Uhuru na Ruto wateue vijana katika nyadhifa kuu

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, March 15  2013 at  12:40

Kwa Muhtasari

Matarajio yangu ni kwamba muungano wa Jubilee utatafuta wataalamu wa kuteuliwa kuwa mawaziri ambao watawezesha kutimizwa kwa ahadi nyingi walizotoa. Wakuu wake wasichague wazee waliokaa uongozini miaka mingi.

 

UCHAGUZI Mkuu ulifanyika wiki iliyopita na washindi na walioshindwa wakajulikana.

Kwa sasa, Muungano wa Jubilee umo mbioni kuunda serikali ijayo, ikiwa kesi ya Muungano wa CORD haitabadilisha mambo.

Kila baada ya uchaguzi, ni kawaida Kenya kwa washindi kusahau ahadi walizotoa na manifesto ambazo walikariria Wakenya kama nyimbo na kuangazia maslahi yao binafsi.

Waliokuwa maadui wakuu uchaguzini huwa marafiki kuwawezesha kula vyema.

Ni kawaida pia kwa viongozi waliokataliwa na wananchi kurejeshwa serikalini kupitia milango ya nyuma.

Katika muungano wa Jubilee, kuna vigogo wengi ambao walikuwa wakiwania viti vya ubunge, useneta na ugavana ambao waliaibishwa nyumbani.

Baadhi walikuwa na mkosi kwa kujipata wakienda kinyume na wimbi la kisiasa. Mfano ni Prof Sam Ongeri, Bw Najib Balala, Bw Chirau Mwakwere, Bw Kazungu Kambi, Bw Kiema Kalonzo na Bi Charity Ngilu.

Wengi walifagiliwa na kibunga cha CORD.

Ingawa muungano wa Jubilee umekuwa ukijitangaza kama muungano wa wanasiasa wa kizazi kipya au digitali, baadhi ya hawa ni wa kizazi cha analogi.

Wamekuwa serikalini kwa miaka mingi bila lolote la kujivunia. Tayari kumeibuka uvumi kwamba wengi huenda wakakabidhiwa nyadhifa za uwazi au kufanywa mabalozi na wakuu wa mashirika ya umma 'kurudisha mkono.’

Ingawa ni vyema kushukuru waliounga mkono muungano huu, si vyema kwenda kinyume na maadili na moyo wa Katiba kwani itakuwa ni sawa na kuturejesha tulimotoka.

Ahadi

Matarajio yangu ni kwamba muungano huu utatafuta wataalamu wa kuteuliwa kuwa mawaziri ambao watawezesha kutimizwa kwa ahadi nyingi walizotoa.

Ili kusawazisha, wataalamu hawa wanafaa kutoka kila jamii Kenya bila kujali ikiwa jamii hiyo iliunga mkono muungano utakaounda serikali au la.

Ni kupitia mbinu kama hizi ambapo tutaweza kustawisha nchi na pia kuangamiza ukabila.

Katika Bunge, nimesikia mapendekezo ya kumteua aliyekuwa spika Francis ole Kaparo ambaye sasa ni mwenyekiti wa chama cha URP kuwa Spika.

Ingawa ana ujuzi na anafaa kuhudumu,  sidhani kama ataongeza chochote katika serikali mpya.

Anafaa kukaa kando na kutoa tu mwelekeo kwa watakaokuwa wakiongoza nchi.

Wakuu wa Jubilee wasipofanya haya, nina wasiwasi kwamba walioyoahidi kwenye kampeni zao huenda yakabaki tu hivyo - ahadi.

pmwai@ke.nationmedia.com