Siri ya kuwa na siku njema Machi 4

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Saturday, March 2  2013 at  14:16

Kwa Muhtasari

Ukitaka siku yako iwe sawa, rauka muda wa kufunguliwa kwa vituo na kupiga kura yako kabla foleni hazijaanza kuwa ndefu. Uamuzi kuhusu nani utapigia ni wako binafsi! Kumbuka, ukipiga kura, jiendee zako nyumbani ukasubiri matokeo.

 

KAMPENI zote zinatarajiwa kufikia kikomo kesho na wananchi kusubiri hadi Jumatatu kufanya uamuzi wao kuhusu nani wanafaa kuongoza nchi hii.

Ikizingatiwa kwamba huu ni mwaka wa kuadhimisha miaka 50 tangu uhuru, na hali kwamba uchaguzi huu utafanikisha utekelezaji kikamilifu wa Katiba tuliyopitisha zaidi ya miaka miwili iliyopita kwa kuwezesha kuundwa kwa serikali za kaunti, uchaguzi huu una umuhimu mkubwa.

Ni jukumu la kila mwananchi mzalendo kuhakikisha kwamba uchaguzi huu unafanikiwa. Njia moja ni kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki kwa kutojihusisha katika udanganyifu na pia kuripoti visa hivi kwa watawala.

Pili, wananchi wana wajibu wa kudumisha amani. Imesisitizwa mara nyingi kwamba mtu akigundua kwamba haki haikutendwa uchaguzini, hakuna haja ya kuandamana au kuchochea ghasia.

Mahakama zetu zimefanyiwa mageuzi na kuimarisha kushughulikia kesi hizi. Wagombea wote wa urais tayari wameahidi kutumia mahakama zetu kutatua mizozo ambayo huenda ikazuka.

Tuliwaona wote katika mijadala ya urais wakiahidi haya na pia katika mkutano wa maombi na toba Uhuru Park Jumapili.

Njia ya tatu na ya umuhimu mkubwa ni kuhakikisha siku ya uchaguzi, mtu anafanya uamuzi wa busara. Uamuzi huu sio tu katika kuchagua wagombea mbali katika kuamua wakati wa kufika kituoni.

Serikali wiki hii ilitangaza kuwa Jumatatu itakuwa siku ya mapumziko hivyo hakutakuwa na sababu ya kusingizia kwamba mtu atakuwa akienda kazini ila tu labda kwa maafisa wa usalama, madaktari na wanahabari.

Ukitaka siku yako iwe sawa, rauka muda wa kufunguliwa kwa vituo na kupiga kura yako kabla foleni hazijaanza kuwa ndefu. Kuna msemo wa jamii moja nchini usemao, mwanzo mbaya ni wa kudungwa mkuki tu kwani utakufa kabla ya wenzako. Pia, kutangulia kula si ishara kwamba wewe ni mlafi.

Wingi wa wagombea

Kuna uwezekano mkubwa kwamba kutokana na wingi wa wagombea wanaochaguliwa, huenda foleni zikawa ndefu na wapiga kura kutumia muda mwingi kwenye debe.

Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) imesema wazi kwamba vituo vitafungwa saa 11 jioni na ni wapiga kura watakaokuwa kwenye foleni wakati huo na kuwa ndani ya vituo ambao wataruhusiwa kupiga kura. Isitoshe, kwa kuwa siku iliyotangazwa ya kupiga kura ni Machi 4, hakuna atakayeruhusiwa kupiga kura baada ya saa sita usiku kwani itakuwa tayari ni Machi 5.

Kuwa wa kupiga kura usiku kuna hatari zake na huenda hata usipate fursa. Uamuzi ni wako! Kumbuka, ukipiga kura, jiendee zako nyumbani ukasubiri matokeo.

pmwai@ke.nationmedia.com