Vimanilizi vya kaida

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Friday, November 17  2017 at  06:47

Kwa Muhtasari

Utokeaji wa vimanilizi vya kaida hautegemei muktadha wa mazungumzo.

 

KATIKA makala iliyotangulia, tuliangazia dhana ya vimanilizi na vimanilizi vya mazungumzo.

Leo tunatoa maelezo ya vimanilizi vya kaida. Hivi ni vimanilizi ambavyo utokeaji wake hautegemei muktadha wa mazungumzo.

Hii ina maana kuwa unaweza kupata kimanilizi cha kawaida kutokana na kauli fulani hata bila ya kujua muktadha ambao kauli hiyo ilitolewa.

Vimanilizi vya kaida havitegemei kanuni ya ushirikiano na hivyo havitokani na kuvunjwa au kukiuka kanuni ndogondogo za kanuni ya ushirikiano badala yake vimanilizi hivi hutegemea maana ya kipragmatiki inayopatikana moja kwa moja kutokana na maneno fulani yanayotumika.

Baadhi ya maneno muhimu yanayotumika katika vimanilizi kaida ni haya yafuatayo:- na, kwa hiyo, hata, kwa sababu, bado, lakini na kadhalika.

Mfano 1: Njoro ni Mkikuyu, kwa hiyo anajua kutafuta pesa. (Kimanilizi ni Wakikuyu  wanajua kutafuta pesa

Mfano 2: kijana yule ni mfupi hata hivyo siyo mbishi hata kidogo. (Kimanilizi ni wafupi ni wabishi)

Mfano 3: Haka kasichana wamekatoa kijijini ndio sababu kanachapa kazi kwelikweli (kimaninilizi ni wasichana wa kijijini wanafanya kazi kwa bidii (Ngeli ya Karanja)

 Mfano 4: Nakwambia katika Harusi ya Nuru hata George alikuwepo. (Kimanilizi ni George hakutarajiwa)

Mfano 5: Dereva bado hajafika? (Kimanilizi ni alitakiwa kuwa amefika)

Sababu za kukiuka kanuni za ushirikiano

1. Mgongani wa vikanuni

Hali hii hutokea pale ambapo mtu hujikuta amevunja kanuni nyingine. Katika jitihada zake za kutii kanuni fulani inasababisha kuvunja kanuni nyingine. Kwa mfano:-

A: Vipi huyo mchumba wake wa sasa ni maua sana.

B: Yaelekea anampenda.

Hapa mzungumzaji B anatii kanuni ya ukweli na kujikuta anavunja kanuni ya uhusiano

2. Kuonyesha upole au staha

Katika jamii za watu wa Ulaya, msichana anapokataa ombi la kutoka na mvulana kimapenzi huwa anajibu kwa upole kwamba "I will be washing my hair tonight" lakini pia jambo hili linajitokeza katika jamii zetu.

Mtu anakutafutia sababu kadhaa tu badala ya kukwambia kwamba hataki. Kwa hiyo kuna wakati mtu anaweza kuvunja kanuni fulani kwa lengo la kuonyesha staha fulani.

Mfano wa mazungumzo ya mwalimu na mwanafunzi.

Mwalimu: Umekuja darasani saa hizi?

Mwanafunzi: Samahani mwalimu kiatu changu kilikatika ghafla njiani nikalazimika kupitia kwa fundi kukishona ndio maana nimechelewa.

Hivyo heshima hiyo imesababisha yeye kuzungumza hivyo na kupelekea kukiuka kanuni ya kiasi.

3. Kuonyesha ukali au hasira/ kukosa staha

Kwa mfano:

A: Mbwa wako anang‘ata?

B: Hang‘ati.

A: (anamchezea huyo mbwa na anang’atwa ) Alaa! Si ulisema mbwa wako hang‘ati!

B: Hang‘ati ila huyu si mbwa wangu.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo

1.      Massamba P. B. D (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.

2.      Mdee, J. S (1997), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam: TUKI.

3.      Morris, Charles W. (1971), Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton