Dawa ya ukabila si maneno na ahadi tupu

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Thursday, February 14  2013 at  15:01

Kwa Muhtasari

Ninashangaa mbona wanasiasa hawawezi kuchukulia sisi sote kuwa Wakenya wenye haki sawa. Unapoanza kudai mwingine ni mkabila, tayari unatumia mizani ya kikabila. Hata wewe unaugua!

 

UKABILA umekuwa suala kuu katika siasa na uongozi wa taifa hili. Hata kwenye mjadala wa wagombea wa urais Jumatatu, suala hili lilijadiliwa sana katika jaribio la kuangamiza ukabila.

Kila mwanasiasa anajua kuwa kubandikwa jina 'Mkabila’ ni sawa na kukabidhiwa hukumu ya kifo na ndio maana kila mmoja amekuwa akijitetea kwamba anapiga vita ukabila.

Sawa na alivyosema Kiongozi wa Narc Kenya Bi Martha Karua na aliye mwanamke wa pekee katika kinyang’anyiro cha urais, hakuna mwanasiasa yeyote ambaye atajitokeza na kukiri kwamba anaeneza ukabila.

Baada ya kufuatilia kwa kina kampeni za wagombea wanaoongoza, nimegundua kuwa wote ni wakabila na hawatatupeleka popote.

Mmoja anadai kwamba kwa sababu alisema mtu wa kabila jingine anatosha wakati mmoja, amepita mtihani wa kutokuwa mkabila.

Mwingine anajitetea kwamba amekuwa akizunguka Kenya yote kutafuta kura na hivyo hawezi kuwa anategemea kabila lake pekee.

Mwingine naye anajitetea kwa kuwapiga vita wenzake na kudai yeye pekee ndiye afaaye. Ajabu ni kwamba, usiku, anaapa na jamii yake kwamba lazima wafunze makabila mengine funzo.

Kama huamini haya, chukua kwa mfano Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka ambaye licha ya kudai alihama uliokuwa muungano wa G7 ili kupiga vita ukabila, kwenye kampeni zake mara nyingi hakosi kutaja kuhusu watu wa Ukambani.

Imani yangu ni kwamba, dawa ya ukabila miongoni mwa wanasiasa ni kuhakikisha kwamba hawaneni kuuhusu.

Ninashangaa mbona hawawezi kuchukulia sisi sote kuwa Wakenya wenye haki sawa. Unapoanza kudai mwingine ni mkabila, tayari unatumia mizani ya kikabila. Hata wewe unaugua!

Ni kweli kwamba kwa kiasi fulani, ukabila umetokana na umaskini na uchochezi na kwamba mara nyingi hutumiwa na viongozi na wanasiasa waliojilimbikizia mali na mamlaka kujilinda.

Mizizi

Kwa kupitisha Katiba Mpya zaidi ya miaka miwili iliyopita, matumaini yalikuwepo ya kuangamiza ukabila kwa kuhakikisha umaskini unapigwa vita. Maeneo yote yanahakikishiwa mgao wa haki kutoka kwa hazina ya kitaifa.

Lakini kwenye katiba iyo hiyo, kuna mizizi ya ukabila ambayo tusipochunga, itaendelea kutuandama kama kivuli.

Ingawa katiba yenyewe inasema kwamba mtu hafai kubaguliwa kwa misingi ya kikabila, katiba hiyo inaruhusu kubaguliwa kwa mfano wakati wa uajiri wa wafanyakazi wa umma kwa kuweka viwango maalum vinavyofaa kutimizwa kutoka kwa makabila mbalimbali.

Ni kutokana na hili ambapo unaweza kupata watu waliohitimu wakitaka kuteuliwa lakini kwa kuwa mtu wa kabila hilo aliteuliwa, mfano kuwa mkuu wa tume, hawawezi kupewa unaibu.

pmwai@ke.nationmedia.com