Maradhi yawashangaza walimu Shangaa

Imepakiwa Thursday April 11 2013 | Na Mathias Momanyi

Kwa Muhtasari:

Vitanda vya wanafunzi wengi Shangaa vimeshambuliwa na kunguni wanaotuliza ngozi kwenye magodoro zaidi ya mia saba. Afya za wanafunzi wengi Shangaa zinaashiria balaa na unyonge wa kustaajabisha.

MARADHI ni suna nacho kifo ni faradhi... Kawaida ni kama sheria, mwanadamu huyapitia majanga kadha wa kadha kabla ya kutimiza umri wa kuitwa MTU...  Maradhi ni mojawapo ya sehemu ya mlimwengu kupitia hadi akaitwa mtumzima. Unautambua utapiamlo, kifuakikuu, surua au ukambi na kichocho...Mjomba kumbuka namna chawa walivyokushambulia enzi zile ukiwa gwarideni kwenye jua kali la adhuhuri. Usingeficha hisia zako kamwe!

Chawa huyoo... Katokezea kwenye ukosi wa shati lako lenye nongo na ukoga mzito.

Mara kalala ndani ya shungi chafu la nywele sokotero au ndani ya mavuzi machafu yasiyoona sabuni wala marashi... Harufu ya vikojozi ndiyo raha za vimelea msomaji wangu. Hawa wadudu wajao na misimu labda ishara za ukoo. Katu! Usikubali mwanawe kukosa kushtaki koga kila siku aidha wewe kulala bila kuoga.

Uchafu ndio asili ya vimelea. Haitoshi, kunguni, funza na viroboto watamjali  mwanawe kitandani...  Tahadhari sana! Majanga ya zamani yanarejea shuleni kwa mpigo...Wadudu hawa hawana siri mwanakwetu. Raha za kuumwa ni kujikunakuna kushoto, ulimwengu wa kati na kulia... Utajikuna kwenye kwapa si kinena si shingoni si vitangani bora tu upate nafuu ya muda tu...Ajikunaye utadhani anasakata rumba bila ngoma.

Kuvumilia ni muhali. Utamwona akilegeza ulimi na kukaza meno huku macho kiyafikicha mtoto wa watu. Aumwaye huchekacheka na kujitia shughuli lakini wapi? Mficha maradhi, kilio kitamfichua haishi kuepuka...Wacha mzaha msomaji wangu turejee kule Shangaa, shule ya mheshimiwa mteule aliyeketi bungeni ilhali kwake kunaungua.

Mwanawe mheshimiwa fulani yu Shangaa. Ameathirika pakubwa na kusononeka sonone sonone! Upele umemzingira ajabu! Mwili mzima kuanzia huko mpaka kule kusikotajika maskini! Amekwisha waambukiza wanafunzi wengine na sasa shule imeandamwa na mkosi mkubwa wa upele. Wanafunzi wanaigiza kwa kujikunakuna darasani badala ya kuandika matini ubaoni.

Mwalimu amepata hali ngumu kulituliza darasa. Imekuwa vurugu kama ya siafu na mzoga.  Watoto wa Mungu wameukosa utulivu kabisa na wamekosa raha! Asiye na kucha hakosi kigunzi au kiguguta cha mahindi mfukoni. Jamani wanatokwa usaha unaopasukia vidoleni kama maziwa kwenye viwele! Do! Usimcheke aumwaye wala kilema, hata kwenu kipo... Si wakumbuka lisani za waswahili hujafa hujaumbika? Hiyo ndiyo taabu ya sasa shuleni mle mjomba. Kila tunapoizuru hatukosi mikosi pamoja vihendo vya kuandika magazetini.

Wapendwa

Naomba kuuliza swali wasomaji wapendwa; upele ni maradhi, uchafu, umaskini au kasoro ya kuzaliwa? Tusemezane ukumbini, usinijibu kwa sasa. Madaktari wamekwisha fika kule kutoa chanjo kadha wa kadha kwa minajili ya kulidhibiti janga hilo.

Tiba mbadala za asili zingali zinatekelezwa na wazuza nyumbani. Waliokosa chanjo za awali huenda nao wakahudumiwa baada ya uchunguzi mzima kukamilika. Fauka ya upele, vitanda vya wanafunzi wengi vimeshambuliwa na kunguni wanaotuliza ngozi kwenye magodoro zaidi ya mia saba. Afya za wanafunzi wengi Shangaa zinaashiria balaa na unyonge wa kustaajabisha.

 Hizi fedha za elimu zikichelewa zaidi kutumwa shuleni, hakuna huduma stahiki kwa watoto... Hivyo ndivyo walimu wakuu wanavyozembea kusingizia...Enhe! Baada ya kisa huja mkasa na ukiona zinduna ambari i papo... Misimu kama vile kipupwe huja na maradhi ya hewa yakiwemo maradhi ya mkamba. Kunao wasiwasi wa mkurupuko wa maradhi mengine, hata baada ya misala kujaa na kufurika pote.

Shule sasa yavunda ghaya ya kuvunda, hata mazingira ya kusoma yamejaa uvundo uo huo usio kifani mithili ya shombo mavuvini. Ngozi zimepauka, mashavu yamewabokoka na nzi wanawanong'ona kila kukicha.

Afya kwa wanafunzi ni haki. Tuanafaa kuyaboresha mazingira wanakosomea wanafunzi wetu. Wafanyakazi wengi pia huyalalmikia mazingira machafu lakini kilio chao huangukia viduko.

Tazama misala yenu ofisini namna ilivyojaa mpaka kila mfanyakazi anahofia kushiba. Huna pa kusaliti haja wala pa kupunguzia uzito...

mzeemzim@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating