Umuhimu wa sare za shule

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Wednesday, October 3  2018 at  07:31

Kwa Muhtasari

Baadhi ya watu hujiuliza na hata kuulizana iwapo sare ndiyo isomayo au mwanafunzi.

 

Na PHYLLIS MWACHILUMO

JE, sare za shule zina umuhimu wowote? Pengine jibu la swali hilo linategemea mwenye kuulizwa. Kwa hakika majibu ni chungu nzima.

Kwanza tuanze na mvaa sare, yaani mwanafunzi. Bila shaka wengi wao hujiuliza na hata kuulizana iwapo sare ndiyo isomayo au yeye mwanafunzi! Wenine nao huuliza ni lini wata zivaa nguo zao za aina aina walizonunuliwa na wazazi wao. Maswali haya bila shaka huulizwa kwa bezo na kejeli ikielekezwa kwa wale wanaoshikilia kuwa sare ni muhimu.

Hata hivyo, bila shaka kunao wanafunzi wanaozienzi sare kwa kuwa hawana mavazi yoyote ya maana ya kujivunia huko makwao!

Wengine huziona sare kama njia ya kuzitambulisha shule zao ambazo wao huziona bora kuliko shule nyingine ‘mchwara’ wanazoenda vijana wenzao! Kwa kweli mitazamo ya wanafunzi juu ya sare zao ni mingi mno

Kwa walimu, mambo ni tofauti kabisa kwani sare ni chanzo cha kudhibiti nidhamu shuleni.

Nidhamu hudhibitiwa kwa njia mbalimbali kwa kutumia sare, moja ya hizo ni kuwa na sare ifaayo tena nadhifu. Zaidi ya hayo ni kuhakikisha kuwa sare haijabadilishwa na wanafunzi. Hayo yote huashiria nidhamu kwa kiasi fulani.

Pamoja ya hayo ni kuwa sare huwasaidia waalimu kuwatambua wanafunzi wao hata wanapokuwa mbali.

Mchezo wa paka na panya

Bila sare hizo, wanafunzi wangewapiga chenga walimu wao na kuishia kuwa mchezo wa paka na panya.

Hebu fikiria kunapokuwa na mkusanyiko mkubwa wa wanafunzi, je, mwalimu atawatambuaje wanafunzi wake iwapo watahudhuria  maonyesho ya kibiashara ya Nairobi au mengineyo?

Vilevile, kuwatambua wanafunzi wa shule yoyote ile hasa wanapofanya makosa hivyo basi hatua huweza kuchukuliwa haraka na wahusika.

Bila shaka sare zitasalia katika shule zetu kwa muda mrefu kwani pia ni ishara ya usawa unaoendelezwa na elimu yenyewe. Usawa huu lazima udumishwe.