Udhaifu wa mwalimu

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Monday, December 18  2017 at  06:44

Kwa Muhtasari

Katika hadithi fupi ya Mwalimu Mstaafu (Dumu Kayanda), mwalimu Mosi anasawiriwa kwa kiasi kikubwa kama mtu mkamilifu.

 

KATIKA hadithi fupi ya Mwalimu Mstaafu (Dumu Kayanda), mwalimu Mosi anasawiriwa kwa kiasi kikubwa kama mtu mkamilifu.

Hali hii inajitokeza pale wanafunzi wake wa zamani wanapotoa hotuba zenye kumlimbikizia sifa chungu nzima katika sherehe ya kumuaga anapostaafu.

Kwa kweli, jamii huwatarajia walimu wake kuwa watu wenye sifa zinazokaribiana na za miungu.

Yaani ukarimu, upole, ucheshi huruma na nyingine chungu nzima. Hata hivyo, mwalimu huyu anamsifu mwanafunzi wake mmoja wa zamani aitwaye Jairo kwa kumwambia ukweli wake bayana.

Huyu Jairo anamchukia mwalimu kwa kumpotezea wakati wake burekutokana na huo upole wake na matumaini ya uongo licha ya kuwa yeye Jairo hakuwa mwanafunzi mzuri. Kwamba alikuwa mbumbumbu, hakuelewa chochote darasani.

Mwalimu naye anamshukuru Jairo kwa kumwambia ukweli bila kumficha na kumwonyesha kuwa yeye ni mkamilifu kama miungu Artemis, Zeus na Osiris.

Mwandishi wa hadithi hapa huenda anadokeza kuwa, licha ya mchango mkubwa wa walimu katika kuhakikisha kuwa watoto wengi hawatoroki shule, waalimu hawachangii vilivyo kuwasaidia watoto wasiyoyaelewa masomo yanayofundishwa shule.

Hali hii inaweza kulinganishwa na daktari anayempa mgonjwa matumaini ya uongo ya kubakia tu huspitali licha ya kuwa ugonjwa auguao mgonjwa hautibiki. Hivyo huwa si haki kumweka mgonjwa huyo hospitali bure!

Hali ya mwalimu huenda inachangiwa na upungufu wa mfumo wa elimu na imani kuwa elimu ya shule ndio chanzo pekee cha maisha bora.

Ingawa mwalimu ana upungufu katika kali hio, anaonyekana pia kumfaidi sana mwanafunzi kwa kumweka shule na kumzuia kujiingiza katika maovu mbalimbali nje ya shule.

Maovu haya ni kama wizi, ulevi na unyang’anyi.

Mwalimu anampongeza mwanafunzi wake ambaye hakufanikiwa sana kimasomo na kudai kuwa huyo ndiye angefaa kuzungumza katika mazishi yake ili auseme ukweli kumhusu yeye wala asimpake mafuta kwa mgongo wa chupa kama wafanyavyo wengi mazishini mwa watu.

Phyllis Mwachilumo

Baruapepe: pmsambi@yahoo.com

Nambari ya Rununu: 0720218095