Tofauti kati ya matendo uneni dhahiri na matendo uneni yasiyo dhahiri

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  13:04

Kwa Muhtasari

Mwanafunzi anawaambia wenzake, "Mwalimu anakuja" badala ya kuwaambia waache kelele.

 

1. MATENDO UNENI DHAHIRI

MATENDO uneni dhahiri huonyesha kiwima kati ya aina ya sentensi na dhima ambayo inabeba. Mfano wa maelezo:

Kaka yangu ni dereva wa daladala.

Wakenya tumejifunza mengi kutokana na ushindi wa Uhuru Kenyatta.

Maelekezo

Mfano;

Weka dawa mahali pasipofikiwa na watoto

Marufuku kutupa takataka katika eneo hili

kimuundo si maelezo ila ni maelekezo yenye amri na ombi.

Maswali

Mfano;

Familia yenu ina watu wangapi?

Mbali na Wamasai ni watu gani wengine wanaojihusisha na ufugaji?

 

2. MATENDO UNENI YASIYO DHAHIRI

Haya ni matendo ambayo aina ya sentensi haiwiani bali inakinzana. Kwa mfano:-

Unaweza kumkopesha shilinga elfu kumi

Sentensi hii kimuundo ni swali lakini dhima ni ombi. Kwa hiyo inafanya tendo uneni lisilo dhahiri.

 

Njaa inaniuma sana

Kimuundo sentensi hii inatoa taarifa lakini dhima ni kuomba chakula. Kwa hiyo katika muundo huu ni kuwepo kwa muundo tofauti na dhima.

 

Aina za Matendo Uneni

Austin (1962) ametaja aina tatu za matendo uneni:-

1. Kile kisemwacho: Aina hii inahusu usemi wa sentensi yoyote yenye maana inayoeleweka pia iwe na kitu kinachorejelewa.

2. Lengo la kusema/kunena: Hii inahusu lengo la kile msemaji anachokisema au anachozungumza kuhusu. Lengo la kile msemaji anazungumzia kinatengeneza tendo uneni.

Kwa mfano mwanafunzi anawaambia wenzake, "Mwalimu anakuja." badala ya kuwaambia waache kelele.

Wanafunzi wanaosikia wito huu wanaweza kuitika tofauti tofauti. Wengine kwa kunyamaza, wengine kuzomea au wengine kuendelea kupiga kelele tu.

3. Matokeo ya kisemwacho: Inahusu athari/matokeo ya kile kisemwacho kwa msikilizaji. Matokeo ya kisemwacho kwa msikilizaji inaweza kuwa iliyokusudiwa au haikukusudiwa. Kwa ufupi aina hii inahusu majibu ya msikilizaji kimwili, kimaneno, kisaikolojia, kiakili na kadhalika.

 

Aina za Matendo Uneni Zilizoboreshwa

John Searle (1975) aliboresha aina za matendo uneni. Katika uboreshaji wake alisema kwamba kuna aina nyingi sana za matendo uneni na labda hazina ukomo.

Hii ni kwa sababu aina hizo hutegemea lengo, muktadha na lugha husika. Hivyo basi alipendekeza aina za ziada za matendo uneni. Alipendekeza baadhi ya aina za matendo uneni zilizoboreshwa.

Marejeo

1. Massamba P. B. D (2004), Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.

2. Mdee, J. S (1997), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam: TUKI.

3. Morris, Charles W. (1971), Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton

Wasiliana na mwandishi kupitia anwani:marya.wangari@gmail.com