Maombi ya watahiniwa siku hizi yamejaa vituko

Na Mathias Momanyi

Imepakiwa - Friday, November 30  2012 at  14:50

Kwa Muhtasari

Watoto wa siku hizi labda hawahudhurii madrasa, semina za maadili wala vikao vya mashababi vya Jumamosi na Jumapili. Wazazi mko wapi?

 

ASHTAKIAYE Mungu, kawesha mahakimu, haogopi silaha wala vitisho vya mahasimu... Jina hili lina sifa - MUNGU... Jina hili halifanyiwi mzaha wala dhihaka kwenye mitaa na makanisani - MUNGU... Waulize walokole nikiwa mmoja wao mjomba.

Salaam aleikum wazalendo wetu? Kila kiumbe ulimwenguni, kina imani yake lakini imani isiyodhibitiwa sawasawa huwa potovu. Nimeyaona maombi yakifanyika Shangaa wakati wa kufanya mitihani pekee. Shuleni mle, wanafunzi hawaruhusiwi kuimba nyakati za kawaida gwarideni.

Iwapo mtaimba hamtaruhusiwa katu kupiga makofi... Sielewi dhehebu dhamini wala imani ya shule ile. Maombi ya kuwaandaa wanafunzi katika mtihani wa KCPE yalifanyika Jumapili shuleni Shangaa huku imani za kila muumini shuleni mle zikitiliwa shaka. Wanafunzi wengi Shangaa aghalabu hutoka katika jamaa za kila nui.

Kuna makabwela ambao hawajawahi kulalia mikeka wala ngozi za ng'ombe kama mie na wewe na kuna wachochole wanaobahatisha maisha ilimradi wapate senti za kuganga njaa. Nasikitika kusema kuwa, si wanafunzi wote waliomo Shangaa wana nia njema ya ufanisi wao.

Kasisi Mlienda Mkalala aliwaombea wanafunzi huku ubishi ukizuka kutoka kwa wasimamizi wa makanisa mbalimbali yakiwemo mahekalu na misikiti. Uteuzi wake wa kuwaombea wanafunzi ulizua mjadala katika eneo takatifu! Fauka ya hayo, wengine walikaidi amri za kasisi kufumba macho wakidai imani yao haiwaruhusu kutenda hilo na wengine kavalia vilemba si bulibuli si chepeo hata hirizi... "

Wanafunzi wapendwa, naomba muwe watulivu tufumbe macho tuombe... Wale mnaozungumza tafadhali tunyamaze... Kwa jina la baba..." Wapi? Wanafunzi walimfokea mteule wa Mungu. Heshima maabadani ikaadimika kama maziwa ya kuku...Kasisi alibaki kujiombea mwenyewe pamoja na wachache waliomtii... Audhubillahi! Mungu si Athumani wala mzee Mkumba msomaji wangu!

Sijui makanisani kulikoni...Watoto wa siku hizi labda hawahudhurii madrasa, semina za maadili wala vikao vya mashababi vya Jumamosi na Jumapili. Wazazi mko wapi? Mmelala m macho au m macho ilhali mmelala kisungura? Wangeombewaje wapite katika mtihani wao ujao ilhali wanazisaka laana za mbingu badala ya baraka za mitume?

Kuna wale wangali wanaabudu miungu badala ya Mkawini mbingu. Maombi hayo yaliyosindikizwa kwa burudani za kukata shoka kwa miziki ya ''Reggae na ile ya kufokafoka'' si michezo ya kuigiza na hamrere za kila aina, yote hayo yalituacha na wanahabari wenzangu tukishangaa namna kanisa linavyogeuzwa uwanja wa biashara na fujo... Mwalimu mkuu Fisidume hakujua pa kuanzia wala pa kumalizia.

Aliwalimbikizia wazazi wengi lawama kwa kutowapa wanao mielekeo. Hii ilizuka tu baada ya mwanafunzi mmoja kumrushia kasisi chupa ya maji kwa kishindo mimbarini. Enhe! Wanafunzi wa siku hizi wanaolelewa na katiba mpya badala ya katiba kubadili vifungu kuwalea wana kwa mielekeo stahiki!

Ungalikuwa pale ungalifanya nini msomaji wangu? Sheria inampa mwanafunzi uhuru wa kujitendea bila adhabu wala makanyo ya kiboko. Hamjui kuwa huenda mkuki kwa nguruwe ukawa mchungu na kwa mwanadamu mtamu?
Kasisi Mlienda Mkalala aliumeza mrututu.

Aliunyosha mkono wake imara kama suezi kuwapa baraka wachache ambao walionyesha subira, utulivu na nidhamu. Kweli, kila soko lina wendawazimu wake... Hakika, baadhi ya watahiniwa wa mwaka huu K.C.P.E walikuwa walevi chakari!

Pahala patakatifu

Aliyewapa mvinyo asubuhi ile ya sala za kuwatakia heri simjui. Wavulana walinyoa denge na wengine vishoroba. Walisahau kuwa pahali patakatifu si jukwaa au medani ya mbwembwe kamwe! Walikinai kila babu au sura iliyosomwa mimbarini. Wengine walicheka ovyoovyo kwa kelele za chiriku aliyemeza maji ya choo ashakum si matusi...
Mtume asimame! Hawa ndio wanafunzi wa miaka ya sasa tunaowasubiri kuurithi ufalme wa nchi na ule wa mbingu? Eti! Viongozi wa kesho gani? Wacha hadithi za pangu pakavu tia mchuzi... Nikirejea shuleni, walimu wote wa darasa la nane walilazimika kuibeba mikongojo kwa minajili ya kuzituliza kelele za wasumbufu wao.

Vurumai hiyo ilinikumbusha operesheni ya kuwasaka sombombi wale wa Bondeni Suguta - Baragoi. Yaani nyakati za dunia kupasuka na ardhi kutuzika chambilecho marehemu P.P Mwai Wa Githinji ndizo hizi. Huu ni wakati wanafunzi katika viwango vyote wanafaa kuuona umuhimu wa mitihani na mistakabali yao.

Mzaha mzaha hutunga usaha kwenye jeraha bila kupojaa. Wape walimu uhuru wao. Elimisheni watoto kuhusu umuhimu wa dini. Dini si jini. Hamna haja ya kuwafunga mbwa minyororo ilhali wezi wamo nyumbani... Enzi za wanafunzi kuwa walimu na walimu kuwa wanafunzi zaja.

Natabiri hili bali sichochei. Nawajua nyie mnaosoma fasihi kutoka nyuma kwenda mbele badala ya kuufuata urari wa matukio chasili. Naomba tusingoje dawa za babu Masapile kutoka Loliondo jamani! Hatua za mabadiliko zinafaa kuanza na sisi la sivyo, shule zetu zitayakosa matokeo mazuri kila mwaka kwa visingizio bwete, tukabaki kuwalaumu walimu tukisahau kuwa ajuaye misonoe ni yule alalaye naye. Tuishi kama zamani...
mzeemzim@gmail.com