Mapenzi ya kileo

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Monday, December 18  2017 at  07:04

Kwa Muhtasari

Mapenzi ya kileo yamesawiriwa na wasanii wengi kuwa ya nipe nikupe.

 

MAPENZI hujitokeza katika kazi nyingi za kisanii kuwa jambo muhimu tena lenye mvuto na nguvu za kipekee.

Aghalabu wasanii wa kila nui huyaimba mapenzi, huyatungia mashairi, kuandika na hata kuchora michoro yenye kuvutia au kutoa hisia na jumbe za kimapenzi.

Mapenzi hata hivyo hubadilika na wakati kama yafanyavyo maisha ya watu na tabia zao. Kwa mfano leo fulani anampenda fulani. Kesho huyo fulani kaachana na fulani na anaingiliana na fualni.

Mapenzi ya kileo hata hivyo yamesawiriwa na wasanii wengi kuwa ya nipe nikupe.

Kwamba mapenzi ya kweli hayapo tena ila imebakia kuwa aina fulani ya biashara wafanyayo watu.

Inaonekana kuwa hawamjali mtu bali zaidi wanaijali pochi yake na ukubwa au uzito wa pochi hiyo.

Je, madai hayo ni ya kweli? Je ni kweli kuwa mwanamume na mwanamke wanaweza kuendeleza uhusiano wao wa kimapenzi bila kutarajia zawadi, malipo au faida fulani ya kifedha?

Ukweli mwingine ni kuwa mapenzi ya mijini hujitokeza kuwa na matarajio mengi ya kifedha kwa mfano, kunao mabinti wanaodai kuwa hawawezi kuwa na wapenzi wasiokuwa na magari wala kazi nzuri kwa kuwa hawataweza kuwashugulikia kifedha. Pengine hayo ndiyo mapenzi ya aina yao ila, je, hayo ni mapenzi ya kweli?

 Mapenzi ya kileo yanasawiriwa kuwa lazima yawe na faida fulani na iwapo mtu atampenda maskini basi yeye huonekana kuwa mjinga.

Hasa ikiwa yeye ni kidosho mrembo.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa mapenzi ni kipaji kisichoweza kuukwa na iwapo mtu atajaribu kuyauza, basi katu si mapenzi hayo bali ni biashara yenye kujaa hadaa.

Vijana wa kileo wafundishwe juu ya hatari za ubinafsi ili kuepusha vizazi na tamaa inayotishia maadili muhimu.

Phyllis Mwachilumo

Baruapepe: pmsambi@yahoo.com

Nambari ya Rununu: 0720218095