Miaka yawazidia wanafunzi Shangaa

Imepakiwa Friday February 1 2013 | Na Mathias Momanyi

Kwa Muhtasari:

Shuleni Shangaa, wanafunzi wazee wenye vitambulisho wangali madarasani. Huzungumza kwa sauti ya ubeji na kumsalimu mwalimu wao kwa jina "Mzeiya". Sare zinawaruka msomaji wangu! Kutokana na urefu wao ngoringori, soksi hazifiki magotini...

UJANA ni moshi, ukienda haurudi... Hii ni methali iliyotumiwa na Wachagga wakati marika kadhaa yalipohamasishwa kuhusu umuhimu wa kuyarithi mali ya wazazi licha ya kupuuzilia mbali mila na desturi za walezi wao. Wazazi wengi na walezi wa watoto wa Kichagga walilalamikia vijana wao dhidi ya kukumbatia ujana na kuupa kisogo uzee, walikaidi kilimo katika mabonde ya mlima Kilimanjaro bila kujua kuwa siku moja wangekonga kuitwa vikongwe na wazee wa jadi.

Methali hii inawapa nuru vijana wetu kuepukana na anasa za ujanani. Raha zao huja kwa muda mfupi yaani raha za mbwa kuukalia mkia. Ipo siku wataagana na ya ujana wakiulaki uzee kwa vitanga vya mikono wazi. Nazitoa kongole zangu kwa watahiniwa wote waliotia fora nchini. Nawe uliyekosa kufaulu na mambo yakakuendea mzahule, usife moyo, usijitie kitanzi mwanangu.

Aliyekupa wewe kiti kampa mwenzio kumbi. Mungu hakupi hiki akakunyima kile. Kuishi kuna pandashuka zake. Kuna wale hawajajaaliwa kuyaona madarasa wala kuisikia sauti ya mwalimu hadharani. Kuna wengi kambini yaani wakimbizi, mayatima na chokoraa...Wanatamani kupata elimu lakini hali inawasononokea maskini! Hamwaoni? Siyaonei fahari maisha yao wala sicheki dhiki, ikabu na mizingile yao.

Tayari wamekwisha fungwa mikatale, silisili za majanga na tabu tele zenye songombingo! Mwachie Mungu awape subira maishani. Waama, mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi...

Wacheni hayo turejee Shangaa kushuhudia vifijo, raha na mbwembwe za wachache waliotia fora katika masomo yote sita katika mtihani wa KCPE 2012. Wanafunzi na walimu wao wangali wanasherehekea. Hali ya utulivu haijarejea katu! Raha imo kilelechani! Wameisahau silibasi ambayo huenda ikawaacha nyuma huku watahini wa mwaka huu wakiyanoa makali ya utahini wa mwaka 2013.

Raha imejaa karibu imwagike shuleni. Walimu walipata fursa ya kubwakia mishikaki na kunywa tembo fauka ya kuyashabikia mapuya! Madarasa yaligeuzwa hoteli maarufu ya Bwagamtwae... Wamesahau kwamba raha ikizidi sana huwa karaha mjomba? Wanafunzi wa mwaka huu ni wazee zaidi kuliko walimu wao. Wameupata ugumu mkubwa zaidi kumwelewa mwalimu wao Katululu. Hawaelewi Kiswahili wala ufasaha wake. Anawachezea mbuzi gambusi madarasani  wacheze ashakum! Wamepoteza dira katika hisabati na Sayansi.

Walimu wawili wamepata tabu kuwafundisha wanafunzi thelathini wazee... Wanafunzi wanaosoma na watoto wao, sijui nani humlipia karo mwengine... Do! Mzazi na mwana wanashindania nini? Baba akisahihishiwa, mtoto yu pembeni. Sijui wanaitanaje wote wakiwa darasani..." Wee, babu wee... Kijana Buda... Mbuyu...Mzee Kijana Mwenzangu..."

Wakisahihishiwa na mwalimu, kila mmoja huzitazama alama zao...Nasaha zikitolewa na masomo nyeti yakifundishwa, Baba na mwanawe hubaki vinywa achama na heshima kuizika. Wamekwisha vinyoa videvu vyao na sasa umri umewazingira kama pepo za chamchela. Mabega na vifua vinawatutumka kwa misuli tinginya mithili ya wanyanyua vyuma... Ebo! Huamini!

Kumsalimu mwalimu

Wanafunzi wazee wenye vitambulisho wangali madarasani. Huzungumza kwa sauti ya ubeji na kumsalimu mwalimu wao kwa jina "Mzeiya". Sare zinawaruka msomaji wangu! Kutokana na urefu wao ngoringori, soksi hazifiki magotini... Wamekiuka mazingira yale. Wakikalia madawati lazima yavunjike kutokana na uzito wao. Yarabi! Miaka mingi ni janga na uzee si kitu chema japo njia ya lazima kwa kila mmoja wetu. Kuna wale waliofeli katika mitihani yao ya darasa la saba wakatishia kujinyonga lakini Baba Mungu akakataa.

Sasa mwaka huu, hali ni mbovu Shangaa. Elimu na miaka ni suala la mjadala wa kesho hata mitondogoo... Kuna wazee ambao hufundishika japo uzee wao wameuficha stakabadhini. Kumwelimisha mzee ni sawa na kumnyonyesha bibiu na babu. Wanaobahatika huyanasa mambo madarasani kama sumaku. Taibu, elimu ni bahari, huwa sawa na taa ya kuuzagaza mwangaza gizani.

Akizungumza na wanahabari pamoja na washikadau katika sekta mbalimbali barazani, Waziri wa elimu Mutula Kilonzo amepiga marufuku kurudia kwa wanafunzi madarasani. Amewatahadharisha wazazi kubainisha umuhimu wa kisomo na kipaji cha mwanafunzi. Si wote hufeli maksudi. Baaadhi yao hufeli kwa kuurithi uvivu na kutohamasishwa na wazazi wao.

Kurudia kutamwathiri kisaikolojia japo wapo wanaoandaliwa kisaikolojia na kuafikiana na wazazi wao kabla ya kurejelea madarasani. Huu ni wakati wa kukipigania kipaji chako. Iwapo hukujaaliwa kimasomo, tumia uwezo wako kuzumbua riziki yako. Kinolewacho hupata nacho butu hupoteza. Karne zinavyozidi kusonga ndivyo hali huja na mabadiliko. Elimu ni bahari wajomba. Someni.

mzeemzim@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating