Shangaa: Uchumi wazorotea walimu baada ya mgomo

Imepakiwa Saturday September 22 2012 | Na Mathias Momanyi

Kwa Muhtasari:

Walimu wa Shangaa waliufakamia mgomo wakayasusia masomo wakasusia vipindi madarasani na sasa ngoma i karibu kuwapasukia viwambo.

CHURA na samaki hupenda maji lakini si majimoto wasomaji wangu. Madaftari ya wanafunzi yamejaa mavumbi nyumbani. Huenda shule ya Shangaa ikaitwa ganjo au mahame yaani makao yaliyohamwa...Walimu wa Shangaa waliufakamia mgomo wakayasusia masomo wakasusia vipindi madarasani na sasa ngoma i karibu kuwapasukia viwambo... Nyasi zimemea zikameana shuleni kwani hapajafyekwa.

Hata wafanyakazi wa muda wamezidiwa na msimamo huu ngangari wa walimu. Mabawabu wa shule wamechoka kubeba vijirungu huku jua likipausha ngozi na vipara vyao. Serikali inavyozidi kusita kuitikia wito wa walimu ndivyo uchu unavyozidi kuwaingia wasomi hawa! Walimu wengine wangali wanauguza makali ya viboko na fimbo za askari makalioni, baada ya mshikemshike wa kuandamana barabarani wiki mbili mtawalia. Sasa mavazi yameanza kumpwaya Katululu mzee wa hekima na zee la walimu. Suruali yamwanguka maskini mume wa watu hadharani! Havalii bila mkanda. Kakondeana huku mawazo na fikra zikimsonga si nyumbani kwake si katika maeneo ya mvinyo... Kitambi chake kimeyoyomea hadi kwenye mbavu...Posho kapungua maghalani hata baada ya 'tusheni' kugonga majabali.

Anadaiwa kope si zake kwa sababu ya 'waziri wa elimu.' Madeni ya nyanya na mboga magengeni ni makubwa ajabu! Hajalipia bidhaa kadha wa kadha. Wauzaji hawapati chembe za sarafu kwa sababu walimu, madaktari na wahadhiri hawajatimiziwa ahadi zao. Kumbe hela ni tamu mjomba? Hujaziona, hujalalama. Usiambe kabla ya kuona heri uone ndipo uambe.

Kosa fedha mfukoni wiki moja useme, wallahi utanuka na kuchekwa mithili ya kinyago na jamaa wakiwemo marafiki wako wa dhati! "Daddy, mgomo huu utaisha lini? Kwani siku hizi hatuli nyama...?" Haya ndiyo maswali ya watoto wake Katululu. Maswali yanayomwandama kila jioni ya kula sukumawiki badala ya maini kilo saba waliyoyazoea kila baada ya siku mbili nyumbani pamoja na samaki wa kupaka. "

Mume wangu, sasa tutalala njaa kwa sababu ya mgomo tu? Si ajabu nitaiona nyumba hii ikiingia wazimu... Saluni sijaenda, jikoni kiporo kimetuchosha... Naona nikigura nyumba hii nirudi kwa wazazi wangu..." Mkewe Katululu amemjaza mume wake ghadhabu nusra juzi wamchinje nyau ukipenda paka...Aisee! Hiyo ndiyo balaa ya mwalimu kumwoa mwanamke asiye na ajira, kazi wala bazi!

Mitihani

Mbona hatushirikiani jamani? Ajira si ya mume au mke pekee. Tukiachana na hilo la kugomea posho, imesalia wiki moja mitihani ya Kifaransa na masomo mengine yang'oe nanga nchini kwenye mtihani wa KCSE. Tazama kwenye kalenda KCPE i mlangoni... Bado madarasa wala vidato havijakanyagwa na baadhi ya wanafunzi. Mabweni yamefungwa ndi! Yangali machafu na kakolea utandabui si haba!

Wanafunzi wamegeuka kuwa mizigo mizito vyumbani. Waliozoea kuelekea katika shule za mabweni nchini nao wameharibu bajeti za familia zao. Watoto wengine wamezaliwa kisungura si kumi si wanane si saba! Wanakula kama nzige matawini. Watoto hula kwa pupa kama majuju au majini ashakum si matusi. Wanakula bila kusaza matonge mezani... Lo! Wazazi wanalia midomo juu kama mbwakoko.

Wazazi wameomba makanisani na swala zikiijaza misikiti lakini wapi! Wimbo mui utaongolewa wana sasa...Hasara imeuzidi uchumi katika sekta ya elimu. Wanajutia sana kulipa karo za mwaka mzima, wasingejua kwamba bahari ingewaka moto baina ya walimu na serikali. Mashauriano haya yamebaki mchezo wa paka na panya uwanjani 'Sokomoko.' Wanafunzi wamegeuka sombombi wasio na adabu wala mipaka majumbani.

Nashuku wamevikosa viboko vya walimu wao... Si wajua tena teke la kuku halimwumizi mwanawe? Wanaiba vyakula na vifaa kadhaa nyumbani huku wazazi wakiendelea kugharamia hasara wanazosisababisha nyumbani. Enhe! Kumbe mtoto si wa wazazi ni wa jamii na nchi japo nchi hii haina huruma yoyote kwa wanawe hususan wanafunzi.

Eti serikali inadai mtoto ana haki ya kupata masomo ilhali imemtenga na kumtelekeza mtoto wa bara jeusi Afrika! Je, huu ni uungwana kweli? Rafiki yangu Mambo Mbotela atauliza pia huu ni uungwana kweli? Tafadhali viongozi nawaomba mwaondolee wazazi zigo hili.

Litakuwa jambo la busara kuwekezea elimu badala ya kuwazamisha wanafunzi na kuifisha kesho yao. Kumbuka asili ya ujambazi, wizi, ufisadi, maradhi na umaskini ni kutokana na uhaba wa kisomo stahiki kwa mwananchi. Wangapi wanajivunia kuwa wakenya nchini?

Share Bookmark Print

Rating