Hasara ya uteuzi wa vyama kuandaliwa Shangaa

Imepakiwa Thursday January 24 2013 | Na Mathias Momanyi

Kwa Muhtasari:

Shuleni Shangaa ambapo uteuzi wa vyama vya kisiasa uliandaliwa, madawati ya wanafunzi yamevunjwavunjwa. Viti vilikaliwa ndivyo sivyo, Kamusi kadha wa kadha zimeibwa. Ubaoni pameandikwa jumbe za kuwachochea wengine mbali na madaftari ya wanafunzi wengi kupotea.

HALAHALA mtu na mji wake, ukichelewa utapata mwana si wako... Huu ni usemi wa Washirazi umaanishao kwamba usiwahi kuchelewa kwa kila ulitendalo, wenzako watakupiku! Hima ujihadhari na haraka mbovu isiyo na baraka. Tazama kura zilivyokuwa. Uteuzi uliochelewa ulikumbwa na mititigo fulani.

Mnamo Alhamisi na ijumaa wiki iliyopita wawaniaji kadhaa walitundika guu begani kujiwakilisha katika maeneotawala yao angalau wateuliwe wakitarajia kuchaguliwa mwaka huu.

Maombi yalifanyika makanisani kwa mara ya kwanza. Waganga wakapata kibarua cha mwaka kuvuna kwa uongo na hadaa za kusubiri taure! Kunao wale ambao vitumbua vyao viliingia mchanga, malimbukeni wakapata fursa ya kuchuana na wenzao na vigogo kuangushwa maksudi kutokana na namna walivyowaongoza wateuzi wao awali. Huo si mwisho! Huo ni mwanzo unaoanza mwisho yaani mwanzo wa ngoma ya uchaguzi ni lele.

Kinyang'anyiro cha kubaini mbivu na mbichi chaja mwanakwetu... Funga mkanda. Walimu kadhaa kule Shangaa waliodhamiria kubisha malango ya bunge na mabara  ya miji, vyuma vyao vi motoni...Waliupoteza uteuzi wa ubunge na sasa wamo mbioni kurudi Shangaa kuchekwa na wenzao.

Wanafunzi watawauliza maswali mengi kana kwamba ni mahojiano ya polisi, Munkari na Nakiri...Si ajabu! Baadhi yao kuwa wamekwisha poteza ajira zao. Hii ni kutokana na ukosefu wa hakikisho la usalama wao kazini.

Haijalishi nani kiongozi wako. Waswahili husema misitu ni ileile lakini nyani ndio tofauti... Wanafunzi wengi katika shule za msingi na baadhi ya zile za kibinafsi, walipata likizo ndefu na kwa hiyo, wameathirika sana kimasomo ikilinganishwa kuwa bado mwezini Machi, tarehe nne mwaka huu hali itakuwa iyo hiyo.

Shuleni Shangaa, madawati ya wanafunzi yamevunjwavunjwa. Viti vilikaliwa ndivyo sivyo, Kamusi kadha wa kadha zimeibwa. Ubaoni pameandikwa jumbe za kuwachochea wengine mbali na madaftari ya wanafunzi wengi kupotea. Mazingira ya shule ni machafu mno kwani kuna madarasa matatu ambayo sasa ni msala wa mwanadamu...!

Jamii ya nzi wanaufuata uvundo madarasani huku wanafunzi wakihofia kuingia mle hadi hali irejeshwe kawaida. Ebo! Wanadamu huajabiwa si razini, hawakosi pia hayawani... Rasilimali hizi ni mali ya wanafunzi, walimu na shule kwa jumla. Huenda IEBC ikaingia mtegoni kwa kugharamia mali haya katika shule zilizohusika japo uchunguzi wa kina hulazimika fauka ya kudai pekee. Waama, sijui walikotoa chaki za kuandikia ubaoni kwa kuwa maandishi mengi ubaoni hayaelimishi katu.

Yamejaa matusi teletele kama pishi la mawele! Muda huu wa kupata mafundisho madarasani waliutoa wapi wajomba! Kweli kukaa bure kwa mkaabure ni balaa...Wapiga kura wengi waliyaharibu mazingira yale ya kusomea na sasa wanafunzi hawana pahala tosha pa kukalia.

Huzuni

Sijui, yupi wa kuongozwa kati ya mtumzima na mtoto? Sijui iwapo magavana, seneta na madiwani wa shule zilizoathirika watakuwa tayari kugharamia au hasara humfika mtu yule mwenye mabezo tu!

Fauka ya hayo, kuna wanafunzi ambao huzuni zimewajaa na kuzifunika nyuso wakishika tama, baada ya wazazi wao kunoa yaani kukosa kuteuliwa. Wanafunzi kashika tama, kuomboleza madarasani wakiustaajabia mustakabali wa wazazi wao. Enhe! Mlidhani kuingia bungeni ni kazi lelemama au jambo la ilambe pua?

Yataka uwajibikaji, hekima na kujitoa mhanga mjomba. Natumai hali ya masomo itaendelea kama kawaida. Shule ya Shangaa na matawi yake, hazina budi kuiharakisha mitaala ikiwemo silabasi kabla ya siku za utahini kuganda.

Hakika, mwaka huu una songombingo zake... Jukumu letu ni kuhakikisha amani ipo shuleni na maeneo jirani tusije tukaziathiri sekta za wenzetu waliochumia juani wakilia vivulini. Pamwe, tuwe wamoja. Tupilia mbali matabaka na makundi haramu ya kuathiri umoja wa mkenya halisi. Kazi kwako. Upo?

mzeemzim@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating