Miili minene ya wanafunzi balaa darasani

Na Mathias Momanyi

Imepakiwa - Monday, January 14  2013 at  14:05

Kwa Muhtasari

Wanafunzi sasa wameripoti Shangaa wakiwa wanene ajabu! Wengi wana vinena na mashavu yaliyoshobwekea ndani. Mashavu yana vidu, mabega kama mfumbati. Wanafunzi wanene hupata taabu sana kuelewa madarasani. Huu si utani wala mzaha mzalendo wangu.

 

ALIYE na hamu ya kupanda juu hukesha. Maana ya tamathali hii ya lugha ni kuwa; yeyote mwenye nia ya kujiendeleza hulazimika kukesha akifanya kazi kwa bidii ya nyuki mtengeneza asali.

Methali hii hutufunza kwamba iwapo tunataka kufanikiwa maishani, lazima kama ibada tuwe tayari kufanya kazi kwa juhudi za kujituma.

Wanafunzi sasa wameripoti Shangaa wakiwa wanene ajabu! Wengi wana vinena na mashavu yaliyoshobwekea ndani. Mashavu yana vidu, mabega kama mfumbati. Matumbo makubwa makubwa na nyama za visogoni zinawataabisha kwelikweli. Kutembea sasa ni tabu. Mwili wa mwanafunzi unayameza mavazi kotekote.

Baadhi yao hutokwa jasho sana darasani mwalimu anapofundisha. Jasho la uji wa mtama wanaopikiwa kila asubuhi kwa mkate wa kusukuma. Wengine huja na mahamri motomoto zikiwemo kaimati za sukari ndani pamoja na vitumbua sandukuni.

Kuna wale ambao hunywa sharubati, hula viazi, njugu, kaukau, kumumunya pipi na kutafuna bazoka walimu wakifundisha. Hawajali hawabali. Sasa kibarua cha kunenepa kimeshika kasi mjomba! Mwili unaishinda miaka. Badala ya kusoma, wanafunzi huzingirwa na gonezi yaani usingizi wa pono huku ute ukiwatoka vinywani taratibu! Wamerejea kwa vishindo vya papa anayeangusha meli baharini. Hawana budi kufanya mazoezi shuleni, kukimbia na kuipasha misuli motomoto angalau waupunguze ufuta na vitambi madarasani.

Naomba utembee, uabiri pikipiki ukazuru Shangaa. Iwapo hujui kule, nipigie simu nikupe mwongozo na dira kamili ya kufika shuleni. Hiyo ndiyo shule yenye maajabu katika shule zote za kibinafsi mijini hususan matawi ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nakuru. Haikosi kuajabisha!

Wanafunzi wanene hupata taabu sana kuelewa madarasani. Huu si utani wala mzaha mzalendo wangu. Asilimia kubwa ulimwenguni ya watu wanene huwa mazumbukuku na wazungu wa reli. Si unawajua masumo kule Uchina? Kupata mambo yoyote yale, kunafaa mtu awe chapuchapu! Mavazi huwaruka. Huwezi kuvalia viatu vyao! Mavazi yao yatakuvaa au kukupwayapwaya.

Jana tuliingia uwanjani Shangaa tukanasa picha za watoto hao wanaotoka katika familia za vizito. Pindi tu mvua iliponyesha, mbio za wanafunzi ziligeuka sinema ya kuangaziwa. Vitambi viliitangulia miguu nayo mikono mifupi ikatawaliwa na mwili mzima. Nilicheka hadi mbavu zikasogea kushoto kulia.

Mvinyo

Aisee mjomba! Kati ya kunenepa na kukondeana utachagua nini? Natumai mwili wastani humfaa mwanadamu kulihali. Nendeni katika mashindano ya kumteua mwanajeshi, askari au mwanariadha bora nchini unijuvye siri ya mwili ni ipi na kina nani huteuliwa washindi? Fauka ya hayo, tazameni Tae-kuon-do au Karate runingani unipashe mjomba!

Sisemi kuwa kuzaliwa mnene ni laana. Katu! Japo ni matatizo, baadhi ya wanafunzi hao wameirithi mili ya wazazi wao. Mzazi kanywa mvinyo klabuni. Kalala funguo za gari lake kazilaza tumboni. Tai hafungi mzee wa watu. Taibu, mtoto wa nyoka ni nyoka.

Wacha hayo yakome turejee Shangaa.

Sasa walimu wote shuleni, wameweka mikakati ya kuipunguza mili ya wanafunzi hao waliotoka nyumbani baada ya kubugia mahanjumati katika sherehe za Krismasi na mwaka mpya.

Patakuwepo na kazi kadha wa kadha za ziada, kuruka maji na viunzi na kuzunguka mduara uwanja mzima mara tano kabla ya kuingia katika kipindi cha Kiswahili cha mwalimu Katululu - gunge mswahili. Maswali ya chemsha bongo yataulizwa papo kwa papo kwa mpigo huku walimu wakihakikisha kuwa walalao darasani huandika insha mbili kwa siku. Enhe! Shauri lako wewe unayekubali nikuchochee.

Mwili wa mwanafunzi huandamanaje na ubongo au kazi hizi? Kuweni waangalifu msije mkayahatarisha masomo ya wanafunzi wetu na kuwasababisha kuchukia shule. Baadhi yenu msije kushtakiwa kwa kutekeleza adhabu za kinyama kwa wanetu. Do! Mwili kuupunguza, yataka mabadiliko ya lishe na mitazamo. Kazi za ziada si chochote mwanakwetu!

Wape ushauri wapunguze mili kwa njia stahiki! Washughulishe katika kazi zinazofaa. Jamani unaukubali uzani wa mwili wako? Uamuzi ni wako mwenzangu. Kila nyani ana starehe zake, zangu zinakuhusu ndewe ama sikio?

mzeemzim@gmail.com