Misukosuko Jubilee ni matokeo ya ubinafsi

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, December 21  2012 at  10:28

Kwa Muhtasari

Vitimbi katika muungano wa Jubilee vimenifanya kukubaliana na Kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua kwamba miungano yote iliyofanywa kabla ya uchaguzi mkuu haikuwa na azma ya kulinda maslahi ya Wakenya.

 

MATUKIO katika muungano wa Jubilee yanaweza tu kuelezwa kama kitimbi na najua bila shaka kimechekesha maadui wa muungano huu na kuudhi wafuasi.

Muungano huu ambao ulikuwa wa kwanza kuundwa, umekabiliwa na misukosuko hasa kuhusu uamuzi wa nani kati ya Musalia Mudavadi na Uhuru Kenyatta atakuwa mgombea wa urais. Wote hawa kwa sasa ni manaibu wa waziri mkuu.

Awamu za mwanzo, vyama vikuu vilivyohusisha muungano huu vilikuwa United Republican Party na The National Alliance vyao William Ruto na Bw Kenyatta mtawalia. Hivi viliafikiana Bw Kenyatta awe mgombea na Bw Ruto mgombea mwenza.

Kufika kwa Bw Mudavadi kulibadilisha mambo na inadaiwa kwamba ndipo akubali kuingia kwenye kapu, Bw Kenyatta alikuwa amekubali kumwachia nafasi ya kuwania urais.

Lakini habari hizo zilipofikia chama cha TNA, wajumbe wake walisisitiza lazima wajumbe wa vyama waamue.

Hili halikufurahisha Bw Mudavadi ambaye licha ya kusisitiza hata alipokuwa ODM kwamba anataka wengi waamue, alisisitiza kwamba mkataba wake na Bw Kenyatta uheshimiwe na akabidhiwe tiketi.

Bw Kenyatta naye alikuwa na wakati mgumu kufafanulia wanachama wa TNA yaliyojiri hadi akatia saini mkataba, na ni hapo aliposema alishinikizwa na watu fulani. Aligusia kuhusu hata 'shetani.’

Ni vituko hivi ambavyo vinadhihirisha kwamba siasa Kenya hazijabadilika na itachukua muda mrefu sana kwa hali kubadilika.

Usisahau kwamba wawili hawa mnamo 2002, ambao ni mwongo mmoja tu uliopita, waliungana na kujaribu kuingia ikulu kwa kutumia mtumbwi wa Kanu uliokuwa tayari umetoboka mashimo.

Kuungwa mkono

Mzozo kati yao unasababishwa na imani ndani ya kila mmoja kwamba ni lazima awe ndiye wa kuungwa mkono. Ni dhana hii ambayo ilipelekea Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka kuwatoroka.

Kwao, hawawezi kutafakari kwamba wakibaki pamoja, wana fursa ya kila mmoja kuongoza miaka mitano, bila umri kuwapiga chenga. Sasa, huenda wakakosa yote.

Mzozo wao kuhusu mkataba unatukumbusha kuhusu yaliyokumba muungano wa NARC muda mfupi baada ya kushinda uchaguzi wa 2002 na ni bahati kwamba unatokea kabla ya uchaguzi.

Aidha, vitimbi hivi vimenifanya kukubaliana na Kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua kwamba miungano yote iliyofanywa kabla ya uchaguzi mkuu haikuwa na azma ya kulinda maslahi ya Wakenya. Lengo ni kuhakikisha tu viongozi husika wanapata mamlaka. Wananchi wataendelea 'kuomba serikali’ na kuimba 'haki yetu’ hadi waishiwe na pumzi.

pmwai@ke.nationmedia.com