Uchawi huanza nawe pamoja na imani yako

Imepakiwa Thursday May 2 2013 | Na Mathias Momanyi

Kwa Muhtasari:

Haimaanishi kila unapozidiwa na maradhi eti ni mwisho wa kurasa zako humu duniani. Haimaanishi kila unapomwona paka amenaswa kibuyuni kwa milio tofauti tofauti eti ni majini au maajabu ya Musa!

MARADHI ni suna kufa ni faradhi. Tamathali hii ya lugha huwapa wenye maumivu ya mwili matumaini makubwa. Kunao wale waliolazwa sadarukini yaani ' intensive care unit' Wengine wanauguza na kuaguliwa tego za uchawi mkubwa!

Je, wajua kuwa uchungu huwa kwa mfiwa?  Kila unapougua, fikra hukuelekeza kuwili. Sehemu ya kwanza ni kaburini na ya pili ni penye wosia. Utawakumbuka wote uliowakosea angalau uwape msamaha ukiyataja maghufira kabla ya toba kwa mwenyezi Mungu S.W.A... Haimaanishi kila unapozidiwa na maradhi eti ni mwisho wa kurasa zako humu duniani.

Haimaanishi kila unapomwona paka amenaswa kibuyuni kwa milio tofauti tofauti eti ni majini au maajabu ya Musa! Hizo ni fikra tu. Kwa kawaida paka huwa na milio mia moja na kumi. Uchawi huanza nawe pamoja na imani yako. Unamkumbuka Vuai katika riwaya ya Kisima cha Giningi? Katu! Jipe moyo.

Kula dengu, mboga pamoja na mchuzi wa uyoga na kuipa siha mwamko mpya. Samahani nina swali kizushi tu... Uyoga ni nyama au mboga? Iwapo ni mboga, basi,  za rangi gani? Nawaonya nyie mlao 'chipsi' maarufu vibanzi siku kwa siku. Mafuta yameganda mishipani hata kupumua ni balaa... Vitambi mmetunga pasi na kujua kuwa ni maradhi si afya.

Tumbo au kitambi cha minyoo labda. Nawaonya mlao nyama mbichi kwa tamaa na pupa. Hamkumbuki yaliyomkuta fisi kwenye safari zake zenye tamaa? Kweli hamjasoma hadithi. Anza kusoma zile za Esopo kabla ya zile za Mfalme Edipode.  Hadithi zipo vitabuni lakini si vitabu vya sasa vinavyoandikwa kwa dakika sitini na kuchapishwa kwa siku mbili. Utavijua barabarani vikiuzwa kwa bei ya njugu. Wacha hayo...

Naelekea kwa mwalimu Mkuu kumjulia hali. Mwalimu Fisidume. Zee lenye sharafa na ndevu ndefu mithili ya bwenzi la mbuzi. Shule ya Shangaa yakaribia kufunguliwa ijapokuwa majengo kadhaa yalitishiwa na mafuriko makubwa. Maradhi yamemteka mwalimu wa watu mzimamzima. Kadhoofika mno! Hukohoa kikohozi sugu chenye uzito wa gundi. Mashavu yamembokoka na mboni sasa zinachungulia vikawani.

Enhe! Maradhi hayo siyajui wala sitamani kuyabashiri. Kunayo mengi ambayo huja na misimu. Tulipomzuru mapema wiki iliyopita, alikuwa amelazwa katika hospitali kuu ya wilaya ya Kakamega. Familia ilimzingira kumtakia ashekali. Nafurahia kuwa huenda ukamwona wiki ya kwanza kazini, akiwa bukheri wa hamsa wa ishirini. Hapendi kukaa nyumbani. Anaitumikia shule kwa dhati si chati za kisebusebu kijoyo ki papo. Japo wanafunzi wengi wanamwogopa, hachelei kutenda haki shuleni.

Kofi

Angali kipenzi cha wengi na kila anapokosa shuleni, utasikia fulani kamzaba mwenziwe kofi, darasa fulani kazua patashika na wanafunzi kutorokea uani... Fisidume huogopwa kama shetani. Walimu wengi huzembea kazini kila anapokosa kufika shuleni. Mkono wake wenye mishipa umekaukiana ajabu!

Kazaliwa na ukali mtamu. Kila aishikapo chaki, ubao hutetemeka tetematetema! Si temtem au tetemtem wanavyosema waandishi bandia. Fasili ya kiigizi hicho imo kamusini. Tetema ni kitenzi kitokanacho na nomino mtetemeko.

Kwa hiyo, tuwe waangalifu tuandikapo insha zetu. Walimu kadha wa kadha watashika hatamu za kuzikagua kazi zenu za ziada baada ya likizo ya kipupwe kumalizika. Mlipokelewa kwa mvua za masika na huenda mkarudi nazo. Naipa Shangaa pole pamoja na wizara nzima ya elimu kwa kumpoteza waziri wao wa elimu; Mwanasheria Mutula Kilonzo. Maombolezo hayo yatasindikizwa kwa bendera kupepea nusu milingoti shuleni kwa muda wa wiki moja.

Sera za elimu Shangaa zinafaa kuboreshwa zaidi. Yeyote atakayethubutu kukaidi sheria zilizowekwa na mabaraza ya elimu pamoja na wizara, basi, mambo yataiendea Shangaa yombo.

Nawatakia wanafunzi wote ufunguzi mwema wa shule. Pawepo na uwajibikaji kazini tukikumbuka kwamba; Kazi mbi si mchezo mwema. Heri. Asalaam aleikum?

Share Bookmark Print

Rating