Dhana za msingi za nadharia Sarufi Zalishi

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Monday, October 22  2018 at  12:38

Kwa Muhtasari

Umilisi ni ujuzi alio nao mjua lugha kuhusu lugha yake.

 

Na MARY WANGARI

KATIKA makala iliyopita, tulianzisha uchambuzi wa mada kuhusu nadharia ya sarufi zalishi katika Kiswahili.

 

Hii leo, tutatathmini kwa kina kuhusu dhana za husika katika nadharia hii ikiwemo viambajengo muhimu.

Umilisi- Huu ni ujuzi alio nao mjua lugha kuhusu lugha yake. Ni ujuzi alio nao mjua lugha ambao upo katika ubongo wake.

Ujuzi huo huhusu kanuni zinazotawala lugha hiyo husika na humwezesha mtumiaji lugha kutambua sentensi sahihi, zisizo sahihi na kupambanua sentensi zenye utata.

Aidha, ujuzi huo humwezesha kupuuza makosa ya kiutendaji katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, na kukatiza sentensi.

Kwa mujibu wa Chomsky, mtu anapojifunza lugha huanzia na umilisi (ujuzi) na anaendelea kufafanua kuwa kwa kiasi kikubwa umilisi wanaokuwa nao wazawa wa lugha moja hufanana na hii ndiyo inayowafanya waelewane katika mazungumzo yao hivi kwamba mzungumzaji anasema kile anachotaka kusema na msikilizaji anaelewa kile kilichosemwa na msikilizaji. (Rubanza, 2003)

Umilisi humwezesha mzawa wa lugha:

1. Kuijua miundo ya sentensi katika lugha yake. Kwa mfano mmilisi wa lugha ya Kiswahili lazima ajue muundo wa sentensi za Kiswahili kuwa unaanza na nomino ikifuatiwa na kitenzi na kuishia na kitendwa.

Mfano: 

Baba anaongea na mjomba.                                                                                                     

Juma amekwenda sokoni.

Kwa hiyo mmlisi wa lugha hawezi kuchanganya muundo huu wa sentensi za Kiswahili kwa kusema;

            Mfano:   

Amekwenda   Juma   sokoni.                                                                                                   

Shambani  analima  baba.                  

Kwa hiyo, kulingana na muundo wa sentensi za Kiswahili, muundo wa sentensi zilizopo katika mfano wa pili si sahihi kwani zimekiuka sintaksia ya lugha Kiswahili.

2. Kutambua sentensi sahihi na ambazo si sahihi mfano:

         Maria ni msichana mcheshi (sahihi)

         Mtundu mtoto ni wako (si sahihi)

3. Kutunga sentensi nyingi zenye urefu wowote:

 

Msichana mpole na mrembo uliyekutana naye jana, nimekutana naye leo asubuhi amekamatwa na polisi kwa tuhuma za ujambazi.

 

4.Kutambua sentensi zenye utata, mfano;

              Mama Rehema amesafiri

              Nyumbani kwao kuna mbuzi

5.Kutambua sentensi zenye maana sawa.

Mfano;

Watoto wapo uwanjani wanacheza mpira.

Mpira unachezwa na watoto uwanjani  

6. Kutambua aina mbalimbali za sentensi katika lugha yake.

Mfano;

Leo ni sikukuu ya mashujaa (sentensi arifu).

Njoo hapa! (sentensi amrishi)

Umenunua kalamu ngapi? (sentensi ulizi)

Kumbe umerudi! (sentensi mshangao)

Miraj angelisoma kwa bidii angelifaulu. (sentensi shurutia).

Hivyo mmilisi wa lugha huweza kuelewa sentensi hizi zinataka nini.

 

7. Kutambua sentensi zenye maana na zile zisizo na maana.

Mfano;

Kitabu anasoma mwanafunzi (isiyo na maana).

Mwanafunzi anasoma kitabu (yenye maana)

Wasiliana na mwandishi kwa baruapepe iliyo hapa chini: