Umuhimu wa shajara

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Friday, April 20  2018 at  11:39

Kwa Muhtasari

Shajara humwezesha mtu binafsi kupangia muda wake vilivyo na hata kumwezesha kutekeleza mengi zaidi kwa kupanga matumizi ya muda.

 

Na PHYLLIS MWACHILUMO  pmsambi@yahoo.com

SHAJARA ni maandishi yanayorekodi shughuli za mtu za siku, mawazo, matendo na hata hisia zake.

Bila shaka, iwapo ni shajara za kikazi, huandikwa shughuli zinazoambatana na kazi za ofisi hiyo tu. Bali zile za kibinafsi, huwa karibu zaidi na mwandishi wake kwa kuwa ndani yake huandikwa mambo ya kila aina.

Shajara za aina hii ni muhimu sana kwa mtu kwa kuwa humsaidia kupima matumizi yake ya muda alio nao.

Si vyema kutopangia wakati wetu vizuri.

Hivyo basi shajara humwezesha mtu binafsi kupangia muda wake vilivyo na hata kumwezesha kutekeleza mengi zaidi kwa kupanga matumizi ya muda. Wazungu husema kuwa ‘Wasaa ni fedha.’

Zaidi ya hayo ni kuwa shajara huwasaidia watu kuzielezea hisia zao.

Kwa wengine, shajara hizi ni kama rafiki wa siri anayeambiwa hisia za ndani zaidi kuhusu mambo mbalimbali.

Shajara hizi huishia kuwa kama mwenzi wa waja. Wengine wanapokumbwa na mambo magumu huzieleza shajara zao ugumu wa yale waliyokumbana nayo. Maandishi katika shajara za aina hii huweza kuanza hivi:

“Mpendwa Shajara, leo sina furaha! Kukutana kwangu na Neema kumenikumbusha mengi ya zamani. Machungu sana…. Tuyaache hayo! Nimeweza kufanya mengi leo. Siku imeisha vyema.”

Kutafakari

Shajara zetu bila shaka hutusaidia kutafakari kuhusu mengu katika maisha yetu.

Hutusaidia kujifikiria, kujipima na kujirudia katika maisha yetu ya kila siku. Vilevile tunakadiria jinsi tulivyoutumia muda wetu hivyo basi tunafanikiwa kujiuliza iwapo tunaweza kuboresha hali hiyo na vipi.

Kwa wale ambao shajara zao huwa ndio kama wandani wao wa siri, hulazimika kuzificha shajara hizi mbali sana na macho ya ulimwengu ili waepuke hukumu zao. Hata hivyo, shajara za kibinafsi kama hizo hatimaye huwa chanzo cha kuwaelewa watu ambao pengine katika uhai wao ilikuwa vigumu kuwaelewa au walieleweka kinyume.

Kunao watu mashuhuri ambao baada ya kufa kwao ndipo huwashangaza wengi kutokana na yale waliyoyarekodi katika shajara zao za kibinafsi! Tujiulize basi ikiwa yafaa tuwe na shajara za kibinafsi au la. Kwangu mimi bila shaka jibu ni “Ndio!’