Michecheto Sangaa wanaposubiri matokeo ya KCPE

Imepakiwa Friday January 25 2013 | Na Mathias Momanyi

Kwa Muhtasari:

Siku ya Jumatatu mambo yatakuwa tebwere Shangaa kwa wapenzi watahiniwa wa mwaka uliopita. Kwa wengine mambo ni mswaki huku wengine wakiikwea milima ya jitimai.

JAMBO usilolijua ni usiku wa giza... Tamathali hii ya usemi ilichipukia pwani ya Kenya wakati ngano za wakazi wa Jomvu ziliposhamiri sana. Makanyo, sanaa na hadhi zilifundishwa sana. Vijana walionywa kutofanya maamuzi kwa pupa kama popo mla maembesakua. Hujui kwamba hujui na hutaki kukubali kuwa hujui hicho usichokijua? Utajuaje sasa kama si umbeya?

Tumewaonya walimu na wanafunzi katika shule ya Shangaa dhidi ya visa vyao vya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa, aghalabu wao hutumezea puani wakitutemea kinywani na sasa chuma chao ki motoni... Walikaidi kufuata sera mpya zilizobuniwa na baraza la mitihani nchini KNEC lakini hayo yote wakayafukia katika makaburi ya liliwala.

Siku ya Jumatatu mambo yatakuwa tebwere kwa wapenzi watahiniwa wa mwaka uliopita. Kwa wengine mambo ni mswaki huku wengine wakiikwea milima ya jitimai. Mtihani huo utatangazwa katika majengo ya Baraza la mitihani kwenye barabara ya Ikulu huku mashirika kadhaa zikiwemo shule kuwatuma wawakilishi wao kupokea matokeo hayo.

Wanafunzi shuleni Shangaa tayari wamekuwa wagonjwa...Hawali wali wakashiba! Wakila hutapika kwa hofu na riahi. Matumbojoto, wanaendesha kwa hofu na jitimai  ya bure bahasa. Vyoo vinalalamika!

Wanafunzi wa mwaka huu hawasomi kwa kuwa 'hukumu' ya wenzao itakuwa chanzo cha bidii yao masomoni. Afisi ya mkuu wa shule tayari imejaa wazazi wasio na subira wala ngoja.Wanamtafuta Fisidume kuulizia tarehe ya matokeo kwani, hawatazami runinga wala kusoma makala magazetini? Kuna wale wanaodhani kwamba mwalimu mkuu au walimu  wana kidokezo cha matokeo yao... Hasha!

Heri waisubiri siku ya 'hukumu.' Siku ambayo ukweli utadhihirika na uongo kujitenga hadharani mwanakwetu. Walimu wakuu waliozitafuna senti za wangwana, watazitemea gerezani. Wazazi waliokataa kuhudhuria vikao vya kujadili mistakabali ya wanao sasa watajuta vyanda vikiwa vinywani.

Waziri Mutula Kilonzo atachukua usukani kwa kuyasoma paruwanja matokeo huku wanahabari nikiwemo na wapigapicha wa Taifa Leo kwa hisani ya NMG na maoni ya mwananchi. Wapekuzi wa ukurasa huu wanadai kuwa Shangaa imejengewa ukuta wenye zege nzito na saruji ya kusindika kuwazuia wanahabari kuingia mle kunasa matukio mazima baada ya mitihani kutangazwa.

Hawajui kuwa, huwezi kulizuia jua kwa ungo mjomba! Kuna wale watakaosherehekea wakibebwa hangahanga. Wapo wale watakaotokwa machozi ya furaha pengine wakililia hali zao ngumu walizozipitia katika shule za msingi. Hii ni pamoja na kuamka asubuhi kwa adhabu kali za Mwalimu Katululu, viboko vikali vya kuvimbisha nyama za ulimwengu wa nyuma pamoja na kazi za sulubu bila kukamilisha kazi za ziada. Masomo ya Sanaa yanapigiwa upatu kule Shangaa kufanya vyema. Hofu inatanda katika lugha ya Kiingereza, Hisabati na Kiswahili. Wanafunzi Shangaa hupenda lugha za kwanza almaarufu mama na baba.

Wakimwona mwalimu wa Hisabati, kila mmoja huomba ruhusa kuenda msalani. Hawaithamini hesabu...Je, mfumo wa sasa uliowaruhusu wanafunzi kutumia vikokotoo katika hisabati huenda ukaikweza elimu nchini? Kutokuwepo kwa sera maalumu za kuitumia lugha ya mawasiliano, kumesababisha viwango vya lugha kudorora zaidi shuleni.

Walimu wengi hufundisha kwa lugha za mama darasani huku wakichambua kwa kina kwa kutumia mafumbo na mithali ya lugha za mama... Wamewekewa vikwazo na wakuu wao...Do! Shangaa itazama au itaelea? Masomo mengi hayajashika kasi kutokana na ukosefu wa motisha kwa walimu. Chaki hazimo.

Kufichwa

Rejista hufichwa na wanafunzi... Mishahara yao ingali ile ile na kuongezwa kwao kutategemea ufanisi wa watahini wa mwaka uliopita. Aidha, kufeli kwa watahiniwa kutawasababishia balaa mara hiyo hiyo. Afanalek! Mshahara wa mwalimu u mkononi mwa wanafunzi eti! Baraza litayatangaza matokeo ya kwanza baada ya kuusanifisha uhakiki, utahini na uboreshaji mzima wa utendakazi barazani mbali na kuwaajiri wafanyakazi wapya wakiwemo watahini chipukizi.

Mtandao wa simu na tarakilishi utakuwa umegubikwa na wimbi zito la kusakura, pindi tu baraza litakapozindua orodha na mwongozo kamili wa kufuatilia matokeo kupitia mfumo wa dijitali yaani mfumo elektroniki wa E.

Mahojiano yetu kwa watahini wa mwaka uliopita yaligonga mwamba baada ya kugundua kuwa wengi wao wamo mafichoni wakikisubiri kisu cha ngariba kuwapasha makali ya 'jando' na 'unyago.'

Simu za wazazi zimezimwa. Hawataki maswali mengi kama yale ya polisi, namna wanao walivyofanya na kufaulu...Ingawa Bwana Katululu alikiri wazi kuwa watahiniwa wake wataupasi mtihani wa Kiswahili, tajriba yake ilieleza bayana tabasamu ya ndani kwa ndani iliyojificha kwenye shavu lake la kulia.

Enhe! Sisi tunawapa tumaini jipya fauka ya kuwatakia kila lenye heri na mbinu za kuifikia mbingu katika ufanisi wao. Kila uta wa ushindi wa mwenye bidii, huangikwa.

mzeemzim@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating