Nyani alivyotimka na karatasi za mtihani wa KCSE

Na Mathias Momanyi

Imepakiwa - Saturday, November 3  2012 at  11:11

Kwa Muhtasari

Nasikitika kusema kuwa walimu walifurahia sana kupata mwanya huu wa kuwaruhusu wanafunzi kusomea mtihani badala ya kujiandaa kufanya mtihani. Do! Haki iko wapi? Tumlaumu nani katika mkasa huu? Naomba majibu na jumbe zenu tafadhali...

 

DUNIA haiishi vituko wala vihendo mwanakwetu... Aghalabu Kenya huwa nchi ya kujionea kila sampuli ya sarakasi, vituko na vimbwanga. Hili ndilo taifa ambalo mafahali huchuana kule Ikolomani au Shinyalu huku watazamaji wakienda kushuhudia bwerere bila kulipa kiingilio chochote kule magharibi ya Kenya.

Je, fahali mmoja au wote wakifa, nani hulipa fidia? Sijasikia. Enhe! Wakenya hupenda sinema za bure wakasahau kwamba bure ni ghali...Hayo ni ya ngoswe tumwachie ngoswe mwenyewe chambilecho watanganyika na hujafa hujaumbika, utakesha kucheka hadi mbavu zitunge majipu na vidonda vya ndani kwa ndani kifuani.

Mapema mwaka huu jamii kubwa ya manyani iliivamia shule ya Shangaa kwa sababu ya amani na utulivu wa mazingira hayo wakiwemo wanafunzi wanaowaburudisha kwa vicheko na michezo ya kibe na gungwi. Mara ya kwanza nilipotambiwa kisa cha nyani kuingia sokoni kununua vyakula kama mtu mzima sikuamini hadi nilipojionea kwa macho yangu mawili sokoni.

Niliamini simulizi zake Jilani Wa Mbura. Wanafunzi wa Shangaa hula nao na hucheza nao bali hawajui nyani haoni soni. Usisahau kuwa mzaha mzaha hutunga usaha...Inafaa ufahamu kuwa nyani huona raha akimdhulumu mwanafunzi au mtoto. Hujidai kuigiza alifanyalo mwanadamu japo akili zake si razini wala tambuzi na kamilifu kuafiki nia za mtu mkamilifu!

Huketi kwa mapozi na tabasamu za kuajabia na kucheka kama mzee Suleimani mwenye meno ya ugolo. Hulala kifudifudi na chali kama babu yangu akiwa na kichokoo au kichokonoo mdomoni sijui, kala nyama katika mkahawa gani? Anaweza kujipaka mafuta, hina pamoja na kidomwa mdomoni. Mambo yake ukweli! Huaibisha wakati mwingine ulingoni kwa matendo yake hafifu ya kuwafurahisha watalii... Humkosi maktabani! Husoma magazeti na kubukua hisabati bila kupata majibu mjomba. Hazungumzi ila hujikunakuna sana tena zaidi.

Ipo siku ataibua viroboto wenye maradhi shuleni... Tutaona nani tabibu wa kweli kuyadhibiti maradhi yake! Starehe zake sambamba na sokwemtu... Baada ya mzaha wote wa wanafunzi kumwamkia na kumpokelea kwenye chumba cha mtihani, nyani yule alikaidi vitisho na kufukuzwa, aliingia kwa mbwembwe, mwendo wa dalji na madahiro akiiandama ndizi ya mkaguzi.

Kukurukakara

Mkaguzi mkuu Bi Sandona alimwogopa na kutoroka na ndizi yake akiiacha mitihani dawatini! Chambilecho Waswahili, ukikosa la mama hata la mbwa huamwa. Nyani alionesha jinsi kisasi hulipizwa hadharani. Mkaguzi maskini bibiye mtu aliondoka kwa lazima kuenda kumwita askarikanzu akiwaacha wanafunzi wakiiba mtihani. Eti! Wanamtumia nyani kuwa kigezo cha kuviziavizia mwakenya!

Ujanja wa nyani na wanafunzi, utaishia jangwani... Wacha watahini wakalie majibu yenu, mtashangaa watakavyougundua ujanja mdogo wa kuiba na kunakili kivoloya maswali... Basi,  nyani huyoo alijiendea zake, kwapani kabeba burungutu na mabunda kadhaa ya karatasi za mtihani wa kitaifa KCSE.

Kachupachupa hadi mti wa pili huku mlinzi akimfuata unyounyo. Kukurukakara za askari na nyani siliwachekesha wanafunzi na wafanyakazi wote walioshuhudia mkasa wa mchana mwangavu. Wanafunzi nao waliutumia wakati ule kutalii katika mabuku kuisaka siri ya baraza la mitihani bila hofu ya adhabu za baraza. Askari aliiparaga miti akapanda akishuka.

Mwanamume wa wenyewe eti! Utumishi kwa wote hadi mitini? Siamini usemi wa mbio za sakafuni huishia ukingoni laiti wangalisema mbio za nyani na mtu huishia porini. Askari alijikwaa akaviangukia visiki akaumia vibaya zaidi.

Mtume! Kumbe  hiyo ilikuwa raha ya wanafunzi? Najuta kuamini usemi wa mwenye kisu mkononi ndiye mchinja sarara ya shahamu... Nakumbuka namna rafiki yangu Antony Omuya ambaye pia ni paparazi mstahiki chumbani Taifa Leo alivyong'ang'ania picha za kunasa. Aliupata wakati mgumu kusogeza matawi kunasa sura ya mlinzi na nyani.

Iwapo huamini, tazama Shangaa kwenye 'facebook' hujionee jinsi ulimwengu una raha na sinema tamu kuliko za wazungu. Hii ilitukia baada ya wanafunzi kupokea kisabechana chao wiki hii kule tarafa ya Manga. Nyani alizua tabu iwapo si tandabelua moja juu ya nyingine. Mara kazirarua karatasi mbili kisha akaonyesha machachari yake ya kukibeba kitopa kizima bila huruma hata chembe!

Asilimia hamsini ya wanafunzi ililazimika kusubiri hadi pale nyani atakapoamua kuwateremshia karatasi kutoka kilelechani. Kumbe bunduki zile za askari si zote huwa na risasi? Mbona asingemfyatulia hayawani yule kwa minajili ya kuwaokoa wanafunzi waliotaabikia katika utandabui wa nyani na mitihani? Aidha sheria  ya kuwalinda wanyamapori isingemruhusu kuyatekeleza mauaji ya aina yoyote! Enhe! Mjomba ungefanya nini iwapo ungekuwa askari au mwalimumkuu wa Shangaa baada ya trivyogo hii.

Najua utajidai kuyaleta maarifa yako na ujanja kama wake nyani lakini wapi? Utaishia kunawa, kurudi ukala mabaki badala ya kima mjomba.

Hivyo ndivyo visa vya kushangaza wanakwetu wacha vituko vya uswahilini vya Shangazi kufunga ndoa na mpwa wake! Sijakuhadaa msomaji wangu hadi pale utakaposafiri nami katika safu hii uwajue wanadamu, uwafahamu wanyama na kila aina ya kiumbe kinachoshangaza kule Shangaa. Samahani narudi kwenye kisa.

Askari

Kutokana na ghadhabu za nyani yule, aliamua kuziacha karatasi katika mabati ya ghorofa nambari kumi na saba. Huduma za kila aina zilitafutwa kwa dharura kuzichukua karatasi zile. Mwelekeo wa askari na ukaguzi wake uliyumbayumba ajabu! Sijui kamkagua nyani au kawakagua wanafunzi? Uhuru wa wanafunzi ulishamiri madarasani huku wizi wa mtihani ukishukiwa katika baadhi ya madarasa.

Nasikitika kusema kuwa walimu walifurahia sana kupata mwanya huu wa kuwaruhusu wanafunzi kusomea mtihani badala ya kujiandaa kufanya mtihani. Do! Haki iko wapi? Tumlaumu nani katika mkasa huu? Naomba majibu na jumbe zenu tafadhali... Eti! Siku ya kufa kwa nyani miti yote huteleza... Nyani haoni kundule au ghubaye... Nyani haoni ngokoye...Zitaje methali zote za nyani unazozijua.

Umewahi kuacha kazi zako kwa mfano stakabadhi, hundi au barua ofisini-mezani ukazipata hazimo, aidha zimefichwa au akazipoteza mwafulani? Wengine huingia katika tarakilishi na mitambo yako wakasambaratisha na kupoteza data zako? Je, huyo ni nyani au ni kama nyani? Kati ya nyani na yeye ipo tofauti gani? Funzo. Tudumishe maadili. Tusiwe kama nyani au popo si ndege si mnyama...

mathimomanyi@yahoo.com