Uhuru asiwapite wakazi wa kaskazini anapowazuru wengine

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Sunday, June 21  2015 at  13:36

Kwa Muhtasari

Ningefurahi sana kumuona Rais Kenyatta akizuru na kukizindua hospitali ya kisasa Mandera, Lodwar au hata mjini Marsabit ambako ingawa hakuna kura nyingi, wakazi hutatizika zaidi.

 

SERIKALI ya Jubilee imejizatiti sana kuzindua miradi pande mbalimbali za nchi katika juhudi za kuimarisha maisha ya wananchi.

Tumeshuhudia Rais Uhuru Kenyatta na Naibu William Ruto wakizindua hospitali ya kisasa Machakos, wakifuatilia ujenzi wa reli ya kisasa Voi, na hata kuzindua mradi wa kufikisha stima mashinani kwa jina Last Mile Connectivity huko Matungulu.

Vituo vya Huduma Centre pia vimejengwa kwa wingi katika miji mikuu na kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali kwa wananchi.

Serikali inafaa kupongezwa kwa haya yote. Lakini kuna kasoro moja, nayo ni kwamba maendeleo haya yote yamefanikishwa katika maeneo ambayo tayari yamekuwa mbele kimaendeleo, yaani yanafanyika Kenya.

Ikiwa hujanielewa, Kenya hapa ina maana ya maeneo ya nchi ambayo yanajihisi kuwa sehemu ya Kenya. Sijasikia hata siku moja miradi hii ya kisasa ikizinduliwa katika miji iliyo maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki, ambako wakazi tangu uhuru wamelilia uwepo wa serikali.

Kupata barabara za rami maeneo hayo huwa kisa, na wakazi husafiri mbali sana kupata huduma za afya na elimu.

Vijana maeneo hayo hutatizika sana kupata vitambulisho vya kitaifa.

Ningefurahi sana kumuona Rais Kenyatta akizindua hospitali ya kisasa mjini Mandera au hata mjini Marsabit ambako ingawa hakuna kura nyingi, wakazi hutatizika zaidi.

Vituo vya Huduma Centre pia vitafaa zaidi huko ambako wananchi wamekuwa hawawezi kupata vitambulisho na huduma nyingine muhimu. Wakazi wa Nairobi na miji mingine mikuu tayari wamekuwa wakiishi karibu na vituo vya kupokea huduma za serikali na hatua ndogo tu ya kulainisha utendakazi wa maafisa wa serikali katika afisi hizi ingetosha.

Nimeshuhudia kila Rais anapozuru eneo fulani barabara pamoja na miundomsingi mingine hukarabatiwa ili Rais asitatizike na pia kumficha soni ya eneo husika. Ukweli ni kwamba baada ya ziara hizi, Rais huwa habebi maendeleo haya na kurudi nayo Nairobi - huwa yanabaki na kuwafaa wenyeji.

Kukarabati barabara

Nina uhakika wakazi wa maeneo ya Turkana wangefurahia sana kuona tingatinga zikikarabati barabara Rais akizuru eneo hilo.

Kiongozi wa nchi anapozuru eneo fulani, huwa pia ni lazima ulinzi uimarishwe ndipo usalama wa Rais usihatarishwe. Hili hupelekea eneo husika 'kufagiliwa’ na maafisa wa usalama. Ziara kama hizi mwishowe zinaweza kuchangia kumalizwa kwa wahalifu hasa Kaskazini mashariki.

Kwa sasa ni aibu kwamba wakazi hukumbatana na magenge ya wahalifu zaidi ya wanavyokutana na Rais wao. Amealika wengi ikuluni, sasa awatembelee kwao!

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Uhuru, kujipendekeza kwa umma pekee hakutoshi

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, May 29  2015 at  16:15

Kwa Muhtasari

Vitendo vya Rais Kenyatta kujinyenyekeza na kutangamana na watu vingelitumiwa kama kigezo cha utendakazi wa Rais, basi angeibuka nambari wani. Lakini ukweli ni kwamba haya huwa ya kufurahisha macho na fikira za watu kwani baada ya hapo, wananchi hurudi kukumbana na maisha magumu na shida nyingine za dunia.

 

RAIS Uhuru Kenyatta alichaguliwa na Wakenya kuongoza taifa hili miaka miwili iliyopita kutokana na sifa zake za kutaka kutangamana na watu.

Licha ya kuzaliwa ikuluni na kutangamana na watu wenye ushawishi mkubwa nchini, ni mtu anayependa sana kujihusisha na wananchi wa kawaida.

Katita UhuRuto, kama ulivyojulikana ushirikiano wake na Naibu wake William Ruto wakati huo akiwa mgombea mwenza, wapiga kura waliona 'vijana’ wanaoweza kuwatega sikio na kusikia vilio vya wananchi.

Wengi wamedai Rais Kenyatta huwa anaiga Rais wa Marekani Barack Obama ambaye amejulikana sana kwa kutangamana sana na watu na kuwapa walinzi wake kazi ngumu.

Ninaamini hii ni sifa yake asili na wala hamuigi Obama.

Majuzi tu alikuwa muungwana kiasi cha kuwashikia mwavuli wanawake wawili wakitoka kwenye ndege baada ya mvua kunyesha wakiwasili ikuluni White House.

Hapa nyumbani, Rais alimetenda mengi. Amekaribisha watu wengi sana ikulu, wakiwemo watoto, na kwa sasa makao makuu hayo ya uongozi ambayo watu walizoea kuyatazama tu kwa mbali yamekuwa ya wananchi.

Mwaka uliopita, alipigwa picha akiwa pamoja na Ruto wakila nyama choma eneo la kawaida Kajiado. Juzi, alifika kwenye kioski na kununua soda kisha akainywa kama mwananchi wa kawaida jambo lililovutia wengi.

Haya yote yangelitumiwa kama kigezo cha utendakazi wa Rais, basi Uhuru angeibuka nambari wani. Lakini ukweli ni kwamba haya huwa ya kufurahisha macho na fikira za watu kwani baada ya hapo, wananchi hurudi kukumbana na maisha magumu na shida nyingine za dunia.

Sikushangaa nilipoona kwenye utafiti wa Ipsos-Synovate kwamba umaarufu wake umeshuka kutoka asilimia 67 Novemba hadi asilimia 48 kufikia Aprili mwaka huu.

Hizi ni dalili kwamba wananchi hawaridhishwi na utendakazi wa serikali yake. Kuna mambo mengi ambayo yanawatatiza wananchi lakini Rais haonekani kujishughulisha nayo.

Kutojali

Mwanzo ni tatizo la usalama. Wananchi wanauawa kama nzi kila pembe ya nchi. Polisi pia hawajasazwa. Alipokuwa akinywa soda Machakos, kumbukumbu za kuhangaishwa kwa maafisa wa polisi na Al-Shabaab Yumbis, Garissa mapema wiki hii zilikuwa bado akilini mwa watu.

Gharama ya maisha pia imepanda pakubwa lakini serikali yake haionekani kujali.

Mengi anayotangaza hadharani hayatekelezwi na maafisa walio mashinani. Mfano tangazo lake kwamba bei ya kuwekea watu stima ishuke hadi Sh15,000 kutoka Sh35,000. Hafahamu kuwa hata kuitishwa hizo Sh35,000 kwa wengi imekuwa ndoto.

Majuzi pia alitoa agizo kwa makurutu wafike Kiganjo, lakini siku moja baadaye Serikali ikawafukuza kituoni.

Na vita dhidi ya ufisadi nani ana matumaini? Kushughulikia haya ni bora kuliko kunywa soda!

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Jubilee imesaliti maskini kwa kupuuza maafa ya pombe

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Thursday, May 8  2014 at  11:41

Kwa Muhtasari

Hatua ambazo zinachukuliwa na serikali hii siku baada ya siku, zinabainisha kwamba hamna tofauti kubwa sana kati ya serikali hii na serikali za awali. Ni serikali ya mabwanyenye ambao lengo lao ni kuendelea kujivunia utajiri wao na mali yao.

 

WAKATI wa kampeni na hata wakati wa kutwaa mamlaka mwaka jana, muungano wa Jubilee ulijipendekeza kwa raia kama muungano wa kutetea maslahi ya maskini.

Lakini hatua ambazo zinachukuliwa na serikali hii siku baada ya siku, zinabainisha kwamba hamna tofauti kubwa sana kati ya serikali hii na serikali za awali.

Ni serikali ya mabwanyenye ambao lengo lao ni kuendelea kujivunia utajiri wao na mali yao. Uhusiano wa maskini na serikali ulifika kikomo baada yao kupiga kura Machi 4 mwaka jana na hali isipobadilika, watahitajika tena Agosti 2017.

Tukio linaloashiria ukweli wa haya ni maafa ambayo yamekumba wakazi wa kaunti za Embu, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nairobi, Kitui na Makueni ambapo watu zaidi ya 80 walifariki baada ya kubugia pombe haramu.

Kwa siku mbili, viongozi wakuu serikalini walikuwa kimya, hali tofauti kabisa na ilivyokuwa shambulio la kigaidi lilipotekelezwa kwenye duka la jumla la Westgate ambapo jamaa za Rais Kenyatta waliathiriwa.

Mashambulio ya kigaidi yanapotekelezwa mijini na mahotelini, ambapo maslahi ya matajiri yanawekwa hatarini, serikali imekuwa mstari wa mbele kujitokeza na kulaani mashambulio hayo na kuapa kwamba itakabiliana vikali na wahusika. Ajali za barabarani pia kwa kiwango fulani zimechukuliwa kwa uzito.

Lakini maskini waliokufa kwa sababu ya kunywa pombe ya Sh30? Walikuwa wanasumbuliwa na nini? Mbona hawakunywa pombe na bia rasmi zinazouzwa kwenye baa ambapo hawangehatarisha maisha? Hao ni watu waliojitakia msiba! Haya yanaonekana kuwa mawazo ya serikali, ambayo pia nimeyasikia kutoka kwa marafiki zangu. Wanachosahau ni kwamba walalahoi hawa wangetamani sana kunywa divai na bia nyingine ghali lakini uwezo hawana.

Aidha, hawakunywa Wings, Kavuthuria, Countryman na Sacramento wakijua kwamba zilikuwa na sumu. Walikuwa wamewaamini watawala kwamba wangehakikisha viwango vya kuandaa pombe hizi vinafuatwa na hivyo kuwaepusha mauti.

Machifu

Wengi wa walevi hawa pia hunywa kukimbia upweke nyumbani labda kwa sababu hawana runinga au stima ya kuwawezesha kupitisha muda wao wa jioni baada ya kazi, au kazi inapokosekana. Binadamu hawezi akakaa kwenye giza chumbani akajitumbuiza, lazima atangamane na wenzake.

Jambo linalosikitisha zaidi ni kwamba 'Hustler Nambari Moja’ Naibu Rais William Ruto ndiye aliyekuwa ameachiwa usukani wakati huu, lakini hawezi kukumbuka 'Mahustler’ wenzake.

Jambo linaloudhi ni kwamba maafisa wa serikali wa viwango vya chini, machifu na manaibu wao, ambao wengi ni walalahoi pia ndio waliofutwa. Vigogo serikalini wanaendelea kunywa mvinyo na kula vinono! Maskini ajue hana lake.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Magavana wamenoa kwa kulilia bendera

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, April 5  2013 at  11:06

Kwa Muhtasari

Magavana wameonyesha ulafi kwa kutaka kupeperusha bendera za Serikali ya Kitaifa kwenye magari yao. Inashangaza kwani bendera hizi ni za serikali ya kitaifa ambayo wenyewe wanadai kwamba hawafai kuwa wakipokea maagizo kutoka kwayo. Waunde zao inavyotakikana kisheria.

 

WAKENYA walipoidhinisha kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi Kenya na kuunda serikali za kaunti walilenga kuweka rasilimali za nchi karibu nao.

Walipanga kunufaina zaidi kutokana na viongozi ambao kwa kuwa mashinani wangeelewa shida zao vyema zaidi.

Kuwepo kwa pesa za kusambaziwa kaunti pia kungezuia baadhi ya maeneo kubaguliwa na watawala.

Lakini katika ndoto hii, kuna wachache waliokuwa na mpango tofauti - wanasiasa.

Kwa mbali, walikuwa wameona nafasi ya kujivunia nyadhifa na mamlaka kama ya rais katika kaunti zao.

Ndio maana wakati wa uchaguzi, wagombea wa vyama mbalimbali walitumia mamilioni ya pesa kwenye kampeni kuhakikisha wanaongeza Gavana kwenye majina yao.

Matukio ya siku chache zilizopita yananionyesha kwamba kinyume na matarajio ya wengi, huenda serikali za kaunti zikaendelea uovu uliotekelezwa na serikali kuu kwa nusu karne sasa tangu uhuru.

Hata kabla ya kuchukua rasmi majukumu yao, wameanza kuzozana na serikali kuu kuhusu bendera.

Mzozo umetokea baada ya Mkuu wa Sheria Githu Muigai kuwakataza kupeperusha bendera za serikali kuu na kuwaambia kuwa ni Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Mawaziri, Spika wa Bunge na Mkuu wa Sheria pekee walioruhusiwa na sheria kutumia bendera hizo.

Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Bendera na Nembo, Sura ya 99, ya Sheria za Kenya.

Magavana wamejitokeza kama watoto waliokatazwa kula keki na kudai kwamba ni haki yao.

Kila mmoja alijitetea kivyake. Gavana wa Juja William Kabogo ni mmoja wa walioteta zaidi.

Kuna waliodai kwamba wadhifa wao ni mkuu kushinda mawaziri hivyo ni haki yao.

Misongamano ya magari

Wanatetea bendera hizo kwa kuwa wanafahamu kwa mfano katika barabara za jiji, ni tiketi ya kukwepa misongamano ya magari. Hawataki maisha ya kawaida tena. Ni Waheshimiwa Watukufu!

Linaloshangaza zaidi ni kwamba bendera hizi ni za serikali ya kitaifa ambayo wenyewe wanadai kwamba hawafai kuwa wakipokea maagizo kutoka kwayo.

Watakataaje maagizo hali wanataka bendera?

Magavana wanaweza kufananishwa na mameya na wakuu wa mabaraza ya miji na wilaya ambayo yamekuwepo awali.

Walikuwa wakitumia nmfumo wa Serikali za Mitaa na rangi ya nambari za usajili za magari zina rangi ya kijani kibichi. Msimamo wangu ni kwamba hata magavana wanafaa kuundiwa mfumo wao tofauti wa kudhihirisha mamlaka na kazi yao.

Tayari kuna Sheria ya Serikali za Kaunti ambayo imeeleza wazi katika Kifungu 4(1) kuwa kila kaunti ijiundie bendela, sili, ngao ya ulinzi na nembo nyingine.

Wakuu wa kaunti ndiyo wanaofaa kufanikisha hayo, na zinafaa kutumika sawa na zile za kitaifa kuambatana ana Sheria ya Bendera, Nembo na Majina ya Kitaifa (Sura 99).

Hizi hazifai kufanana na zile za kitaifa!

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Wananchi pia wana maswali ya kujibu kuhusu uchaguzi

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, March 22  2013 at  12:48

Kwa Muhtasari

Wengi wametayarisha maswali wanayosema IEBC inafaa kujibu. Mtazamo wangu ni kwamba wananchi wenyewe na wanasiasa ndio wenye maswali makuu ya kujibu na ambao wanawajibika kwa yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu.

 

WIKI zipatazo tatu zimepita tangu Wakenya wafurike katika vituo vya kupigia kura kujiamulia viongozi wao wa miaka mitano ijayo.

Ingawa uchaguzi ulihusisha nyadhifa sita, ni uchaguzi wa urais ambao umeleta utata zaidi kukiwa na kesi tatu kuuhusu katika Mahakama ya Juu.

Ni kawaida kwa binadamu kujiuliza nini kilienda mrama baada ya shughuli yoyote kukosa kufanikiwa.

Ni kutokana na haya ambapo karibu kila mtu ambaye hakuridhika na matokeo ya uchaguzi huo na jinsi ulivyoendeshwa ameelekeza lawama kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kuna baadhi waliodai kwamba ilifanya hiana kuliko iliyokuwa Tume ya Uchaguzi (ECK).

Wengi wameenda hatua mbele na kutayarisha msururu wa maswali ambayo wanasema IEBC inafaa kujibu. Mengi yamejibiwa na yaliyosalia nadhani hayana majibu.

Mtazamo wangu ni kwamba wananchi wenyewe na wanasiasa ndio wenye maswali makuu ya kujibu na ambao wanawajibika kwa yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu.

Hata shuleni wanafunzi wanapoanguka mtihani, unapomuuliza mwalimu maswali lazima uangazie wanafunzi ambao labda ndio waliokuwa dhaifu darasani kiasi cha kutoelewa walioyokuwa wakifundishwa na mwalimu wao darasani.

La kwanza kabisa ni: Ni wangapi walikuwa tayari kukubali matokeo iwapo wangeshindwa?

Wengi wa wapiga kura walifika vituo wakiwa na msimamo kwamba hawawezi kushindwa. Walifika tayari kuthibitisha hilo kwa wapinzani wao wakuu.

Hata katika mikutano ya kisiasa, ingawa wanasiasa waliahidi kwamba wangekubali matokeo, sikumsikia hata mmoja aliyekosa kuongeza kwamba “ikiwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.”

Kwa uchaguzi huru na wa haki, wanasiasa walikuwa na maana ya haki yao kushindwa.

Hivyo, kama wangeshindwa, hawangekubali matokeo.

Sisi wapiga kura tuliwafuata katika hili. Wengi wameshangaa ni kwa nini pia kura zilizoharibika zilikuwa nyingi (108,975).

Laumu wapiga kura ambao licha ya kuwepo kwa karatasi nyingi zenye maelezo kuhusu upigaji kura, wengi walijifanya werevu na kutozisoma. Matokeo yake ni hayo.

Tofauti

Wewe binafsi ulisoma karatasi hizo? Kutojua huku huenda pia kulichangia tofauti kubwa ambayo imo kati ya kura zilizopigiwa baadhi ya nyadhifa.

Kwa wanasiasa ambao wanadai IEBC haikufanikisha uchaguzi wa haki, wajiulize kwanza: Chama chetu kilifanya uteuzi huru?

Vingi vinavyopiga domo viliongoza kwa kukiuka uamuzi wa wapiga kura na kulazimisha viongozi.

Wanasiasa wawa hawa ndio waliokuwa wabunge wakati wa kununuliwa kwa mifumo ya kiteknolojia na vifaa vya kutumiwa kusajili wapiga kura na mwishowe kutumiwa kupiga kura.

Walifanya nini kuhakikisha vilikuwa vya ubora wa hali ya juu?

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Uhuru na Ruto wateue vijana katika nyadhifa kuu

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, March 15  2013 at  12:40

Kwa Muhtasari

Matarajio yangu ni kwamba muungano wa Jubilee utatafuta wataalamu wa kuteuliwa kuwa mawaziri ambao watawezesha kutimizwa kwa ahadi nyingi walizotoa. Wakuu wake wasichague wazee waliokaa uongozini miaka mingi.

 

UCHAGUZI Mkuu ulifanyika wiki iliyopita na washindi na walioshindwa wakajulikana.

Kwa sasa, Muungano wa Jubilee umo mbioni kuunda serikali ijayo, ikiwa kesi ya Muungano wa CORD haitabadilisha mambo.

Kila baada ya uchaguzi, ni kawaida Kenya kwa washindi kusahau ahadi walizotoa na manifesto ambazo walikariria Wakenya kama nyimbo na kuangazia maslahi yao binafsi.

Waliokuwa maadui wakuu uchaguzini huwa marafiki kuwawezesha kula vyema.

Ni kawaida pia kwa viongozi waliokataliwa na wananchi kurejeshwa serikalini kupitia milango ya nyuma.

Katika muungano wa Jubilee, kuna vigogo wengi ambao walikuwa wakiwania viti vya ubunge, useneta na ugavana ambao waliaibishwa nyumbani.

Baadhi walikuwa na mkosi kwa kujipata wakienda kinyume na wimbi la kisiasa. Mfano ni Prof Sam Ongeri, Bw Najib Balala, Bw Chirau Mwakwere, Bw Kazungu Kambi, Bw Kiema Kalonzo na Bi Charity Ngilu.

Wengi walifagiliwa na kibunga cha CORD.

Ingawa muungano wa Jubilee umekuwa ukijitangaza kama muungano wa wanasiasa wa kizazi kipya au digitali, baadhi ya hawa ni wa kizazi cha analogi.

Wamekuwa serikalini kwa miaka mingi bila lolote la kujivunia. Tayari kumeibuka uvumi kwamba wengi huenda wakakabidhiwa nyadhifa za uwazi au kufanywa mabalozi na wakuu wa mashirika ya umma 'kurudisha mkono.’

Ingawa ni vyema kushukuru waliounga mkono muungano huu, si vyema kwenda kinyume na maadili na moyo wa Katiba kwani itakuwa ni sawa na kuturejesha tulimotoka.

Ahadi

Matarajio yangu ni kwamba muungano huu utatafuta wataalamu wa kuteuliwa kuwa mawaziri ambao watawezesha kutimizwa kwa ahadi nyingi walizotoa.

Ili kusawazisha, wataalamu hawa wanafaa kutoka kila jamii Kenya bila kujali ikiwa jamii hiyo iliunga mkono muungano utakaounda serikali au la.

Ni kupitia mbinu kama hizi ambapo tutaweza kustawisha nchi na pia kuangamiza ukabila.

Katika Bunge, nimesikia mapendekezo ya kumteua aliyekuwa spika Francis ole Kaparo ambaye sasa ni mwenyekiti wa chama cha URP kuwa Spika.

Ingawa ana ujuzi na anafaa kuhudumu,  sidhani kama ataongeza chochote katika serikali mpya.

Anafaa kukaa kando na kutoa tu mwelekeo kwa watakaokuwa wakiongoza nchi.

Wakuu wa Jubilee wasipofanya haya, nina wasiwasi kwamba walioyoahidi kwenye kampeni zao huenda yakabaki tu hivyo - ahadi.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Changamoto uchaguzini ni ishara za kutojiandaa vyema

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, March 8  2013 at  15:57

Kwa Muhtasari

Kila ishara zinaonyesha kwamba wakuu wa IEBC hawakutathmini maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa kina na kujiandaa kwa baadhi ya changamoto ambazo zimeshuhudiwa.

 

MGEMA akisifiwa, wahenga walinena, tembo hulitia maji. Msemo huu umejidhihirisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika usimamizi wa uchaguzi uliofanyika Jumatatu.

Tume hii inayoongozwa na Bw Ahmed Isaack Hassan kwa muda imesifiwa kutokana na utendakazi wake.

Maafisa wake wengi walihudumu katika iliyokuwa Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC) na walisimamia vyema chaguzi nyingi ndogo.

Kilele cha ufanisi wao kilikuwa kura ya maamuzi kuhusu katiba mwaka 2010 ambayo ilifana sana.

Ni katiba hii iliyopelekea kuundwa kwa IEBC na tume hiyo ikaongezewa majukumu.

Kila mmoja alifahamu kwamba Uchaguzi Mkuu wa Machi 4 ungekuwa mtihani mkubwa kwa tume hiyo.

Mara kwa mara wadau, baadhi kutoka nje ya nchi, walihimiza tume juu ya umuhimu wa kujiandaa mapema.

Tume hii, kila wakati iliahidi Wakenya kuhusu kujiandaa kwao kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.

Lakini kasoro nyingi ambazo zilishuhudiwa uchaguzini, kuanzia utata kuhusu upigaji kura na ujumuishaji wa kura zenyewe ulidhihirisha hali tofauti.

Kila ishara zinaonyesha kwamba wakuu wa IEBC hawakutathmini shughuli yote kwa kina na kujiandaa kwa baadhi ya changamoto ambazo zimeshuhudiwa.

Walipoongea kuhusu matumizi ya teknolojia katika kutambua wapiga kura na kupeperusha matokeo, hawakutilia maanani kwamba mitambo hiyo labda ingefeli au waliopewa jukumu la kuitumia kushindwa kuitumia.

Ni kutokana na hili ambapo licha ya ahadi ya matokeo ya urais kuwa yatajulikana saa 48 baada ya uchaguzi, tume hii ilikuwa bado inatapatapa gizani Jumatano jioni Wakenya wakiwa hawajui la kufanya. Mfumo wa teknolojia ulionekana kutupiliwa mbali na badala yake tukarudia usafirishaji wa matokeo hadi kituo cha kuhesabia kura kitaifa.

Aliyopitia Kivuitu

Hali hii ilikumbusha watu kuhusu mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya ECK marehemu Samuel Kivuitu mwaka 2007 na alivyohangaika kukusanya matokeo.

Matukio ya wiki hii yaliwafanya wengi kuelewa masaibu aliyopitia Bw Kivuitu 2007.

Tofauti ni kwamba wakati huu teknolojia imeimarika na taasisi za dola, mfano polisi na mahakama ni thabiti kiasi.

Kuchelewa kwa matokeo hutoa dhana kwamba kuna mtu 'anayekoroga’ kura mahali.

Ni matumaini yangu kwamba IEBC imejifunza mengi kutokana na uchaguzi huu na itajiimarisha siku za usoni.

Lakini kando na changamoto hizo, wananchi na wanasiasa kwa kiasi kikubwa waliwajibika.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Siri ya kuwa na siku njema Machi 4

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Saturday, March 2  2013 at  14:16

Kwa Muhtasari

Ukitaka siku yako iwe sawa, rauka muda wa kufunguliwa kwa vituo na kupiga kura yako kabla foleni hazijaanza kuwa ndefu. Uamuzi kuhusu nani utapigia ni wako binafsi! Kumbuka, ukipiga kura, jiendee zako nyumbani ukasubiri matokeo.

 

KAMPENI zote zinatarajiwa kufikia kikomo kesho na wananchi kusubiri hadi Jumatatu kufanya uamuzi wao kuhusu nani wanafaa kuongoza nchi hii.

Ikizingatiwa kwamba huu ni mwaka wa kuadhimisha miaka 50 tangu uhuru, na hali kwamba uchaguzi huu utafanikisha utekelezaji kikamilifu wa Katiba tuliyopitisha zaidi ya miaka miwili iliyopita kwa kuwezesha kuundwa kwa serikali za kaunti, uchaguzi huu una umuhimu mkubwa.

Ni jukumu la kila mwananchi mzalendo kuhakikisha kwamba uchaguzi huu unafanikiwa. Njia moja ni kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki kwa kutojihusisha katika udanganyifu na pia kuripoti visa hivi kwa watawala.

Pili, wananchi wana wajibu wa kudumisha amani. Imesisitizwa mara nyingi kwamba mtu akigundua kwamba haki haikutendwa uchaguzini, hakuna haja ya kuandamana au kuchochea ghasia.

Mahakama zetu zimefanyiwa mageuzi na kuimarisha kushughulikia kesi hizi. Wagombea wote wa urais tayari wameahidi kutumia mahakama zetu kutatua mizozo ambayo huenda ikazuka.

Tuliwaona wote katika mijadala ya urais wakiahidi haya na pia katika mkutano wa maombi na toba Uhuru Park Jumapili.

Njia ya tatu na ya umuhimu mkubwa ni kuhakikisha siku ya uchaguzi, mtu anafanya uamuzi wa busara. Uamuzi huu sio tu katika kuchagua wagombea mbali katika kuamua wakati wa kufika kituoni.

Serikali wiki hii ilitangaza kuwa Jumatatu itakuwa siku ya mapumziko hivyo hakutakuwa na sababu ya kusingizia kwamba mtu atakuwa akienda kazini ila tu labda kwa maafisa wa usalama, madaktari na wanahabari.

Ukitaka siku yako iwe sawa, rauka muda wa kufunguliwa kwa vituo na kupiga kura yako kabla foleni hazijaanza kuwa ndefu. Kuna msemo wa jamii moja nchini usemao, mwanzo mbaya ni wa kudungwa mkuki tu kwani utakufa kabla ya wenzako. Pia, kutangulia kula si ishara kwamba wewe ni mlafi.

Wingi wa wagombea

Kuna uwezekano mkubwa kwamba kutokana na wingi wa wagombea wanaochaguliwa, huenda foleni zikawa ndefu na wapiga kura kutumia muda mwingi kwenye debe.

Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) imesema wazi kwamba vituo vitafungwa saa 11 jioni na ni wapiga kura watakaokuwa kwenye foleni wakati huo na kuwa ndani ya vituo ambao wataruhusiwa kupiga kura. Isitoshe, kwa kuwa siku iliyotangazwa ya kupiga kura ni Machi 4, hakuna atakayeruhusiwa kupiga kura baada ya saa sita usiku kwani itakuwa tayari ni Machi 5.

Kuwa wa kupiga kura usiku kuna hatari zake na huenda hata usipate fursa. Uamuzi ni wako! Kumbuka, ukipiga kura, jiendee zako nyumbani ukasubiri matokeo.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Dawa ya ukabila si maneno na ahadi tupu

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Thursday, February 14  2013 at  15:01

Kwa Muhtasari

Ninashangaa mbona wanasiasa hawawezi kuchukulia sisi sote kuwa Wakenya wenye haki sawa. Unapoanza kudai mwingine ni mkabila, tayari unatumia mizani ya kikabila. Hata wewe unaugua!

 

UKABILA umekuwa suala kuu katika siasa na uongozi wa taifa hili. Hata kwenye mjadala wa wagombea wa urais Jumatatu, suala hili lilijadiliwa sana katika jaribio la kuangamiza ukabila.

Kila mwanasiasa anajua kuwa kubandikwa jina 'Mkabila’ ni sawa na kukabidhiwa hukumu ya kifo na ndio maana kila mmoja amekuwa akijitetea kwamba anapiga vita ukabila.

Sawa na alivyosema Kiongozi wa Narc Kenya Bi Martha Karua na aliye mwanamke wa pekee katika kinyang’anyiro cha urais, hakuna mwanasiasa yeyote ambaye atajitokeza na kukiri kwamba anaeneza ukabila.

Baada ya kufuatilia kwa kina kampeni za wagombea wanaoongoza, nimegundua kuwa wote ni wakabila na hawatatupeleka popote.

Mmoja anadai kwamba kwa sababu alisema mtu wa kabila jingine anatosha wakati mmoja, amepita mtihani wa kutokuwa mkabila.

Mwingine anajitetea kwamba amekuwa akizunguka Kenya yote kutafuta kura na hivyo hawezi kuwa anategemea kabila lake pekee.

Mwingine naye anajitetea kwa kuwapiga vita wenzake na kudai yeye pekee ndiye afaaye. Ajabu ni kwamba, usiku, anaapa na jamii yake kwamba lazima wafunze makabila mengine funzo.

Kama huamini haya, chukua kwa mfano Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka ambaye licha ya kudai alihama uliokuwa muungano wa G7 ili kupiga vita ukabila, kwenye kampeni zake mara nyingi hakosi kutaja kuhusu watu wa Ukambani.

Imani yangu ni kwamba, dawa ya ukabila miongoni mwa wanasiasa ni kuhakikisha kwamba hawaneni kuuhusu.

Ninashangaa mbona hawawezi kuchukulia sisi sote kuwa Wakenya wenye haki sawa. Unapoanza kudai mwingine ni mkabila, tayari unatumia mizani ya kikabila. Hata wewe unaugua!

Ni kweli kwamba kwa kiasi fulani, ukabila umetokana na umaskini na uchochezi na kwamba mara nyingi hutumiwa na viongozi na wanasiasa waliojilimbikizia mali na mamlaka kujilinda.

Mizizi

Kwa kupitisha Katiba Mpya zaidi ya miaka miwili iliyopita, matumaini yalikuwepo ya kuangamiza ukabila kwa kuhakikisha umaskini unapigwa vita. Maeneo yote yanahakikishiwa mgao wa haki kutoka kwa hazina ya kitaifa.

Lakini kwenye katiba iyo hiyo, kuna mizizi ya ukabila ambayo tusipochunga, itaendelea kutuandama kama kivuli.

Ingawa katiba yenyewe inasema kwamba mtu hafai kubaguliwa kwa misingi ya kikabila, katiba hiyo inaruhusu kubaguliwa kwa mfano wakati wa uajiri wa wafanyakazi wa umma kwa kuweka viwango maalum vinavyofaa kutimizwa kutoka kwa makabila mbalimbali.

Ni kutokana na hili ambapo unaweza kupata watu waliohitimu wakitaka kuteuliwa lakini kwa kuwa mtu wa kabila hilo aliteuliwa, mfano kuwa mkuu wa tume, hawawezi kupewa unaibu.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Wanasiasa wajadili sera zao kuhusu ardhi

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, February 8  2013 at  17:04

Kwa Muhtasari

Hakuna aliyekatazwa kujadili kuhusu sera ambazo atatumia kuhakikisha mamilioni wasio na ardhi wanaipata, na wale waliopokonywa wanairejesha. Lakini ni hatia kushambulia familia moja, au kundi ndogo la watu kwa sababu eti “wanamiliki ardhi kubwa.”

 

TOFAUTI kuu zimeibuka kuhusu uhalali wa kutumiwa kwa ardhi kama suala kuu katika kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

Hili limetokana na majibizano kati ya miungano miwili mikuu, Cord na Jubilee.

Mgombea urais wa Cord Waziri Mkuu Raila Odinga amenukuliwa akisema wote walionyakua mali ya umma wanafaa kuirejesha mwaka wa Jubilee (maadhimisho ya miaka 50 tangu uhuru).

Lakini yeye na Bw Moses Wetangula wameenda hatua mbele na kuonekana kulenga Bw Uhuru Kenyatta na kwa jumla familia ya mwanzilishi wa taifa, Mzee Jomo Kenyatta.

Kumekuwa na madai ambayo ukweli wake sijabaini ardhi inayomilikiwa na familia hiyo inatoshana na Mkoa wa Nyanza.

Akijibu haya, Bw Kenyatta alisema wale wenye ushahidi kwamba ardhi anayomiliki ni ya kuibwa wautoe.

Majibizano haya yamepelekea Inspekta Mkuu wa Polisi David Kimaiyo na Tume ya Utangamano na Umoja wa Kitaifa (NCIC) kuonya dhidi ya kutumiwa kwa mjadala kuhusu ardhi kuwa silaha ya kisiasa.

Tahadhari hii imechukuliwa na baadhi ya wanasiasa kuwa jaribio ya kuzima uhuru wa kujieleza na kukashifiwa vikali. Mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji wa Katiba Charles Nyachae mwenyewe amesisitiza kwamba hakuna mwenye haki ya kuzima watu wasiongee kuhusu ardhi.

Huu ni ukweli mtupu. Lakini ninaamini kuwa alicholenga Bw Kimaiyo ni kutumia matamshi ya kiholela kuhusu ardhi kuchochea hisia za wananchi.

Hakuna aliyekatazwa kujadili kuhusu sera ambazo atatumia kuhakikisha mamilioni wasio na ardhi wanaipata, na wale waliopokonywa wanairejesha.

Lakini ni hatia kushambulia familia moja, au kundi ndogo la watu kwa sababu eti “wanamiliki ardhi kubwa.”

Nilishangaa Bw Odinga aliposema majuzi kwamba Bw Kenyatta anafaa kugawia ardhi wale wasio na ardhi ikiwa kweli ana moyo wa kuwasaidia.

Kwa kusema hivi, bila shaka, alilenga kuonyesha uchoyo na kukosa utu kwa Bw Kenyatta. Lakini ukweli ni kuwa, kuwa tajiri si kosa. Katiba, inampa kila Mkenya haki ya kumiliki ardhi.

Utu

Aliposema hivyo, Bw Odinga mwenyewe hakusema anamiliki kiasi gani cha ardhi. Isitoshe, hawezi hesabiwa kuwa miongoni mwa maskini na hajagawia maskini sehemu ndogo ya mali anayomiliki kuonyesha utu.

Hata vijijini, si wote walio sawa katika umiliki wa ardhi. Wapo wenye ekari zaidi ya 10, na wengine wasio pa kujenga kibanda.

Hakuna asiyejua kwamba kwa kiwango fulani vita vya kikabila Rift Valley vilichochewa na ardhi. Kuna waliodhani wakifukuza wenzao watatwaa ardhi wanayomiliki. Hatutaki kurudi huko.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Kalonzo alinoa kuhusu maafisa wa utawala wa mkoa

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, February 1  2013 at  11:44

Kwa Muhtasari

Kwa kudai kwamba kuna njama ya kutumia idara nzima ya utawala wa mkoa kusaidia muungano wa Jubilee katika kampeni Bw Kalonzo Musyoka anawaweka hatarini maelfu ya maafisa ambao wamo kila pembe ya nchi kuhakikisha haki, usalama na amani.

 

TANGU aungane na Waziri Mkuu Raila Odinga, na Bw Moses Wetangula na kuunda muungano wa Coalition for Reforms and Democracy (CORD), Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka amebadilika pakubwa.

Kinyume na alivyofahamika awali kama mtu asiyekuwa na msimamo mkali, siku hizi ana ujasiri na anaonekana kuwa na lengo moja tu, nalo ni kuhakikisha mrengo huo unashinda urais.

Hili huenda limetokana na imani kuwa mrengo wake utashinda uchaguzi jambo ambalo ni la busara kwa kila aliye kinyang’anyironi kwani hali ingekuwa kinyume, mgombea hawezi kupata nguvu za kuendelea kujipigia debe.

Lakini katika ujasiri huu, wakati mwingine amejisahau na kutoa matamshi ambayo badala ya kujenga taifa analopanga kuendelea kuongoza, huenda yakalisambaratisha.

Majuzi kwenye mkutano wa kisiasa North Rift alilalamika hadharani kuhusu alichodai kuwa ni njama ya mrengo pinzani wa Jubilee ya kutumia maafisa wa utawala wa mkoa kujipigia debe. Alidai baadhi ya wakuu wa wilaya wamepokea maagizo ya kuendesha kampeni za muungano huo pinzani.

Siku chache baadaye, alijaribu kutia msingi madai yake kwa kugusia kisa cha Othaya amabpo baada ya utata kukumba uteuzi wa chama cha TNA, maafisa wa utawala wa mkoa walihamishwa.

Kulikuwa na madai kutoka baadhi ya watu kuwa walikuwa wameagizwa na 'watu fulani’ wahakikishe kwa hali na mali kuwa Bi Mary Wambui hapati tiketi hiyo.

Kisa hicho kinaonekana kumuondolea ila Bw Musyoka lakini ukweli ni kwamba alitekeleza kosa kubwa.

Kwa kurejerea idara nzima ya utawala wa mkoa, alikuwa amewaweka hatarini maelfu ya maafisa ambao wamo kila pembe ya nchi kuhakikisha haki, usalama na amani.

Hakuna asiyekumbuka yaliyowasibu baadhi ya maafisa wa polisi waliotumwa baadhi ya maeneo wakati wa uchaguzi mkuu.

Walidaiwa kuwa maajenti wa mrengo mmoja wa kisiasa na kushambuliwa.

Ni kweli kwamba wakati huu kutokana na hatari za kiusalama, kuna baadhi ya wakuu wa wilaya na maafisa wa polisi watakaohamishwa. Polisi huenda wakatumwa kuimarisha doria maeneo yanayoonekana kuwa hatarini zaidi ya kukumbwa na machafuko.

Maajenti

Kutokana na matamshi ya Bw Musyoka, ni rahisi sana kwa wananchi kuwachukulia kuwa maajenti wa mrengo pinzani na kuwashambulia.

Huu ni mwelekeo ambao nchi hii haifai kuchukua. Badala ya kupayuka hadharani, Bw Musyoka, kama mwananchi mzalendo alifaa kuwasilisha madai haya na ushahidi kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili hatua ichukuliwe.

Waziri wa Usalama Katoo ole Metito tayari amemjibu na kumtaka atoe ushahidi.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Sheria mpya, nyani wale wale, vifo zaidi

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, January 4  2013 at  11:18

Kwa Muhtasari

Suluhisho la kupunguza ajali za barabarani ni kusafishwa kabisa kwa kikosi cha polisi kutoka juu kuelekea chini. Wakati umefika kwa wakuu kuchukulia kwa uzito ripoti za ulaji rushwa zinazotolewa na raia wazalendo kila siku wanapopitia katika barabara hizi.

 

MWANZONI mwa mwezi uliopita, wengi walisubiri kwa hamu na ghamu kuanza kutekelezwa kwa Sheria Mpya za Trafiki. Adhabu kali zilizopendekezwa kwa wanaokiuka sheria za barabarani zilifanya wengi kudhani kwamba hatimaye nidhamu ingerejea barabarani.

Kabla ya mwezi kuisha, habari zilitokea kwamba mwezi huo ulikuwa umeshuhudia ajali chache ikilinganishwa na miezi sawa miaka ya nyuma. Kwa hili, tukadhani kwamba tumefika nchi ya ahadi. Tulijidanganya. Ukweli ni kwamba, kwa kubadilisha sheria, tulikuwa tumebadilisha msitu lakini nyani walikuwa ni wale wale.

Maafisa wa polisi ni wale wale, madereva na manamba wale wale, na abiria wale wale wenye haraka ya kutaka kufika waendako.

Ni kutokana na hili ambapo tumegutushwa kutoka usingizini na habari za ajali za kuhuzunisha zilizotokea punde tu baada ya kuvuka mwaka. Siku ya kwanza, watu 12 waliangamia Salgaa, ya pili 19 wakafa Molo na sita Meru.

Katika kipindi kifupi, tukawa tumepoteza takriban watu 50 na kuanza kwa kishindo safari ya kutimiza 'lengo letu’ la watu 3,000 kufa kila mwaka barabarani na wengine zaidi ya 6,000 kulemazwa.

Tayari Msemaji wa Serikali, Muthui Kariuki amepata kibarua cha kwanza mwaka mpya cha kulaani ajali hizo. Wizara ya Uchukuzi msimu wa sikukuu imekuwa ikipeperusha matangazo ya kutahadharisha watu kuhusu umuhimu wa kutii sheria za trafiki. Hizi zote ni hatua nzuri lakini ukweli ni kwamba haziwezi kubadili hali katika barabara zetu.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba wale wanaofaa kutuongoza katika kutii sheria ndio wanaoongoza kuzikiuka.

Msimu uliopita, maafisa wa trafiki wametajirika pakubwa kutokana na magari ambayo yamekuwa yakisafirisha watu mashambani na kurudi.

Hili halikubadilika hata baada yao kupata mkuu mpya. Ulaji rushwa unaendelea hata katika barabara za miji mikuu mbele ya wakuu wa trafiki.

Kwao, Sh50, kutoka kwa kila gari ni muhimu kuliko kazi waliyopewa na maisha ya watu.

Vizuizi barabarani

Madereva na hasa wa matatu wamegundua hili na huwa hawana haya kubeba abiria kupita kiasi hata wanapopitia vizuizi vya polisi kwani wanajua haja kuu ni pesa. Hivi, maisha ya Wakenya hunadiwa kama Yuda alivyomnadi Yesu.

Na usiseme ni umaskini kwani kunao maskini zaidi kuwashinda na hawawi wakatili kiasi hiki.

Suluhisho litatokana na kusafishwa kabisa kwa kikosi cha polisi kutoka juu kuelekea chini.

Wakati umefika kwa wakuu kuchukulia kwa uzito ripoti za ulaji rushwa zinazotolewa na raia wazalendo kila siku wanapopitia katika barabara hizi.

Wakiwajibika na kuchukulia hatua wanaovunja sheria bila huruma inavyotakikana, nidhamu itarejea.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Sera si kusema tu, ni kutenda

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, December 28  2012 at  11:07

Kwa Muhtasari

Kila uchao, tunawasikia wagombea wakuu wakiahidi kuwa kampeni zao zitaangazia sera. Lakini hakuna hata mmoja ambaye amekuwa akifanya hivyo na wimbo umekuwa ule ule wa ukabila, umri, vijana, wanawake na mageuzi.

 

WANASIASA ni watu wajeuri sana. Wamegundua kwamba Wakenya wamechoshwa na siasa za zamani za kugawanywa kwa misingi ya ukabila na asili na wamebadili mbinu.

Wanajua kwamba Wakenya wangependa kusikia yale watakayotekeleza watakapoingia mamlakani.

Wanatumia maneno matupu kutugawanya kama walivyofanya tangu tujinyakulie uhuru.

Kila siku utawasikia vigogo wa Jubilee na Cord wakizomeana, kila mmoja akidai mwenzake anafuata siasa duni.

Kila siku, tumewasikia Waziri Mkuu Raila Odinga, Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta, Mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto, Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na wengine wengi wakiahidi kuwa siasa zao zitaangazia sera.

Lakini kesho hiyo ya kuangazia sera ni kana kwamba haijatimia.

Badala yake, wamegeuza masuala yasiyo na maana kwa mfano umri kuwa mjadala mkali.

Mara wanasiasa wakongwe hawana mapya ya kuletea Wakenya na hivyo wanafaa kwenda nyumbani. Wameenda kiasi cha kujaribu kufafanua maana ya maneno 'analogi’ na 'dijitali.’

Wengine sijui msichague yule na yule eti wana kesi, na wengine eti wapinzani wangu ni wakabila.

Haya yanaweza kuandikwa kwenye kitabu na yasitoshee, na ukweli ni kwamba hawawezi kusaidia kiongozi yeyote kutimiza Ruwaza ya 2030.

 Tunataka kusikia mipango yao kwa kina na yale ambayo watatenda kinyume na mipango ambayo imetekelezwa kwa sasa.

Vile vile kwa wanawake. Wengi wanaongea tu kuhusu kuwapa pesa za kuanzisha biashara lakini hili limekuwepo kwa sasa. Ikiwa ni suala la kutoa mikopo bila riba, wametathmini athari kwa sekta ya benki nchini na watachukua hatua gani kuhakikisha sekta hiyo haiporomoki.

Suala la ardhi

Kuhusu ardhi, tunataka kujua sera zitakazotumiwa kuhakikisha maskwota wanapata makao na wale waliopokonywa ardhi kurejeshewa.

 Ikiwa ni suala la kuwafidia wenye mashamba haya, pesa zitatoka wapi na watakaofidiwa ni wangapi kuhakikisha maskwota wote wanapata ardhi.

Elimu imekuwa bila malipo msingi na upili, lakini wanafunzi wa maskini hawajafaidika kwani viwango ni duni. Ni mikakati ipi viongozi hawa watarajiwa watatumia.

Kuna mpango wa bima unaoumiza maskini. Lakini hospitali pia zahitaji pesa.

Kujitokeza kwa viongozi hawa kufafanua kuhusu masuala haya ndiko kutakakobadilisha siasa zetu.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Misukosuko Jubilee ni matokeo ya ubinafsi

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, December 21  2012 at  10:28

Kwa Muhtasari

Vitimbi katika muungano wa Jubilee vimenifanya kukubaliana na Kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua kwamba miungano yote iliyofanywa kabla ya uchaguzi mkuu haikuwa na azma ya kulinda maslahi ya Wakenya.

 

MATUKIO katika muungano wa Jubilee yanaweza tu kuelezwa kama kitimbi na najua bila shaka kimechekesha maadui wa muungano huu na kuudhi wafuasi.

Muungano huu ambao ulikuwa wa kwanza kuundwa, umekabiliwa na misukosuko hasa kuhusu uamuzi wa nani kati ya Musalia Mudavadi na Uhuru Kenyatta atakuwa mgombea wa urais. Wote hawa kwa sasa ni manaibu wa waziri mkuu.

Awamu za mwanzo, vyama vikuu vilivyohusisha muungano huu vilikuwa United Republican Party na The National Alliance vyao William Ruto na Bw Kenyatta mtawalia. Hivi viliafikiana Bw Kenyatta awe mgombea na Bw Ruto mgombea mwenza.

Kufika kwa Bw Mudavadi kulibadilisha mambo na inadaiwa kwamba ndipo akubali kuingia kwenye kapu, Bw Kenyatta alikuwa amekubali kumwachia nafasi ya kuwania urais.

Lakini habari hizo zilipofikia chama cha TNA, wajumbe wake walisisitiza lazima wajumbe wa vyama waamue.

Hili halikufurahisha Bw Mudavadi ambaye licha ya kusisitiza hata alipokuwa ODM kwamba anataka wengi waamue, alisisitiza kwamba mkataba wake na Bw Kenyatta uheshimiwe na akabidhiwe tiketi.

Bw Kenyatta naye alikuwa na wakati mgumu kufafanulia wanachama wa TNA yaliyojiri hadi akatia saini mkataba, na ni hapo aliposema alishinikizwa na watu fulani. Aligusia kuhusu hata 'shetani.’

Ni vituko hivi ambavyo vinadhihirisha kwamba siasa Kenya hazijabadilika na itachukua muda mrefu sana kwa hali kubadilika.

Usisahau kwamba wawili hawa mnamo 2002, ambao ni mwongo mmoja tu uliopita, waliungana na kujaribu kuingia ikulu kwa kutumia mtumbwi wa Kanu uliokuwa tayari umetoboka mashimo.

Kuungwa mkono

Mzozo kati yao unasababishwa na imani ndani ya kila mmoja kwamba ni lazima awe ndiye wa kuungwa mkono. Ni dhana hii ambayo ilipelekea Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka kuwatoroka.

Kwao, hawawezi kutafakari kwamba wakibaki pamoja, wana fursa ya kila mmoja kuongoza miaka mitano, bila umri kuwapiga chenga. Sasa, huenda wakakosa yote.

Mzozo wao kuhusu mkataba unatukumbusha kuhusu yaliyokumba muungano wa NARC muda mfupi baada ya kushinda uchaguzi wa 2002 na ni bahati kwamba unatokea kabla ya uchaguzi.

Aidha, vitimbi hivi vimenifanya kukubaliana na Kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua kwamba miungano yote iliyofanywa kabla ya uchaguzi mkuu haikuwa na azma ya kulinda maslahi ya Wakenya. Lengo ni kuhakikisha tu viongozi husika wanapata mamlaka. Wananchi wataendelea 'kuomba serikali’ na kuimba 'haki yetu’ hadi waishiwe na pumzi.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Serikali ilikosa kutuma majeshi Baragoi na Garissa

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, November 23  2012 at  14:36

Kwa Muhtasari

Kutumiwa kwa wanajeshi Baragoi na Garissa kulikuwa ukiukaji wa Katiba. Nina wasiwasi kwamba huenda wanajeshi 'wakajituma’ eneo lolote Kenya hasa kipindi hiki Kenya inapoelekea uchaguzini na kuwageuka raia.

 

KATIKA kipindi cha wiki moja iliyopita, Kenya imeshuhudia hatua ya kushangaza ambapo Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) yametumwa kupambana na wahalifu.

Walitumwa kwanza Baragoi kusaidia kuandama wahuni walioua maafisa wa polisi. Baadaye, 'walijituma’ kwenda kuandama watu wanaodaiwa kuua wanajeshi watatu mjini Garissa.

Matukio haya mawili yanaonekana yasiyo na kosa ikizingatiwa kwamba lengo kuu lilikuwa kuimarisha usalama na kurejesha uthabiti.

Lakini ukweli lazima usemwe, nao ni kwamba Katiba inayofaa kuongoza nchi ilikiukwa.

Waziri wa Usalama Katoo Ole Metito bungeni Jumatano alijaribu kutetea hatua ya kutuma wanajeshi na kusema walitumwa huko kusaidia vikosi vingine vya usalama.

Matokeo yake ni ya kusikitisha.

Ilivyo desturi ya binadamu ni kwamba kosa dogo likifanyika, huwa rahisi sana kutenda kosa kubwa.

Katiba tuliyopitisha Agosti 2010 katika Kifungu 241 (1) kinachounda KDF na Baraza la Kitaifa la Ulinzi inasema katika kijifungu 241 (3c) kwamba majeshi yanaweza tu kutuma eneo lolote Kenya kurejesha amani eneo lililokumbwa na machafuko kwa idhini tu ya Bunge.

Kaunti ya Tana River ilipoathirika, Bunge liliombwa idhini kutuma wanajeshi huko ingawa haikutolewa.

Baragoi, Baraza la Kitaifa la Usalama lilikutana chini ya Rais Kibaki na kuagiza majeshi yatumiwe. Hili halikuidhinishwa na Bunge.

Uhayawani

Baada ya kukosa wa kupiga, Garissa, wanajeshi walifika 'kulipiza kisasi’ mauaji ya wenzao bila kutumwa na yeyote kirasmi. Rais Kibaki hakutoa taarifa yoyote kuwatuma. Aidha, Waziri wa Ulinzi Yussuf Haji alinukuliwa akisema hakuwa na habari.

Ni jambo la kuhuzunisha kwamba mali iliteketezwa, wanawake kubakwa, watoto kupigwa, watu zaidi ya 48 wakajeruhiwa na wawili wakafariki wakati wa kutekelezwa kwa ukatili huo. Soko liliteketezwa pamoja na mali nyingine na kwa kifupi wakazi walijuta kuwepo kwa jeshi.

KDF imejitetea kuwa wanajeshi wake hawakutekeleza uhuni unaodaiwa lakini hili halitoshi. Wanafaa waseme nani alitenda haya walipokuwa kwenye usukani.

Wananchi wana haki pia ya kuambiwa nani aliamrisha operesheni bila kufuata sheria.

Nina wasiwasi kwamba hili lisipofanyika, huenda wanajeshi wawa hawa 'wakajituma’ eneo lolote Kenya hasa kipindi hiki Kenya inapoelekea uchaguzini na kuwageuka raia.

Kimsingi, KDF, hawana ujuzi wa kuhusiana na raia kwani hii ni kazi ya polisi.

Serikali inafaa ieleze wazi ikiwa polisi wameshindwa na kazi yao na wakuu wake wanafanya nini Kenya inapotumbukia katika uhayawani.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Vitambulisho visiwe kisingizio katika usajili

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, November 16  2012 at  11:46

Kwa Muhtasari

Ukweli ni kwamba wengi wa wanaolia kwamba hawana vitambulisho ndio wale wale wanaokosa kuvichukua vinapowasilishwa afisi za usajili wa watu wilayani na katika tarafa.

 

JUMATATU wiki ijayo, Wakenya wataanza kujisajili kuwa wapiga kurakatika Uchaguzi Mkuu mwakani.

Ni shughuli ambayo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara lakini ni habari njema kwamba hatimaye itang’oa nanga.

Ni jambo la kuridhishwa kwamba mfumo wa kisasa wa kusajili wapiga kura utatumiwa na hivyo kuzuia wafu kurudi kupiga kura tena kama walivyofanya 2007.

Hata walio hai ambao huenda wakashawishika kupiga kura mara mbili au zaidi hawatakuwa na nafasi.

Ni jukumu la kila mwananchi aliyetimiza umri wa miaka 18 na ambaye ana kitambulisho kuhakikisha anajiandikisha mapema.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imefanya jambo la busara kuruhusu watu kujiandikisha katika kituo chochote kwenye wodi hata ikiwa sicho ambacho mtu anakusudia kupigia kura yake.

Hii itawezesha hata wenye shughuli nyingi kuomba muda kazini na kuingia kituoni kwa kutumia dakika chache.

Kutokana na mzozo uliokumba maandalizi ya usajili, hakujakuwa na matangazo mengi au uhamasisho kama ifanyikavyo nyakati nyingine lakini kutokana na teknolojia za kisasa, inawezekana kufikisha ujumbe kwa wengi kipindi kifupi.

Ingawa yote yanaonekana sawa, kuna wanaolalamika kwamba hadi sasa hawana vitambulisho.

Kunao watakaotimiza umri wa miaka 18 Desemba, Januari, Februari na kadhalika na hata siku yenyewe ya uchaguzi, lakini hawatapiga kura.

Wanaharakati

Hii si sababu ya wanaharakati kukosoa shughuli yote na usajili. Kwa wale ambao walitimiza miaka 18 kitambo kidogo, Serikali imekuwa wazi na hata kuagiza vitambulisho vitolewe bila malipo.

Ukweli ni kwamba wengi wa wanaolia kwamba hawana vitambulisho ndio wale wale wanaokosa kuvichukua vinapowasilishwa afisi za usajili wa watu wilayani na katika tarafa.

Wakati mwingine hupelekwa hata afisi za machifu.

Ninawashauri wanasiasa badala ya kulia kuhusu wale wasio na vitambulisho wapige kelele zaidi kuhakikisha wale hawajachukua vyao wafike na kuvipokea.

Tusiwe walanyama wanaolilia nyasi ilihali tumeshindwa na nyama tulizo nazo.

Siku yenyewe inapokaribia, ni vyema tukumbuke kuwa kila mtu atahitajika kujisajili upya kwani hakuna aliye na kadi ya kupigia kura ya IEBC.

Wengi wetu tuna kadi za Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC) na wengine Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK).

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Kenya inahitaji kukomaa kidemokrasia kama Amerika

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, November 9  2012 at  17:49

Kwa Muhtasari

Kukomaa kisiasa kumeifanya hali Amerika kuwa kwamba wachanganuzi wanaweza kutumia vigezo vya asili na rangi kubashiri na pia kutabiri matokeo. Kura za maoni nazo huwa na ufasaha ajabu.

 

ALIPOTOA hotuba yake baada ya kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Amerika, Barack Obama alisifu nchi hiyo kama taifa kuu duniani.

Ukuu wake unadhihirika sio tu kupitia majeshi yake ambayo yamechangia kuangusha watawala dhalimu na magaidi duniani au hata uchumi wake, bali pia katika kuendeleza demokrasia.

Ni mfumo wake wa utawala ambao unafaa kuwa funzo kuu kwa mataifa mengine na hasa Kenya inayojiandaa kwa uchaguzi mkuu mwakani.

Mfumo wa uchaguzi nchini humo ni mgumu kwa wengi kuuelewa na ni ajabu kwamba katika baadhi ya nyakati, anayeongoza kwa wingi wa kura za moja kwa moja anaweza kukosa kutangazwa mshindi.

Ushindi unategemea sana kura za majimbo. Kila jimbo limetengewa kura kuambatana na wingi wa watu, lakini uamuzi wa kugawa kura hizo unategemea sheria katika jimbo husika. Mshindi anatakiwa kupata tu kura 270 za majimbo.

Kidogo mfumo huu unaonekana kutotenda haki kama tunavyoijua katika demokrasia changa lakini Waamerika wenyewe wameuheshimu na kuutumia kuendeleza uthabiti wa nchi.

Kampeni nchini humo pia huangazia zaidi sera na masuala ya umuhimu kitaifa kama vile afya, usalama na sera ya kigeni.

Haya yote hufanywa bila kusahau asili na rangi ingawa hakuna anayejitokeza waziwazi kukiri haya.

Kukomaa kisiasa kumeifanya hali Amerika kuwa kwamba wachanganuzi wanaweza kutumia vigezo vya asili na rangi kubashiri na pia kutabiri matokeo.

Vyombo vya habari navyo vinaruhusiwa kutangaza mwaniaji wanayependelea na hivyo kurahisisha mijadala ya kisiasa.

Kukubali kushindwa

Licha ya kupakana matope na kuraruana baada ya kura kupigwa Mitt Romney aliyeshindwa ingawa shingo upande alikubali kushindwa.

Ni uchaguzi huu unaotudhihirishia kwamba ikiwa tutakomaa kisiasa, tunaweza kunena kuhusu asili zetu kikabila na vyombo vya habari kupendelea wagombea.

Tunaweza kupakana matope wakati wa uchaguzi lakini baada ya wapiga kura kuamua tuendelee kuishi kwa amani kama Wakenya.

Kinyume na hali ilivyo Kenya, kura za maoni Amerika huendeshwa kwa utaalamu mkubwa. Waliofanya kura hizo hawakukosea katika kubashiri kwamba wagombea walifuatana unyounyo. Baadhi walibashiri sahihi kwamba Obama angeongoza japo kwa kura chache.

Ni hili linalofaa kufuatwa na wanaofanya tafiti za kura za maoni Kenya. Hatuwezi kuwa na imani ikiwa shirika moja litampa mgombea asilimia 30 na jingine 20. Hii ni ishara kwamba hakuna utaalamu.

Suluhu la haya yote ni kukomaa kama raia, wanasiasa na wawekezaji.

 

 

Utata kuhusu usajili wa wapiga kura ni hatari

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, October 26  2012 at  10:47

Kwa Muhtasari

Wapiga kura wasajiliwe kwa njia nyingine

 

SIKU chache zimesalia tu kabla ya mwezi wa Novemba kufika. Usajili wapiga kura imepangiwa kuanz amwezi huo.

Ni shughuli muhimu sana katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Machi 4, mwakani.

Lakini huku muda ukiyoyoma, ishara zote zinaonyesha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), haijajiandaa vya kutosha kutekeleza shughuli hii.

Yote yametokana na utata ambao umekuwepo katika ununuzi wa vifaa vya kusajili wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR).

Shughuli hii iliingia doa awali baada ya utata kuzuka kuhusu tenda yake. Serikali iliingilia kati kuokoa jahazi na kuahidi kufanikisha ununuzi ikishirikiana na serikali ya Canada.

Lakini mpango huu pia umeingizwa siasa na vifaa vyenyewe vinaingia nchini kama dawa - kwa vipimo.

Hakutakuwa na muda wa kutosha wa makarani kujifahamisha na vifaa na mitambo hiyo ikiwa ni kweli kwamba usajili utaanza mwanzoni mwa Novemba.

Iwapo itasongezwa mbele,  ratiba yote ya maandalizi ya uchaguzi itaathirika na itabidi wabunge kurekebisha sheria kuihalalisha.

Hizi zote si ishara njema kwa mkuu wa IEBC Ahmed Isaack Hassan na wenzake.

Wasipochukua hatua madhubuti huenda shughuli yote ya maandalizi ya uchaguzi ikavurugwa na wakaishia kulaumiwa kama alivyofanyiwa Mkuu wa iliyokuwa Tume ya Uchaguzi (ECK) Samuel Kivuitu.

Linalotatiza zaidi ni wanasiasa ambao wameingilia mzozo huu baadhi wakijipaka sifa za malaika.

Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga wamenukuliwa wakiwaita viongozi wa IEBC kwa mikutano.

Waziri wa Haki Eugene Wamalwa naye amedai kuna njama ya kuchelewesha uchaguzi. Upande mwingine Waziri wa Fedha Njeru Githae amedai fedha ziko za ununuzi wa vifaa na hakuna haja ya wasiwasi.

IEBC ni tume huru na inafaa kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa na upande wowote hata kama utajidai kwamba unaokoa jahazi.

Juhudi za kuisaidia ambazo zinaweza kuwa na maana njema huenda zikachukuliwa na wapinzani kama ndoa kati ya tume ya wagombea. Hii itatoa nafasi ya madai ya ubaguzi na mapendeleo na kuturejesha tulikokuwa 2007.

Msimamo wangu ni kwamba ni heri tufuate njia ndefu itakayotufikisha twendako.

Badala ya kukimbizana na BVR ambao inaonekana kujaa mashimo, ni heri hata tutumie njia ya kawaida ya kusajili wapiga kura kama alivyopendekeza Waziri wa Mipango Wycliffe Oparanya.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Idara ya polisi iheshimu haki za kibinadamu

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, October 19  2012 at  12:02

Kwa Muhtasari

Ni jambo la kuchekesha kusikia wakuu wa usalama wakisema wanatumia tu nguvu kiasi.

 

Huku mageuzi yanapofanyiwa Idara ya Polisi, itabidi watakaoyasimamia wahakikishe kwamba maafisa wanafunzwa kuheshimu haki za raia hata wanapokosa.

Si ajabu hadi sasa kwamba kila anayesikia kuhusu polisi au maafisa wengine wa usalama hujawa na mzizimo.

Walipotumwa Tana River kupokonya watu silaha, wengi wanajua yaliyojiri baadaye. Wabunge wa maeneo hayo wakiongozwa na Mbunge wa Garsen, Danson Mungatana waliokuwa wa kwanza kuitisha hata wanajeshi, ndio walioongoza kuomba maafisa hao waondolewe.

Ukweli ni kwamba polisi huwa hawabembelezi washukiwa na huwaadhibu hata kabla yao kuhukumiwa na mahakama.

Si siri kwamba haya ndiyo matukio ambayo yamewafika washukiwa wa kundi la Mombasa Republican Council ambao wamekuwa wakiandamwa kwa wiki moja sasa.

Picha za Mwenyekiti wa kundi hilo Omar Mwamnuadzi zilipoanza kusambazwa baada yake kukamatwa Jumatatu, ni wachache sana waliomtambua.

Baadhi zilimwonyesha akisaidiwa kuketi ndani ya seli ishara kwamba aliyokuwa amekumbana nayo, Mungu ndiye ajuaye. Uso wake ulijaa damu na macho yalionekana kama yaliyojeruhiwa.

Ikizingatiwa kwamba ni kiongozi wa kundi ambalo limekemewa kwa kuitisha kujitenga kwa mkoa wa Pwani na hivyo kuhatarisha umoja wa nchi, si rahisi kumwonea huruma.

Si ajabu kwamba Rais Mwai Kibaki alikuwa amesema watu kama hao wanaweza kwenda 'Jehanamu.’

Lilikuwa jambo la kuchekesha kusikia wakuu wa usalama huko wakisema walitumia tu nguvu kiasi.

Haya ni matukio ya kusikitisha ikizingatiwa kwamba waliotendewa unyama huu ni wanadamu.

Zamani, msemo kuwa 'dawa ya moto ni moto’ ulikuwa na maana, na wengine waliongeza kuwa 'amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga’. Enzi hizo, wahalifu walinyongwa au kuchomwa bila huruma.

Lakini ulimwengu umebadilika na tunaishi katika enzi ambazo haki za kibinadamu sharti ziheshimiwe.

Ndiyo maana nchi nyingi hazina hukumu ya kifo. Rais wa Gambia Yahya Jammeh majuzi alikemewa sana kwa kuitekeleza.

Haya yote yametokana na ugunduzi kwamba wakati mwingi matumizi ya ukatili huwafanya watu kuchukia dola zaidi na badala ya kubadilika kuwa wahalifu sugu.

Njia rahisi ya kutatua mizozo siku hizi huwa ni kupitia mashauriano.

pmwai@ke.nationmedia.com

 

 

Tume ilionyesha utepetevu katika chaguzi ndogo

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, September 21  2012 at  14:36

Kwa Muhtasari

Chaguzi ndogo katika maeneo bunge ya Ndhiwa, Kangema na Kajiado Kaskazini zilishuhudia visa vya ghasia, wizi wa kura na kucheleweshwa kwa matokeo. Ni matumaini yangu kwamba wakuu wa IEBC walifuatilia shughuli yote kwa makini na kwamba watarekebisha.

 

IMEBAKI miezi mitano tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, ikiwa taarifa kutoka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Uchaguzi (IEBC) na Serikali ni za kuaminika kwamba hautaahirishwa.

Lakini siku zinavyosonga, linalojidhihirisha wazi ni kwamba mengi yanahitaji kufanywa kuhakikisha Kenya inaandaa uchaguzi huru na wa haki.

Tusipojihadhari, huenda tukawa na uchaguzi usiofaa.

Hili lilidhihirishwa wazi na baadhi ya kasoro ambazo zilishuhudiwa wakati wa chaguzi ndogo Ndhiwa, Kangema na Kajiado Kaskazini Jumatatu.

Hata kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika, na hasa Ndhiwa kuliripotiwa visa vya ghasia na watu kutishwa.

Siku yenyewe, kuliripotiwa visa vya watu kujaribu kuwahonga wapiga kura kwa kutumia pesa. Kajiado, afisa wa IEBC alidaiwa kukiuka kanuni za uchaguzi akisaidia mpiga kura asiyejua kusoma na kuandika.

Wengi watasema kwamba haya yote yalitarajiwa lakini ukizingatia kwamba huu ulikuwa uchaguzi mdogo tu na usio na mengi ya kushindaniwa, ni ishara kwamba uchaguzi mkuu utashuhudia mengi.

Haya ni mambo ambayo maafisa wa tume wakishirikiana na maafisa wa usalama wanaweza kutatua na kuzuia.

Lililotia doa uchaguzi huo mdogo hata hivyo ni mwendo wa kinyonga ambao ulishuhudiwa katika kuwasilishwa kwa matokeo. Mbunge mteule wa Kajiado Kaskazini Moses ole Sakuda kwa mfano alilazimika kusubiri saa sita ndipo apewe cheti cha ushindi kutokana na kuchelewa kwa matokeo.

Katika chaguzi za awali, tume ilijizatiti kutangaza matokeo upesi kadiri yalivyopokelewa.

Lakini wakati huu, mitambo yao iliingia kasoro. Waliokuwa wakifuatilia matokeo mtandaoni walivunjwa moyo kwani hata tovuti ya IEBC wakati mmoja ilikuwa haifunguki.

Ikizingatiwa kwamba waliokuwa wakijaribu kuifikia ni wachache, ni ishara kwamba huenda ikafeli sawa na ifanyavyo ile ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kila matokeo ya mitihani ya kitaifa yanapotangazwa.

Kucheleweshwa kwa matokeo

Hili ni jambo la kuhuzunisha katika enzi hizi za kiteknolojia. Tunapoandaa mipango ya kusajili wapiga kura kwa njia ya elektroniki hatufai kusahau maeneo mengine yaliyo muhimu sana katika uchaguzi.

Itakumbukwa kwamba kucheleweshwa kwa matokeo mwaka 2007 ni miongoni mwa yaliyofanya baadhi ya watu kushuku kwamba udanganyifu ulikuwa ukitekelezwa.

Tume imejitetea kwamba ilikuwa vigumu kufikia baadhi ya maeneo hasa Kajiado na Ndhiwa.

Lakini yakilinganishwa na maeneo ya mbali kama vile Turkana, Wajir na hata Tana kama tulivyoshuhudia majuzi, huenda yalikuwa kionjo tu.

Ni matumaini yangu kwamba wakuu wa IEBC walifuatilia shughuli yote kwa makini na kwamba watarekebisha.

Tulinusurika mwaka 2007 kwa mapenzi ya Mungu na hatujui ikiwa tutabahatika mara ya pili ikiwa hatutarekebisha mienendo yetu.