Tume ilionyesha utepetevu katika chaguzi ndogo

Imepakiwa Friday September 21 2012 | Na Peter Mwai

Kwa Muhtasari:

Chaguzi ndogo katika maeneo bunge ya Ndhiwa, Kangema na Kajiado Kaskazini zilishuhudia visa vya ghasia, wizi wa kura na kucheleweshwa kwa matokeo. Ni matumaini yangu kwamba wakuu wa IEBC walifuatilia shughuli yote kwa makini na kwamba watarekebisha.

IMEBAKI miezi mitano tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, ikiwa taarifa kutoka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Uchaguzi (IEBC) na Serikali ni za kuaminika kwamba hautaahirishwa.

Lakini siku zinavyosonga, linalojidhihirisha wazi ni kwamba mengi yanahitaji kufanywa kuhakikisha Kenya inaandaa uchaguzi huru na wa haki.

Tusipojihadhari, huenda tukawa na uchaguzi usiofaa.

Hili lilidhihirishwa wazi na baadhi ya kasoro ambazo zilishuhudiwa wakati wa chaguzi ndogo Ndhiwa, Kangema na Kajiado Kaskazini Jumatatu.

Hata kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika, na hasa Ndhiwa kuliripotiwa visa vya ghasia na watu kutishwa.

Siku yenyewe, kuliripotiwa visa vya watu kujaribu kuwahonga wapiga kura kwa kutumia pesa. Kajiado, afisa wa IEBC alidaiwa kukiuka kanuni za uchaguzi akisaidia mpiga kura asiyejua kusoma na kuandika.

Wengi watasema kwamba haya yote yalitarajiwa lakini ukizingatia kwamba huu ulikuwa uchaguzi mdogo tu na usio na mengi ya kushindaniwa, ni ishara kwamba uchaguzi mkuu utashuhudia mengi.

Haya ni mambo ambayo maafisa wa tume wakishirikiana na maafisa wa usalama wanaweza kutatua na kuzuia.

Lililotia doa uchaguzi huo mdogo hata hivyo ni mwendo wa kinyonga ambao ulishuhudiwa katika kuwasilishwa kwa matokeo. Mbunge mteule wa Kajiado Kaskazini Moses ole Sakuda kwa mfano alilazimika kusubiri saa sita ndipo apewe cheti cha ushindi kutokana na kuchelewa kwa matokeo.

Katika chaguzi za awali, tume ilijizatiti kutangaza matokeo upesi kadiri yalivyopokelewa.

Lakini wakati huu, mitambo yao iliingia kasoro. Waliokuwa wakifuatilia matokeo mtandaoni walivunjwa moyo kwani hata tovuti ya IEBC wakati mmoja ilikuwa haifunguki.

Ikizingatiwa kwamba waliokuwa wakijaribu kuifikia ni wachache, ni ishara kwamba huenda ikafeli sawa na ifanyavyo ile ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kila matokeo ya mitihani ya kitaifa yanapotangazwa.

Kucheleweshwa kwa matokeo

Hili ni jambo la kuhuzunisha katika enzi hizi za kiteknolojia. Tunapoandaa mipango ya kusajili wapiga kura kwa njia ya elektroniki hatufai kusahau maeneo mengine yaliyo muhimu sana katika uchaguzi.

Itakumbukwa kwamba kucheleweshwa kwa matokeo mwaka 2007 ni miongoni mwa yaliyofanya baadhi ya watu kushuku kwamba udanganyifu ulikuwa ukitekelezwa.

Tume imejitetea kwamba ilikuwa vigumu kufikia baadhi ya maeneo hasa Kajiado na Ndhiwa.

Lakini yakilinganishwa na maeneo ya mbali kama vile Turkana, Wajir na hata Tana kama tulivyoshuhudia majuzi, huenda yalikuwa kionjo tu.

Ni matumaini yangu kwamba wakuu wa IEBC walifuatilia shughuli yote kwa makini na kwamba watarekebisha.

Tulinusurika mwaka 2007 kwa mapenzi ya Mungu na hatujui ikiwa tutabahatika mara ya pili ikiwa hatutarekebisha mienendo yetu.

Share Bookmark Print

Rating