Sera si kusema tu, ni kutenda

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, December 28  2012 at  11:07

Kwa Muhtasari

Kila uchao, tunawasikia wagombea wakuu wakiahidi kuwa kampeni zao zitaangazia sera. Lakini hakuna hata mmoja ambaye amekuwa akifanya hivyo na wimbo umekuwa ule ule wa ukabila, umri, vijana, wanawake na mageuzi.

 

WANASIASA ni watu wajeuri sana. Wamegundua kwamba Wakenya wamechoshwa na siasa za zamani za kugawanywa kwa misingi ya ukabila na asili na wamebadili mbinu.

Wanajua kwamba Wakenya wangependa kusikia yale watakayotekeleza watakapoingia mamlakani.

Wanatumia maneno matupu kutugawanya kama walivyofanya tangu tujinyakulie uhuru.

Kila siku utawasikia vigogo wa Jubilee na Cord wakizomeana, kila mmoja akidai mwenzake anafuata siasa duni.

Kila siku, tumewasikia Waziri Mkuu Raila Odinga, Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta, Mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto, Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na wengine wengi wakiahidi kuwa siasa zao zitaangazia sera.

Lakini kesho hiyo ya kuangazia sera ni kana kwamba haijatimia.

Badala yake, wamegeuza masuala yasiyo na maana kwa mfano umri kuwa mjadala mkali.

Mara wanasiasa wakongwe hawana mapya ya kuletea Wakenya na hivyo wanafaa kwenda nyumbani. Wameenda kiasi cha kujaribu kufafanua maana ya maneno 'analogi’ na 'dijitali.’

Wengine sijui msichague yule na yule eti wana kesi, na wengine eti wapinzani wangu ni wakabila.

Haya yanaweza kuandikwa kwenye kitabu na yasitoshee, na ukweli ni kwamba hawawezi kusaidia kiongozi yeyote kutimiza Ruwaza ya 2030.

 Tunataka kusikia mipango yao kwa kina na yale ambayo watatenda kinyume na mipango ambayo imetekelezwa kwa sasa.

Vile vile kwa wanawake. Wengi wanaongea tu kuhusu kuwapa pesa za kuanzisha biashara lakini hili limekuwepo kwa sasa. Ikiwa ni suala la kutoa mikopo bila riba, wametathmini athari kwa sekta ya benki nchini na watachukua hatua gani kuhakikisha sekta hiyo haiporomoki.

Suala la ardhi

Kuhusu ardhi, tunataka kujua sera zitakazotumiwa kuhakikisha maskwota wanapata makao na wale waliopokonywa ardhi kurejeshewa.

 Ikiwa ni suala la kuwafidia wenye mashamba haya, pesa zitatoka wapi na watakaofidiwa ni wangapi kuhakikisha maskwota wote wanapata ardhi.

Elimu imekuwa bila malipo msingi na upili, lakini wanafunzi wa maskini hawajafaidika kwani viwango ni duni. Ni mikakati ipi viongozi hawa watarajiwa watatumia.

Kuna mpango wa bima unaoumiza maskini. Lakini hospitali pia zahitaji pesa.

Kujitokeza kwa viongozi hawa kufafanua kuhusu masuala haya ndiko kutakakobadilisha siasa zetu.

pmwai@ke.nationmedia.com