Tukiwathamini walimu, lengo la elimu bora litatimia

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Tuesday, October 16  2018 at  12:36

Kwa Muhtasari

Mpango kabambe wa kufuta ujinga, umaskini na maradhi katika Tanzania huru unalenga kuchochea kasi ya maendeleo.

 

HISTORIA inasema Serikali ya Tanzania iliwahi kuweka mikakati ya utekelezaji wa sera ya elimu kwa wote (UPE), iliyopitishwa mwaka 1974 na kuanza kutekelezwa mwaka 1977.

Lengo lilikuwa kuchochea kasi ya maendeleo kupitia mpango kabambe wa kufuta ujinga, umaskini na maradhi katika Tanzania huru.

Wakati huo walimu walipewa nafasi muhimu katika maendeleo ya Taifa na pia waliheshimika na kuthaminika katika jamii.

Hata hivyo, kutokana na matatizo mbalimbali ikiwamo kupuuzwa kwa walimu, miaka ya 1980 hadi 1990 tukaanza kushuhudia kuporomoka kwa ubora wa elimu kwa kasi kubwa.

Hali hii iliisukuma Serikali kuanzisha mpango wa kuinua sekta ya elimu kupitia sera ya kupunguza umaskini.

Ndipo ulipoanza utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MEM)) mwaka 2001 ambao nao haukuwakumbuka walimu

Walimu waliendelea kuishi na kufanya kazi katika mazingira magumu kama vile kukosa nyumba za kuishi, mishahara midogo na kutopewa stahili zao kama vile malipo ya uhamisho na likizo.

Hapa ndipo tulipofikia. Licha ya mchango mkubwa wanaotoa kwenye jamii, walimu bado wanachukuliwa kama watu wa kada ya chini isiyo na thamani ikilinganishwa na kada nyingine za utumishi wa umma.

Inashangaza kuona jamii ya sasa inamchukulia mwalimu kama mtu aliyeshindwa kufanya au kupata kazi nyingine na kukimbilia ualimu.

Inastaajabisha kuona wanajamii ambao watoto wao wanapata elimu kutoka kwa walimu haohao na baadaye wanakuwa wasomi wazuri na kupata kazi nzuri, ndio haohao wamekuwa wakiwadharau walimu na kuwaona ni kundi la watu walioshindwa maisha.

Matatizo haya yote yanawakumba walimu, lakini bado wanaendelea kuwajibika katika mazingira magumu ya kazi kama vile kufundisha wanafunzi wengi darasani.

Utafiti uliyofanywa na shirika la Twaweza kupitia jitihada yake ya Uwezo Tanzania mwaka 2015 na matokeo yake kuzinduliwa mwaka 2017, unaonyesha kuwa wastani wa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kitaifa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 44.

Wilaya yenye uwiano mzuri ina mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25 wakati wilaya yenye uwiano duni ina mwalimu mmoja kwa wanafunzi 75. Takwimu hizi ni kwa wilaya za Tanzania Bara.

Changamoto nyingine wanayokumba nayo walimu ni kufundisha watoto wenye njaa

Kwa mfano, takwimu za Uwezo zinaonyesha kuwa kwa wastani kitaifa ni shule mbili kati ya 10 (sawa na asilimia 24) ndizo zinazotoa chakula cha mchana kwa wanafunzi. Kwa maana hiyo, watoto wengi wanasoma wakiwa na njaa.

Hali hii ya kuhudhuria masomo wakiwa na njaa inawafanya watoto wengi kusoma katika mazingira magumu na kuathiri matokeo yao ya kujifunza.

Mwalimu kusukumiwa mzigo

Kibaya zaidi ni kuwa matokeo ya kujifunza yakiwa mabaya, mwalimu yuyo huyo ndiye anayesukumiwa mzigo wa lawama kwa madai ya kutotimiza majukumu yake ipasavyo.

Oktoba 5 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya walimu, ambapo lengo huwa ni kuthamini na kutambua mchango wao katika jamii na maendeleo.

Kimsingi, walimu ndio waliotufanya kama dunia kwa ujumla tufikie tulipo hivi sasa kwa maendeleo.

Katika siku hii muhimu, shughuli nyingi hufanywa na wadau mbalimbali wakilenga kukuza uelewa wa jamii ili iweze kutambua na kuthamini nafasi muhimu ya mwalimu katika jamii.

Siku ya Mwalimu duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1994 kwa jitihada iliyoanzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).

Tangu wakati huo, siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka na wadau katika sehemu mbalimbali duniani ambapo wengi wameitumia kukumbuka, kuthamini na kutambua mchango mkubwa wa walimu katika maendeleo ya Taifa.

Ijapokuwa tumeadhimisha siku hii wiki iliyopita, nitoe rai kwa Watanzania kwa kila mmoja popote alipo kuthamini mchango wa walimu.

Walimu wanapaswa kushukuriwa na kupongezwa. Watanzania hatuna budi kushirikiana kikamilifu na walimu katika masuala ya elimu mara kwa mara.

Ni kwa kufanya hivyo walimu watakuwa na motisha, ari ya kufundisha itapanda zaidi na watoto watapata elimu bora na dunia itaweza kufikia lengo namba nne la malengo endelevu ya dunia (SDG-4) ambalo linataka kila mtoto duniani apate elimu bora.

Mimi nawathamini na kuwapongeza walimu kwa kazi nzuri waliyofanya kwangu mpaka nimefika hapa. Wewe je?

Greyson Mgoi ni ofisa mawasiliano wa Uwezo iliyo chini ya Twaweza.