Ubaguzi

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Monday, April 23  2018 at  12:19

Kwa Muhtasari

Binadamu ni sharti afanye jitihada za kipekee kujifunza kuwa anaendeleza ubaguzi na jinsi ya kujizuia kuuendeleza.

 

Na PHYLLIS MWACHILUMO

UBAGUZI ni hali ya kutengwa kwa misingi mbalimbali. Watu hubaguliwa kijinsia, kiuchumi, kielimu, kikabila, kidini na hata kutokana na rangi zao tofauti.

Ubaguzi ni mojawapo ya maovu yanayoendelezwa na binadamu aidha kimaksudi au kwa kutojua kwao.

Ni lazima binadamu afanye jitihada za kipekee kujifunza kuwa anaendeleza ubaguzi na kujizuia kuuendeleza.

Ubaguzi wa kijinsia unaiumiza zaidi jamii kwa kuwa wanaume na wanawake wanalazimika kuingiliana katika hali zote za maisha.

Hawawezi kutengwa, na iwapo watatengwa basi hiyo tayari ni dhuluma kwa jamii yenyewe.

Ingawa hali ni hiyo, ubaguzi wa kijinsia huanzia kwenye familia ukaendelea shuleni, makazini na katika nyanja nyingi za maisha hata kwenye muktadha wa kidini.

Pale nyumbani, utammwona mtoto wa kike akifanyishwa kazi chungu nzima za nyumbani ilhali wa kiume anapumzika! Yule wa kike vilevile ataambiwa jinsi kuvaa, kuketi, kucheza na kadhalika. Hana uhuru wa kufanya atakavyo jinsi atakavyo.

Mazoea ya kuwapa watoto wa kike masharti haya ni ubaguzi dhidi yao. Haya huzoeleka na watoto wa kiume ikawa ndiyo kawaida na ubaguzi huu kuendelezwa hata zaidi!

Katika nyanda za usanii siku hizi,hususan uimbaji, mavazi ya wanawake waimbaji huonyesha ubaguzi mkubwa dhidi yao.

Je, ni lazima mwanamke avae nusu uchi ili muziki wake usikike? Ukiwalinganisha na waimbaji wa kiume ambao hujighubika mavazi mengi wasionyesha miili yao ila nyuso tu na wakati mwingine nyuso hizo huwa na kofia na miwani mikubwa mieusi! Inakuaje hivyo?

Katika hali za kikazi ni kuwa wanaume wengi ndiyo wenye kupata nafasi za juu; wanawake hufanikiwa kuwa makatibu tu. Mienendo hii katika jamii ilimuudhi Kazija (katika Utengano – Said A. Mohamed) na ni hali ambayo ilisababisha aamue kulipiza kisasi na kusababisha vurugu katika jamii nzima.

Hali ya ubaguzi inaporuhusiwa na kuendelezwa katiaka jamii yoyote, bila shaka jamii hiyo inakuza maradhi sugu. Ni vyema kwa jamii kutambua mambo haya mapema na kufanya jitihada za kipekee ili kubadilisha hali hiyo na kuwa na hakikisho la amani katika jamii pana.