Teknolojia imepiga wengi chenga

Na Mathias Momanyi

Imepakiwa - Tuesday, March 12  2013 at  14:29

Kwa Muhtasari

Ukuaji wa teknolojia na kasi ya kuasisi vifaa vya elektroniki, tayari umewabwaga wakenya, nikiwemo. Sisemi kuwa Wakenya hawajasoma lakini hawajaifahamu vyema mikakati ya kuidhibiti mitambo.

 

UGENI si kitu chema ndugu yangu. Ukuaji wa teknolojia na kasi ya kuasisi vifaa vya elektroniki, tayari umewabwaga wakenya, nikiwemo. Sisemi kuwa wakenya hawajasoma lakini hawajaifahamu vyema mikakati ya kuidhibiti mitambo...Baadhi ya Wakenya wana pupa ya mambo. Hii ni kutokana na uhaba wa mafundi watekelezi wakati wa uchaguzi wa mwaka huu, tarehe nne, mwezi huu.

Vituo kadhaa viliathirika kikiwemo kituo cha Shangaa ambapo mahiri mmoja pekee alitegemewa kuitumia tarakilishi ya mkononi kuyaingiza na kuyasakura matokeo kwenye foleni ya wasajiliwa elfu mia mbili hamsini! Waliohitimu na kumiliki vyeti kutoka vyuovikuu mbalimbali nchini, katika sayansi ya kompyuta na programu huria, katu hawakuteuliwa wala kupata nafasi ya kuidhibiti mitambo ya BVR...Ningali nachunguza iwapo washuikadau wote walioshiriki katika kusanidi na kusakura kwenye mitambo hii iwapo walikuwa wamehitimu sawasawa. Sasa wamebaki vigeugeu kulaumiana baada ya wakenya kutozwa ushuru tosha kugharamia ununuzi wa vifaa hivi... Wacha yaishe nisichokoe makovu mjomba! Huenda nikakasirika bure nikauma mtu ndewe!

Heri mvua inyeshe tuuvune uyoga chambilecho Wazaramo... Unapoyaona baadhi ya mambo kukosa mwelekeo nchini, kunao wale huyasherehekea bila kuzitambua kombo au kasoro zake. Kuna wale wapendao mvua na jua wengine hukipenda kiangazi na ukame...Hawayafahamu matokeo yoyote au balaa zijazo na matukio yenyewe ya misimu hii.

Sasa wanafunzi wa Shangaa hawaoni athari zozote za urefu wa kuhesabu kura za mwaka 2013. Wapo barabarani wakingoja magari ya viongozi na kuyapungia mikono kihayawani. Uchumi nchini wazorota huku asilimia kubwa ya wanafunzi ikileta hasara nyumbani. Wallahi! Ukweli umebainika kuwa watoto wetu wakiwa nyumbani hula sana! Huleta hasara kubwa kuliko hasara ya panya katika ghala la nafaka. Hula kama nzige wanavyolibugunya shamba la mihogo.

Tayari magunia manne katika nyumba ya jirani mpendwa yanaenda miayo...Majirani wanaombana vibaba vya unga huku kila mmoja akimpa kasma aiwezayo. Mambo yanawaendea mvange! Vyumba vya Mpesa havifunguliwi hadi uwe mwanakwetu eti! Wimbi la uozo, maangamizo na wasiwasi ni la nini vijijini?

Shule nyingi zilizembea kuishughulikia silabasi mapema na kuharakisha ufundishaji kwa minajili ya kukidhi haja za masomo ya kipindi hiki cha muhula wa kwanza. Huenda mtihani wa mwaka huu wa KCPE na KCSE ukawa mlima wa kukwea kwa wengi aidha wengi wakianza kucheka na nyani, huenda wakavuna mabua...Tusheni zilikataliwa na waziri wa serikali ya mpito... Mtihani utatungwa kulenga mihula yote mitatu mtawalia na wenye ndoto za kusubiri mfumo kubadilika watashangaa!

Mambo mageni huwa si rahisi kuyatekeleza... Mmekwisha yaona matokeo ya BVR na mfumo mzima mpya wa 'UCHAGUZI MAMBOLEO' Wanafunzi wa mwaka 2012 waliofanya mtihani wao wa KCPE wangali nyumbani hawajaripoti shuleni. Hawajui siri ya Biolojia, Fizikia au Kemia...

Hizo kwao ni hadithi za pangu pakavu tieni mchuzi... Hawajawafahamu walimu wao wa kidato cha kwanza kulihali. Sare zao za Shangaa - shule ya Sekondari zingali mpya. Wavulana tayari wamekwisha ota ndevu kabla ya kujiunga katika kidato cha kwanza nao wasichana wanatatizika kuhimili wangali nje...

Kukaa bwete

Enhe! Hayo ndiyo masahibu ya kukaa bwete nyumbani. Kura zimekwisha na tunamtarajia mwalimu Bifwoli kujiunga na shule ya upili ya Shangaa ili aweze kushika chaki na kuwaokoa wanafunzi kwenye pembe za ubao kabla jahazi lao la masomo kuzama mithili ya Titanike. Dida amekwisha wapa nmwamko mpya! Mwalimu Kutuny aelekee kidato cha tatu akibeba kitabu cha Isimu jamii kuendeleza fasihi na machachari yake kule Bondeni. Sina habari iwapo kuna tarehe maalumu ya kurejea madarasani kwa vile mwalimu mkuu angali mashambani akipalilia mikorosho. Magari yamegoma na usalama kijijini umedorora.

Hali kule si sawa na ya mjini. Mbinu za usafiri zinazotegemewa na wengi ni punda pamoja na ngamia. Kesho itanilazimu kuibeba kamera nikiwa na mpigapicha mwenzangu Igah, kutalii janibu zote za taifa hili kuwaletea uhondo kamili kutoka mashinani hadi mijini. Nitakuwa nikihoji wafanyakazi, walimu na washikadau wa serikali ambao bado hajaripoti kazini. Wale wanaojipa likizo maksudi wataishia kunawa. Hawataupata mshahara wa bwerere katu!

Sisi tumelala ofisini tukiwaandikia makala na kuyatathmini matokeo mazima ya uchaguzi kutoka suheli mpaka hanali. Hatuna likizo mjomba! Usalama upo msisingizie zahama na fujo zisizokuwepo. Wazembe wasiopenda kuraukia masomo wala kazi wana raha ya ajabu kweli! Nchi hii huwekeza katika kilimo na nina hakika kwamba wazazi wengi wanaoyandaa mashamba kupanda na kutika mimea, hawapo tayari kungoja au kupiga kura tena wakisubiri hesabu ya siku nyingine kumi.

Salaam aleikum wangwana?