Changamoto uchaguzini ni ishara za kutojiandaa vyema

Imepakiwa Friday March 8 2013 | Na Peter Mwai

Kwa Muhtasari:

Kila ishara zinaonyesha kwamba wakuu wa IEBC hawakutathmini maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa kina na kujiandaa kwa baadhi ya changamoto ambazo zimeshuhudiwa.

MGEMA akisifiwa, wahenga walinena, tembo hulitia maji. Msemo huu umejidhihirisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika usimamizi wa uchaguzi uliofanyika Jumatatu.

Tume hii inayoongozwa na Bw Ahmed Isaack Hassan kwa muda imesifiwa kutokana na utendakazi wake.

Maafisa wake wengi walihudumu katika iliyokuwa Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC) na walisimamia vyema chaguzi nyingi ndogo.

Kilele cha ufanisi wao kilikuwa kura ya maamuzi kuhusu katiba mwaka 2010 ambayo ilifana sana.

Ni katiba hii iliyopelekea kuundwa kwa IEBC na tume hiyo ikaongezewa majukumu.

Kila mmoja alifahamu kwamba Uchaguzi Mkuu wa Machi 4 ungekuwa mtihani mkubwa kwa tume hiyo.

Mara kwa mara wadau, baadhi kutoka nje ya nchi, walihimiza tume juu ya umuhimu wa kujiandaa mapema.

Tume hii, kila wakati iliahidi Wakenya kuhusu kujiandaa kwao kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.

Lakini kasoro nyingi ambazo zilishuhudiwa uchaguzini, kuanzia utata kuhusu upigaji kura na ujumuishaji wa kura zenyewe ulidhihirisha hali tofauti.

Kila ishara zinaonyesha kwamba wakuu wa IEBC hawakutathmini shughuli yote kwa kina na kujiandaa kwa baadhi ya changamoto ambazo zimeshuhudiwa.

Walipoongea kuhusu matumizi ya teknolojia katika kutambua wapiga kura na kupeperusha matokeo, hawakutilia maanani kwamba mitambo hiyo labda ingefeli au waliopewa jukumu la kuitumia kushindwa kuitumia.

Ni kutokana na hili ambapo licha ya ahadi ya matokeo ya urais kuwa yatajulikana saa 48 baada ya uchaguzi, tume hii ilikuwa bado inatapatapa gizani Jumatano jioni Wakenya wakiwa hawajui la kufanya. Mfumo wa teknolojia ulionekana kutupiliwa mbali na badala yake tukarudia usafirishaji wa matokeo hadi kituo cha kuhesabia kura kitaifa.

Aliyopitia Kivuitu

Hali hii ilikumbusha watu kuhusu mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya ECK marehemu Samuel Kivuitu mwaka 2007 na alivyohangaika kukusanya matokeo.

Matukio ya wiki hii yaliwafanya wengi kuelewa masaibu aliyopitia Bw Kivuitu 2007.

Tofauti ni kwamba wakati huu teknolojia imeimarika na taasisi za dola, mfano polisi na mahakama ni thabiti kiasi.

Kuchelewa kwa matokeo hutoa dhana kwamba kuna mtu 'anayekoroga’ kura mahali.

Ni matumaini yangu kwamba IEBC imejifunza mengi kutokana na uchaguzi huu na itajiimarisha siku za usoni.

Lakini kando na changamoto hizo, wananchi na wanasiasa kwa kiasi kikubwa waliwajibika.

pmwai@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating