Sheria mpya, nyani wale wale, vifo zaidi

Imepakiwa Friday January 4 2013 | Na Peter Mwai

Kwa Muhtasari:

Suluhisho la kupunguza ajali za barabarani ni kusafishwa kabisa kwa kikosi cha polisi kutoka juu kuelekea chini. Wakati umefika kwa wakuu kuchukulia kwa uzito ripoti za ulaji rushwa zinazotolewa na raia wazalendo kila siku wanapopitia katika barabara hizi.

MWANZONI mwa mwezi uliopita, wengi walisubiri kwa hamu na ghamu kuanza kutekelezwa kwa Sheria Mpya za Trafiki. Adhabu kali zilizopendekezwa kwa wanaokiuka sheria za barabarani zilifanya wengi kudhani kwamba hatimaye nidhamu ingerejea barabarani.

Kabla ya mwezi kuisha, habari zilitokea kwamba mwezi huo ulikuwa umeshuhudia ajali chache ikilinganishwa na miezi sawa miaka ya nyuma. Kwa hili, tukadhani kwamba tumefika nchi ya ahadi. Tulijidanganya. Ukweli ni kwamba, kwa kubadilisha sheria, tulikuwa tumebadilisha msitu lakini nyani walikuwa ni wale wale.

Maafisa wa polisi ni wale wale, madereva na manamba wale wale, na abiria wale wale wenye haraka ya kutaka kufika waendako.

Ni kutokana na hili ambapo tumegutushwa kutoka usingizini na habari za ajali za kuhuzunisha zilizotokea punde tu baada ya kuvuka mwaka. Siku ya kwanza, watu 12 waliangamia Salgaa, ya pili 19 wakafa Molo na sita Meru.

Katika kipindi kifupi, tukawa tumepoteza takriban watu 50 na kuanza kwa kishindo safari ya kutimiza 'lengo letu’ la watu 3,000 kufa kila mwaka barabarani na wengine zaidi ya 6,000 kulemazwa.

Tayari Msemaji wa Serikali, Muthui Kariuki amepata kibarua cha kwanza mwaka mpya cha kulaani ajali hizo. Wizara ya Uchukuzi msimu wa sikukuu imekuwa ikipeperusha matangazo ya kutahadharisha watu kuhusu umuhimu wa kutii sheria za trafiki. Hizi zote ni hatua nzuri lakini ukweli ni kwamba haziwezi kubadili hali katika barabara zetu.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba wale wanaofaa kutuongoza katika kutii sheria ndio wanaoongoza kuzikiuka.

Msimu uliopita, maafisa wa trafiki wametajirika pakubwa kutokana na magari ambayo yamekuwa yakisafirisha watu mashambani na kurudi.

Hili halikubadilika hata baada yao kupata mkuu mpya. Ulaji rushwa unaendelea hata katika barabara za miji mikuu mbele ya wakuu wa trafiki.

Kwao, Sh50, kutoka kwa kila gari ni muhimu kuliko kazi waliyopewa na maisha ya watu.

Vizuizi barabarani

Madereva na hasa wa matatu wamegundua hili na huwa hawana haya kubeba abiria kupita kiasi hata wanapopitia vizuizi vya polisi kwani wanajua haja kuu ni pesa. Hivi, maisha ya Wakenya hunadiwa kama Yuda alivyomnadi Yesu.

Na usiseme ni umaskini kwani kunao maskini zaidi kuwashinda na hawawi wakatili kiasi hiki.

Suluhisho litatokana na kusafishwa kabisa kwa kikosi cha polisi kutoka juu kuelekea chini.

Wakati umefika kwa wakuu kuchukulia kwa uzito ripoti za ulaji rushwa zinazotolewa na raia wazalendo kila siku wanapopitia katika barabara hizi.

Wakiwajibika na kuchukulia hatua wanaovunja sheria bila huruma inavyotakikana, nidhamu itarejea.

pmwai@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating