Mbinu za lugha katika hadithi 'Tumbo Lisiloshiba'

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Thursday, May 24  2018 at  11:04

Kwa Muhtasari

Katika makala hii, tutaangazia mbinu za lugha zilizotumika katika hadithi ya 'Tumbo Lisiloshiba'.

 

Na WANDERI KAMAU akamau@ke.nationmedia.com

KATIKA makala hii, tutaangazia mbinu za lugha zilizotumika katika hadithi hii.

Baadhi ya mbinu za lugha/ uandishi zilizojitokeza hadithini ni: kisegerenyuma, jazanda, uhuishi, kuchanganya ndimi, maelezo ya moja kwa moja, dayolojia, uzungumzi nafsia na misemo.

KISEGERENYUMA/KUMBUKIZI

Hii ni mbinu ambayo mwandishi hurejelea matukio ya awali ili kuweka msingi katika kazi yake ya kifasihi.

Mbinu hii inajitokeza mwanzoni mwa hadithi ambapo Mzee Mago anavuta taswira na mawazo kuhusu uvumi ambao alikuwa ameusikia kwa muda mrefu, ila hakuwa amefahamu sababu yake halisi.

Hakuwa amebaini ikiwa mpango wa kubomoa vibanda vya Wanamadongoporomoka ulikuwa kweli au la (uk1).

Mbali na hayo, Mzee Mago anarejelea usahaulifu mkubwa wa binadamu ambao huwa nao, jambo analolinganisha na tatizo la ukosefu wa ukombozi kamili katika jamii nyingi duniani.

Aidha, anarejelea kwa undani kwamba mtaasisiko wa tamaa na utabaka katika jamii hizo kama kikwazo kikuu cha kujikomboa kwake dhidi ya mifumo kandamizi ya kiutawala.

“Kama si mambo mazito basi mabadiliko muhimu yangepiga kasi harakaharaka. Uzuri lakini sisi tumeumbwa na sahau…”(uk1).

Mwandishi pia anarejelea jinsi Mzee Mago huwa anawakusanya wenzake ili kuangazia uhalisi wa jamii wanamoishi chini ya utawala uliopo. Kumbukizi hii inaendelea hadi katika ukurasa 3 ambapo usimulizi halisi unaanza.

JAZANDA

Hii ni mbinu ambayo mwandishi hutumia mifano kitaswira ili kuwasilisha ujumbe fulani wenye maana ya kindani.

Uvumi anaorejelea Mzee Mago ni hofu ambayo wakazi wa Madongoporomoka walikuwa nayo kuhusu utawala uliokuwepo. Ni hali ya kawaida katika nchi zenye mifumo ya kidikteta.

Jitu linalofika katika mkahawa wa Mzee Mago na kubugia chakula cha watu wote linaashiria tamaa ambayo viongozi huwa nao kwa utajiri wa nchi kiasi cha kuwafilisisha wananchi.

Jazanda ya tumbo lake lisiloshiba linaashiria tamaa na umero wa mabwanyenye kutotosheka na mali ambayo tayari wamenyakua kutoka kwa raslimali za nchi.

Mkahawa mdogo wa Mzee Mago unatumika kama jazanda ya nchi dhalili ambayo uchumi wake unaotegemewa na watu wengi unavamiwa na mtu mmoja mwenye tamaa na kufilisishwa kabisa.

Ikumbukwe kwamba jitu hilo linakula chakula chote ambacho kilikuwa kimepikwa kwa minajili ya wateja ambao walikuwa wamefika.

Urejeleo wa hali duni ya mtaa wa Madongoporomoka, unaashiria hali ambazo wanaishi watu waliotengwa na tawala zilozopo katika nchi za Kiafrika. Katika urejeleo huo, tunaelezwa kwamba mazingira hayo “yananuka kutokana na maji taka” (uk4) ambayo hayakuwa yakizolewa na asasi husika.

Hilo linaashiria uduni wa mifumo ya kiutawala ya nchi za Kiafrika, kwani nyingi zinahimiliwa na mifumo ya kiutawala ya kibepari.

Vilio na malalamishi ya Wanamadongoporomoka dhidi ya kubomolewa kwa viwanda vyao ni jazanda ya ukandamizaji wa kisiasa, kijamii na kiuchumi ambao huendelezwa na viongozi dhalimu, kama Jitu hilo.

Gari aina ya Audi Q7 linaashiria vyombo vya kiutawala au mamlaka makubwa ambayo viongozi hao hujilimbikizia ili kubaki madarakani.

Dereva wake ni waajiriwa watumwa ambao wajibu wao huwa kuendesha mifumo hiyo ya kiutawala kwa maelekezi ya walafi hao.

DAYOLOJIA

Dayolojia ni mazungumzo ya zaidi ya mtu mmoja. Mazungumzo hadithini yanatokea katika kikao kati ya Mzee Mago na Wanamadongoporomoka wenzake, wanapojadilia uvumi kuhusu mpango wa kubomoa vibanda vyao.

“Hawawezi,” alitamka Kabwe (uk5). “Hawawezi, hawawezi, kabisa!” asema Kabwe, akisisitiza kwamba watatumia njia zote kuzuia ubomozi huo.

Mhusika mwingine kwenye mazungumzo hayo ni Bi Fambo.

Hapa, mwandishi analenga kuonyesha undani wa kauli ambazo wakazi walifanya kuzuia unyakuzi wa ardhi yao. Vile vile anaonyesha uchungu waliokuwa nao kuhusu mpango huo.

Mazungumzo mengine yanatokea kati ya Mzee Mago na jitu ambalo linafika katika hoteli yake na kubugia chakula chote ambacho alikuwa amewapikia wateja wake (uk8-9). Hili linalenga kuonyesha kiwango cha udhalimu unaoendeshwa na makabaila katika jamii hiyo.

KUCHANGANYA NDIMI

Mwandishi ametumia lugha ya Kiingereza katika hadithi hii kurejelea baadhi ya matukio.

Baadhi ya maneno ya Kiingereza yaliyotumiwa ni 'departmental stores’, 'mall’, 'Audi Q7’ na 'Coca Cola.’ Lengo kuu ni kuchora taswira ya mtaasisiko wa utabaka katika jamii rejelewa.