kwa moja.

1. Kwa mfano mazungumzo ya mzungumzaji A na mwenzake B 

A: Mzee yupo?

B: Gari lake halipo

B  amevunja kanuni ya ushirikiano kwa sababu alipaswa kujibu hayupo.

Hivyo kimanilizi hapa ni hayupo, maana angekuwepo gari lake lingekuwepo pia.

2. Niliposikia kwamba kuna mwanafunzi amejinyonga nilijua tu kwamba anatoka Nairobi.

Kimanilizi hapa ni kwamba watu wa Nairobi ni wepesi kujinyonga

Aina za Vimanilizi

Kuna vimanilizi vya aina mbili; kimanilizi cha kaida na kimanilizi cha mazungumzo.

1. Vimanilizi vya Mazungumzo (conversational implicate)

Ni vile ambavyo upatikanaji na uelewekaji wake hutegemea muktadha wa mazungumzo. 

Vimanilizi hivi ndivyo hasa vinavyosababishwa na ukiukwaji au uvunjaji wa kanuni ndogondogo za kanuni kuu ya ushirikiano. 

Vimanilizi vya mazungumzo huweza kutokea iwapo kanuni yoyote ndogo miongoni mwa kanuni ndogondogo miongoni mwa kanuni nne za kanuni kuu ya ushirikiano itavunjwa au itakiukwa.

Kwa mfano; 
A: Utakwenda kwenye shoo ya Diamond Jumapili usiku?

B: Nina mtihani wa fonolojia asubuhi

Kwa hivyo: jibu ambalo atalipata akilini mwake ndilo kimanilizi

 (yaani - sitaenda)

A: Dirisha hilo lililo wazi linapitisha baridi kali sana.

B hasemi chochote (anafunga dirisha) kwa hiyo:

kimanilizi hapa ni ombi ‘tafadhali naomba ufunge dirisha’

A: Kwani huyo ni mwanawe eeh!

B: Ni mzuri ninafurahishwa naye au Ni mbaya ninakerwa naye.

Tunaweza kuwa na vimalizi zaidi ya kimoja kutegemea muktadha.

a) Ina maana bumu la kwanza limeisha?

b) Unauliza makofi polisi?

c) Unashangaa vumbi stoo

d) Kwani papa ni mkatoliki?

Kwa hiyo: kimanilizi hapa ni ‘ndiyo’

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo

1.      Massamba P. B. D (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.

2.      Mdee, J. S (1997), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam: TUKI.

3.      Morris, Charles W. (1971), Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton